Jumapili iliyopita, Yanga ilitwaa ubingwa wa Kombe la Shirikisho unaodhaminiwa na Benki ya CRDB kwa ushindi wa penalti 6-5 dhidi ya Azam FC ni baada ya suluhu katika dakika 120.
Mchezo huo uliopigwa usiku kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar na maelfu ya mashabiki ikiwamo waliovuka bahari kutoka Bara kushuhudia mchezo huo uliokuwa mgumu.
Dakika 90 za kawaida na 30 za ziada hazikuamua mshindi wa mchezo huo, hatimaye waliingia hatua ngumu ya penati iliyoshuhudia wachezaji saba wakikosa mikwaju ya penati.
Yanga ndiyo ilikuwa ya kwanza kwa wachezaji wake wawili kukosa penati mbili za awali mfululizo kati ya penati tano za kawaida na baadaye wakafuatia wawili wa Azam.
Katika medani ya soka, moja ya jukumu zito kwa wachezaji ni katika upigaji penalti katika mechi muhimu ikiwamo kama hii ya fainali ya kuwania ubingwa.
Hiyo si mara ya kwanza kwa wanasoka kukosa penalti, itakumbukwa hadi leo hii timu za taifa za Ghana, England na Italia haziwezi kusahau matukio ya wachezaji wao mastaa kukosa penalti.
Mchezaji anaweza kuwa fundi kweli kweli na kuleta mafaniko mengi katika klabu lakini siku ya penalti muhimu akakosa.
Itakumbukwa mwaka 1994 fainali ya Kombe la Dunia, Roberto Baggio wa Italia na Frank Lampard wa England katika robo fainali walikosa penalti muhimu kwa timu zao.
Upigaji wa penalti na kupata mchezaji anahitaji kujiamini na kutokuwa na wasiwasi. Huwa si rahisi kama watu wanavyodhani kwani mchezaji aliyepo uwanjani ambaye ametoka kutumia nguvu nyingi dakika 120 anapewa tena jukumu la kupiga penalti.
Jicho la kitabibu linaona kuwa sababu kubwa inayochangia kwa mastaa wakubwa katika timu kukosa penalti katika mechi kubwa muhimu ni kutokana na kuingia na tatizo la kisaikolojia.
Ukiacha mwili kuchoka kutokana na nguvu nyingi kutumika wakati wa kucheza, pia huwa wanapata msukumo wa mambo mengi kiasi cha kusababisha kuzalisha tatizo la kiakili la wasiwasi.
Tatizo la wasiwasi liko hivi
Tatizo ambalo linasababishwa wachezaji kukosa penati katika hatua kubwa kama ile huwa ni wasiwasi, ni tatizo hili linaainishwa kama tatizo la kiakili ambalo likizidi linasababisha kukosekana umakini.
Wasiwasi hujulikana kitabibu kama Anxiety, ni tatizo linalompata mtu yoyote katika mazingira ya kila siku, ni hali ya kuwa na hisia ya woga au hofu inayotokana na mtiririko wa mabadiliko ndani ya mwili.
Mwili unapokutana na mambo mbalimbali nje na kuyapokea kupitia mfumo wa fahamu hatimaye kupata tafsiri katika ubongo ambao nao hutoa amri kwa mwili kujihami.
Mwili unapochukua hatua ya kujihami husababisha kutiririshwa kwa vichochezi vinavyoambatana na hali mbalimbali ikiwamo woga au hofu au kuwa na ujasiri na nguvu.
Hapo tutaona wale wanaopata wasiwasi, hali hii inapomwingia tu mchezaji inamfanya kushindwa kujikita na kila anachokwenda kukifanya.
Hatua kama hizi, ndipo makipa wanapochukulia pointi tatu. Kwani walimu wao huwafundisha jinsi ya kuwasoma wachezaji wenye wasiwasi wakati wakupiga mikwaji ya penati.
Makipa hawa wanajitikisa na kurusha mikono huku na kule na kujitikisa lengo ni kumtoa katika kujikita katika ulengaji wakati wa kupiga.
Pia huwasemesha kwa maneno ya kejeli au kuudhi ili tu kumtoa katika lenge kuu la kulenga sehemu sahihi yenye nafasi kubwa ya kufunga.
Hii ndio mbinu ambazo wakipa wote wa klabu ya Yanga na Azam walizitumia kuwachochea.
Tumeona usiku huo wa jumapili staa anayewika kwa sasa Aziz Ki na mchezaji bora wa mashindano hayo Ibrahim Bacca wakikosa penalti muhimu.
Wataalam wa Saikolojia za wanasoka wanaoeleza kuwa mastaa wakubwa wenye hofu wanakuwa na nafasi kubwa ya kukosa penalti muhimu kutokana na wao kubeba zigo la matarajio.
Wakati wanapopewa jukumu hilo huwa wanawaza mengi ikiwamo kulaumiwa au kushindwa kutimiza ndoto zake, aidha akiwa mdhaifu huzaa wasiwasi au imara kisaikolojia humpa ujasiri na nguvu.
Mazingira wanayopiga penati hizo huwa yana watu wanaomzunguka wachezaji na benchi la ufundi na huku maelfu ya kelele za mashabiki wanaoshangilia na huku wengine wapinzani nao wanazoemea.
Yote haya yanamweka mchezaji katika hali mgumu ya shinikizo kubwa la kiakili, ikiwa mchezaji atakuwa amekumbwa na tatizo la wasiwasi ndio linazidi kuongeza katika mazingira uwanjani.
Vile vile maneno ya kejeli na makele yote yanaweza kuongeza ukubwa wa tatizo la wasiwasi kwa wachezaji ambao wanajukumu la kupiga penati.
Jaribu kupata picha mara baada ya Yanga kukosa penati 2 mfululizo. Kelele za wapinzani ndani na nje ya uwanja zilikuwa nyingi wakijua kazi imekwisha kilichobaki ni kumalizwa.
Lakini maunjanja ya kipa wa Yanga, Diarra Djigui na penalti ya Pacome ni kama ilienda kuondoa tatizo la wasiwasi wapigaji waliobaki na kupata hamasa na ari mpya.
Jinsi ya kukabiliana wasiwasi wakati wa upigaji penati
Moja, mchezaji anatakiwa kupewa elimu ya saikolojia sio katika siku ya fainali bali katika sehemu ya mafunzo yake. Kwa hiyo atakapokutana na mashinikizo makubwa anajua jinsi ya kukabiliana.
Akijengwa mapema kiakili anapata uzoefu na mbinu zinazomsaidia kukabiliana na hali shinikizo na wasiwasi.
Mbili, kitu kinachochangia kuwapa wasiwasi ni pale anaposhtukizwa kwenda kupiga penalti. Inatakiwa kuwa utaratibu wa klabu kuwapanga kabisa hawa ndio wapiga penalti kutokana kiwango.
Tatu, Wachezaji wanatakiwa kufanya mazoezi ya kweli yaliyo pangwa na wataalam wa eneo hilo. Vile vile kuwa na juhudi binafsi za upigaji penati na kufanikiwa kunasaidia kumjenga na kujiamini.
Ushauri
Wanasaikolojia na madaktari watumike kuwasaidia wachezaji na tatizo la wasiwasi kabla ya mechi muhimu ikiwamo za fainali. Umoja kati ya wachezaji na benchi la ufundi ni muhimu katika kujenga kujiamini.