Kwenye kambi ya timu ya taifa ya England huko Ujerumani, hofu inadaiwa kutanda kutokana na kuenea kwa ugonjwa wa kuhara na kutapika.
John Stones alilazimika kutengwa kutoka kwa wachezaji wenzake na wataalamu wa afya ili kuzuia ugonjwa huo kuenea baada ya beki huyo kuupata.
Beki huyo wa Manchester City ambaye kwa sasa amerejea ndiye mchezaji pekee aliyekosa mazoezi kwenye kambi yao ya Blankenhain Jumatano akipambana na ugonjwa huo.
Kocha wa kikosi hicho, Gareth Southgate alisema; “John alijisikia vibaya jana (Jumanne), kwa hivyo hatujamwona leo. Kuna siku chache hadi Jumapili tutaona kitakachotokea. Lakini niko hapa kucheza michezo na kushinda mechi na tunatumai tuchukua kombe. Hiyo ndiyo sababu niko hapa.”
Kwa mujibu wa taarifa, staa huyo alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa Norovirus uliomsababishia kuumwa na tumbo, kutapika na kuhara.
Timu ya madaktari imetoa tahadhari kwa wachezaji wengi wanataki kujichunga na mazingira kwani vimelea vinaweza kuwapata na wao pia kama ilivyokuwa kwa Stones ambaye kwa sasa ni mzima wa afya.
Kulikuwa na wasiwasi huenda asiwepo kwenye mchezo wa kwanza wa michuano hii dhidi ya Serbia lakini kwa mujibu wa ripoti ya madaktari, staa huyu anaweza kucheza bila shida na jana alionekana akiwa mazoezini tayari kwa ajili ya mchezo huo wa Jumapili.