Tanzania imepata bahati ya kuingiza timu sita kwenye mashindano ya klabu ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF), mbili kutoka Zanzibar ambazo ni KMKM na JKU, ilhali kwa Bara ni Simba, Yanga, Azam FC na Singida Fountain Gate.
Ukiachana na hilo, michezo kw atimu hizo inaanzia nyumbani na Yanga imepata bahati zaidi kwa mechi zake mbili dhidi ya Ali Sabieh ya Djibouti kucheza Tanzania.
Makocha na wachezaji wametoa mitazamo kuhusu michuano hiyo hasa kutumia vyema fursa ya kuanzia kucheza nyumbani.
KMKM v SAINT GEORGE
Imepata nafuu mchezo wa kwanza kuanzia Uwanja wa Azam Complex (nyumbani) dhidi ya Saint George ya Ethiopia - mchezo utakaopigwa Ijumaa, wiki hii.
KMKM inashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kunyakua taji la Ligi Kuu Zanzibar ikiwa chini ya kocha Hemed Suleiman ‘Morocco’ ambaye kwa sasa yupo Geita Gold, lakini kwa sasa inanolewa na kocha mpya, Masoud Djuma ambaye anasema wamejipanga vizuri wakijua michuano ina ushindani mkali.
Djuma anazungumzia maandalizi ya mashindano hayo akisema: “Ni michuano ya ushindani wa juu, lakini tunajipanga kuona ni namna gani tunaweza kutumia vyema fursa ya kucheza nyumbani.”
SINGIDA FG v JKU
Japokuwa Singida Fountain Gate inacheza Kombe la Shirikisho la Afrika kwa mara ya kwanza ndani ya kikosi kuna mastaa wenye uzoefu wa michuano hiyo ambao watakuwa na msaada mkubwa dhidi ya wengine.
Baadhi yao ni Beno Kakolanya, Joash Onyango, Thomas Ulimwengu, Meddie Kagere, Habibu Kyombo, Deus Kaseke, Dickson Ambundo na Nicholas Wadada.
Timu hiyo inaanza michuano dhidi ya JKU ya Zanzibar, mchezo utakaopigwa Uwanja wa Chamazi Complex, na makocha wanazungumzia namna utakavyokuwa na ushindani mkali.
Kocha wa Singida Fountain Gate, Hans Van der Pluijm anasema wamefanya maandalizi kuhakikisha wanafanya vizuri kwenye mchezo huo wakitambua kwamba JKU siyo ya kuibeza.
“Mechi za Ngao ya Jamii zimetusaidia kujiweka sawa. Tumecheza na timu zenye wachezaji wenye uzoefu na michuano ya CAF. Hicho kilikuwa kipimo sahihi kwa kikosi chetu. Utakuwa mchezo mgumu na wa ushindani ila naamini tutafanikiwa kupata ushindi dhidi ya JKU,” anasema.
Kipa wa timu hiyo, Beno Kakolanya anasema michuano ya CAF inahitaji kujipanga na wao wapo tayari kwa ajili ya mapambano
“Mechi za CAF zinahitaji umakini mkubwa. Naamini tutakuwa na mwanzo mzuri, kwani tumefanya maandalizi ya kutosha,” anasema Kakolanya.
YANGA v ALI SABIEH (ASAS)
Yanga inaanzia nyumbani dhidi ya Ali Sabieh ya Djibouti, mchezo utakaopigwa Jumapili, wiki hii na tayari ina uzoefu mkubwa kwani msimu ulioisha ilifika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika ikicheza dhidi ya USM Alger ya Algeria.
Ali Sabieh ndio wenyeji wa mchezo wa Jumapili na marudiano itakuwa Agosti 26 pia utachezwa Tanzania (Uwanja wa Azam Complex), hivyo Yanga imepata bahati ya kucheza michezo yote ikiwa nyumbani.
Mastaa wa Yanga wameonyesha viwango vya juu kwenye mechi iliyochezwa kwenye tamasha la Siku ya Mwananchi dhidi ya Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini ikishinda kwa mabao 1-0 na Ngao ya Jamii dhidi ya Azam FC na ikifungwa na Simba kwa penalti baada ya timu hizo kutoka suluhu.
Licha ya timu hiyo kunolewa na kocha mpya, Miguel Gamondi bado inaonekana ina muunganiko mzuri unaoweza kuisaidia kufanya vizuri kwenye michuano hiyo.
Kocha Gamondi anazungumzia hilo akisema: “Mechi za Ngao ya Jamii zimetusaidia kujiandaa kwa ajili ya CAF, itakuwa michezo migumu, ila naamini uwezo wa wachezaji wangu.”
Japokuwa ndani ya kikosi hicho aliondoka straika tegemeo, Fiston Mayele kuna Aziz Ki aliyeonyesha kiwango bora kwenye Ngao ya Jamii, hivyo anaweza kuwa msaada mkubwa.
AZAM v BAHIR DAR KENEMA
Azam FC imejiandaa vya kutosha na kambi kwa msimu huu ilipiga nchini Tunisia ambako ilicheza mechi mbalimbali za kirafiki. Ukichana na hilo imecheza mechi za Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga na Singida Fountain Gate.
Kutokana na maandalizi hayo yanaweza kuisaidia kufanya vyema kwenye Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Bahir Dar Kenema ya Ethiopia Jumapili.
Azam FC ina uzoefu na michuano hiyo na ndani ya kikosi ina maigizo mapya kama Feisal Salum ‘Fei Toto’ na Yannick Bangala waliotokea Yanga na Gibril Sillah kutoka Raja Club Athletic ya Morocco ambao ni baadhi tu ya wazoefu wa michuano ya CAF.
Kocha wa timu hiyo, Youssouph Dabo anakiri mechi za Ngao ya Jamii kumsaidia kujiandaa dhidi ya Bahir Dar Kenema. “Nimekutana na timu nzuri zimetusaidia kujiweka kwenye ushindani zaidi kwa michuano ya CAF,” anasema kocha huyo.
SIMBA v AFRICAN STAR/POWER DYNAMOS
Simba itaanzia raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa ambapo itacheza na ama African Stars ya Namibia au power Dynamos ya Zambia ambazo zitakutana katika mechi mbili za awali kabla ya mshindi kuja kukutana na Wekundu wa Msimbazi, jambo ambalo kwa sasa linampa nafasi zaidi kocha ‘ Roberto Oliveira ‘Robertinho’ kupambana kutengeneza zaidi kikosi kucheza kwa muunganiko mzuri.
Simba iliweka kambi Uturuki ambako ilicheza mechi mbalimbali za kirafiki na Robertinho aliweka wazi kwamba zilimsaidia kumjua mchezaji mmoja mmoja kwa ubora na udhaifu.
Na baada ya kurejea nchini timu hiyo ilicheza mechi ya kirafiki dhidi ya Power Dynamos za Zambia na kushinda mabao 2-0 katika kilele cha Simba Day.
Beki wa zamani wa timu hiyo, Boniface Pawasa ambaye ni kocha wa timu ya taifa ya Ufukweni anasema Simba ina wachezaji wazuri ingawa anaipa muda zaidi wa kupata muunganiko mzuri.
“Simba ina wachezaji wazuri sana. Nilichoona kwenye mechi ya Simba Day na za Ngao ya Jamii uwezo wa wachezaji ila bado hawajachanganya, naamini kufika Septemba kwenye michuano ya CAF watakuwa vizuri.”