Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hongera Yanga, Hersi kwa mafanikio ya kimkakati

Hersi Yanga Hongera Yanga, Hersi kwa mafanikio ya kimkakati

Mon, 2 Oct 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Pengine kufuzu kwa klabu ya Yanga kucheza hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa wa Afrika kunaweza kuwa kitu kidogo kwa baadhi ya watu, hasa wanaokebehiana mitandaoni baada ya Simba kufika hatua hiyo mara tatu katika miaka ya hivi karibuni.

Yanga, ambayo ilikuwa klabu ya kwanza kucheza hatua hiyo wakati muundo wa michuano ya Klabu Bingwa ya Afrika ulipobadilishwa na kuanza mwaka 1998, ilihitimisha safari yake ya kurudi hatua ya makundi Jumamosi iliposhinda kwa bao 1-0 kwenye Uwanja wa Azam Complex, hivyo kusonga mbele kwa jumla ya mabao 3-0 dhidi ya Al Merrikh ya Sudan baada ya kushinda mechi ya kwanza kwa mabao 2-0 jijini Kigali, Rwanda.

Tofauti na mwaka huu, Yanga ilifuzu kucheza hatua ya makundi mwaka 1998 wakati ikiwa na hali mbaya kiuchumi. Haikuweza kufanya usajili mzuri na wakati fulani ilibidi iazime wachezaji ili iweze kukabiliana na vigogo wa Afrika.

Hivyo, ushiriki wake katika hatua ya makundi ilikuwa ni majanga kwa kuwa ilikutana na klabu kubwa ambazo zilikuwa zimekaa vizuri kiuchumi, huku ligi zao zikiwa changamoto tosha ya kuziwezesha kujiandaa vizuri kwa mechi za Afrika, tofauti na ligi ya Tanzania ilivyokuwa wakati huo.

Katika mechi zote sita haikuonja ushindi hata ule wa Shamba la Bibi. Ilikaribia kuibuka na ushindi dhidi ya Raja Casablanca, lakini Waarabu wakasawazisha mwishoni na mchezo kuisha kwa mabao 3-3. Sare nyingine ilikuwa dhidi ya Manning Rangers kwenye Uwanja wa Uhuru (zamani Taifa).

Kutoka hapo, safari ya Yanga kwenye Ligi ya Mabingwa ikawa ni kuishia raundi za awali, hadi mwaka 2016 wakati mfumo mpya wa kuzipa nafasi kwenye Kombe la Shirikisho timu zinazotolewa raundi ya pili, ndipo Yanga tena ikawa ya kwanza Tanzania kuangukia hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho, ikafuatiwa na Namungo na baadaye Simba mwaka juzi.

Wakati Yanga inaanza mabadiliko, hali yake kiuchumi ilikuwa ishaanza kuwa nzuri. Lakini viongozi hawakutaka kuwapa mashabiki matumaini makubwa yasiyofikika haraka kisayansi.

Tangu miaka mitatu iliyopita, malengo ya Yanga yamekuwa ni kufika hatua ya makundi na chochote kikubwa kinachopatikana kinahesabiwa kama ziada. Ndivyo ilivyofanya kwa miaka mitatu mfululizo ambayo imeshuhudiwa Yanga ikibadilika kutoka kuwa timu ya kawaida Afrika hadi kuwa mshindani dhidi ya vigogo wa bara hili.

Mwaka wa kwanza wa safari ya Yanga ulishuhudiwa timu hiyo ikipata vipigo nyumbani na ugenini dhidi ya Rivers ya Nigeria na hivyo kutolewa mapema. Mwaka wa pili pia haukuwa mzuri kwa safari hiyo. Iling’olewa dhidi ya Al Hilal ya Sudan ilipotoka 1-1 Kwa Mkapa kisha kwenda kufungwa bao 1-0 ugenini.

Lakini safari hii, kulianza kuonekana mabadiliko yaliyokuwa yakiahidiwa tangu enzi za rais, Mshindo Msolla. Iliangukia Kombe la Shirikisho ambako ilitakiwa ipate ushindi dhidi ya Club Africain ya Tunisia kuweza kuingia hatua ya makundi. Kazi ilionekana kubwa kwa mashabiki, hasa wachambuzi, lakini haikuwa ngumu kwa vigogo hao wa Jangwani.

Sare nyumbani na ushindi wa bao 1-0 ugenini viliivusha Yanga hadi makundi, ambako ilipoteza mchezo mmoja na kutinga robo fainali na baadaye nusu na hadi fainali.

Ilikuwa ni mara ya kwanza kwa timu ya Tanzania kufika fainali ya mashindano hayo tangu CAF iliporekebisha muundo wa mashindano yake na kufuta mashindano ya Kombe la Washindi na Kombe la CAF na kubakiwa na michuano miwili ambayo ni Ligi ya Mabingwa wa Afrika na Kombe la Shirikisho.

Ni wazi kubwa haya yalikuwa ni mafanikio makubwa kwa Yanga na nchi. Ukweli kwamba mwishoni mwa msimu, Yanga haikupoteza wachezaji wengi, ulitosha kuimarisha imani kuwa viongozi wamepania kuimarisha timu na nafasi yake kwenye michuano mikubwa.

Pengine ni wachezaji wawili ambao walikuwa sehemu ya kikosi cha kwanza walioachana na timu. Fiston Kalala Mayele na Feisal Salum ndio pekee ambao Yanga inaweza kujuta kuwapoteza, lakini ilikuwa ni lazima waondoke kwa sababu tofauti; mmoja kutokana na ustadi wake na mwingine msimamo wa kutotaka kuendelea kubakia Jangwani.

Ndio, Yannick Bangala na Djuma Shabani walikuwa muhimu kwenye kikosi cha kwanza, lakini ukweli kwamba Yanga iliamua kuachana nao ni ushahidi kuwa ilishajiandaa kwa kutokuwapo kwao.

Ushuhuda wa jinsi ambavyo Yanga imekuwa ikipata mafanikio kwa hatua ni matokeo ya juzi yanayoirudisha timu hiyo kwenye Ligi ya Mabingwa ambako walipotea kwa miaka 25.

Hivi ndivyo timu zinatakiwa ziwe zinajipanga na si kuwa na matarajio makubwa ya kupumbaza watu, wakati hali halisi inaonyesha kinachosemwa hakiwezekani labda kwa miujiza au bahati.

Wakikabiliwa na kazi kubwa ya mabadiliko ya kimfumo, hasa muundo wa klabu na umiliki, viongozi walijua kuwa hayo yote hayawezekani bila ya kwanza kuwa na matokeo mazuri uwanjani. Matokeo mabaya, yangeshuhudiwa Hersi Said na wenzake wakipata misukosuko hadi mwak tajiri wao Ghalib Mohamed, ambaye ama angesusa ama angeamua kuachana na baadhi ya viongozi ili atulize wanachama.

Kwa kipindi cha miaka mitatu, unaweza kuhesabu mechi ambazo Yanga imepoteza katika Ligi Kuu na Afrika, tofauti na ambavyo imekuwa ikipata matokeo kimataifa. Kuanzia robo fainali hadi fainali, vigogo hao wa Kariakoo walipoteza mechi moja tu, walipofungwa mabao 2-1 na USM Alger jijini Dar es Salaam katika mechi ya kwanza ya fainali ya Kombe la Shirikisho.

Mechi nyingine dhidi ya Rivers na Marumo Gallants, Yanga ilipata ushindi, hadi ugenini na kutoka sare moja—waliposhindwa kufungana na Rivers jijini Dar es Salaam.

Ilipoteza mechi moja dhidi ya Monastir na kutoka sare moja dhidi ya Real Bamako. Ilishinda mechi nyingine zilizosalia dhidi ya TP Mazembe, Monastir na Real Bamako.

Kwa hiyo, mafanikio yamekuwa ni hatua kwa hatua na hata baada ya kuijenga timu na kuwa tishio, bado viongozi hawaahidi makubwa. Hadi kabla ya mechi ya Jumamosi, wamekuwa wakisema malengo yao ni kufika hatua ya makundi.

Na kwa jinsi ilivyoonekana katika mechi mbili dhidi ya Al Merrikh, mechi za hatua ya matoano za Kombe la Shirikisho na zile za Ligi Kuu, lolote laweza kutokea kwa Wana-Jangwani.

Wataalamu wanasema usipopongeza mafanikio madogo, hutaweza kuyaona hata makubwa. Pongezi kwa Yanga, na pongezi kwa rais wake, Hersi Said na wenzake.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: