Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hizi timu zinazohitaji kusajili baada ya mechi mbili za ligi

Jeremy Doku Man City 6259115.png Hizi timu zinazohitaji kusajili baada ya mechi mbili za ligi

Fri, 25 Aug 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wiki tu imebaki kabla ya dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi kufungwa. Kwenye Ligi Kuu England baada ya kushuhudia mechi mbili kwa kila timu, tayari imejionyesha wazi ni timu gani zinazohitaji kufanya maboresho makubwa kwenye vikosi vyao kabla ya kipindi cha usajili kupita.

Kutokana na hilo, hivi hapa timu 10 kwenye Ligi Kuu England, ambazo zinapaswa kufanya usajili walau wa mchezaji mmoja kabla ya dirisha hilo la uhamisho wa wachezaji kufungwa mapema mwezi ujao.

10) Man City – Winga

Manchester City imewapoteza Riyad Mahrez na Ilkay Gundogan kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi, huku msataa wake Kevin De Bruyne na Bernardo Silva wakiwa majeruhi wakati Ligi Kuu England ikiwa ndio kwanza inaanza. Nafasi ya Gundogan, kocha Pep Guardiola ameshasajili mbadala, Mateo Kovacic, lakini kwa winga Mahrez bado hajapatikana wa kuziba pengo lake, kitu ambacho miamba hiyo ya Etihad inaweza kufikiria kufanya usajili huo kabla ya dirisha hili kufungwa na ndio maana wanamsaka Jeremy Doku wa Rennes.

9) West Ham – Beki wa kati

Kulikuwa na ukimya sana kwenye kikosi cha West Ham United katika ishu ya usajili, lakini baada ya kumuuza Declan Rice wamepata pesa ya kusajili na kuwanasa Edson Alvarez na James Ward-Prowse. Kukwama kwa dili lao la kumchukua Harry Maguire kunawafanya kuendelea kuwa na uhitaji wa beki wa kati kwenye kikosi chao. Katika kukamilisha usajili na kukifanya kikosi chake kuwa tayari kwa vita kwenye Ligi Ku England msimu huu, kocha David Moyes anahitaji beki wa kati kabla ya dirisha halijafungwa mapema mwezi ujao.

8) Newcastle – Mchezaji mmoja

Kocha Eddie Howe ameweka wazi kwamba yeye si mtu anayeunga mkono matumizi ya pesa nyingi kwenye usajili wa mchezaji mmoja. Wakati kikosi chake kikiwa kwenye majukumu mazito msimu huu, ikitakiwa kucheza kwenye Ligi Kuu England huku ikiwa na michuano mingine ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Kutokana na hilo, Newcastle United inahitaji mchezaji mmoja zaidi kwenye kikosi chao, huku chaguo bora zaidi la mchezaji huyo akiwa beki wa kati watakuwa wametengeneza timu ambayo itakuwa tishio ndani nan je ya England.

7) Wolves – Mfungaji

Kama kuna kitu ambacho Wolves inahitaji kukifanyia kazi kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi kabla halijafungwa ni basi ni kusajili mchezaji wa kuwafungia mabao. Kwenye mchezo wao wa kwanza wa Ligi Kuu England, Wolves ilichapwa na Manchester United bao 1-0 na hakika ilipoteza nafasi nyingi za kusukumia mpira kwenye nyavu na ikashindwa kufanya hivyo. Mechi ya pili walichapwa na Wolves, lakini shida yao ilionekana kuwa ni ileile, kutokuwa na mchezaji mwenye shabaha na goli, mfungaji.

6) Tottenham – Straika/beki wa kati

Ripoti zinafichua kwamba Tottenham Hotspur wanapiga hesabu za kwenda kupiga hodi huko Chelsea kuulizia uwezekano wa kunasa saini ya mshambuliaji wao, Romelu Lukaku. Straika ni eneo ambalo, Spurs itahitaji kulifanyia kazi kwenye dirisha hili kabla ya kufungwa kutokana na kumpoteza Harry Kane na kubaki na Richarlison pekee. Lakini, Spurs pia kwenye eneo ambao wanahitaji kufanya usajili ni kwenye beki ya kati, hivyo kama kuna mchezaji mmoja inaweza kumwongeza kwenye kikosi, anaweza kuwa ni straika au beki wa kati.

5) Arsenal – Beki wa kati

Arsenal ilikuwa kwenye mikono salama hadi hapo beki wao mpya, Jurrien Timber alipoumia na kuwapo kwa uwezekano wa kuwa nje ya uwanja kwa msimu wote. Hilo litamfanya kocha Mikel Arteta atumie mmoja wa mabeki wake wa kati pembeni kwenye eneo alilokuwa akicheza Timber na kuacha pengo sehemu ya kati, ambapo kutahitajika mtu wa kuja kuliziba. Kitu kingine ni kuwapo kwa uwezekano wa kumpoteza beki wao wa Gabriel, anayewindwa na klabu za Saudi Arabia, hivyo Arsenal inahitaji beki wa kati kabla dirisha kufungwa.

4) Chelsea – Mfungaji

Chelsea imetumia pesa nyingi sana kwenye kujenga kikosi chake, huku wakiwekeza kwa nguvu kwenye sehemu ya kiungo. Lakini, Chelsea haina mpango wa kuendelea na huduma ya straika Romelu Lukaku, huku mkali wao mpya waliyemsajili, Christopher Nkunku ni majeruhi, jambo linalowafanya kutokana na uhakika wa kutosha wa mabao. Fowadi yao kwa sasa inaongozwa na Nicolas Jackson, lakini bado hajakoleza moto kwenye Ligi Kuu England. Kwa ubora wa Chelsea, wanahitaji straika wa maana kama Victor Osimhen atue kikosini kwao.

3) Everton – Straika

Dominic Calvert-Lewin majeruhi yake aliyopata hivi karibuni yamekuwa pigo kubwa kwenye kikosi cha Everton na sasa watalazimika kuingia sokoni kabla ya dirisha kufungwa ili kunasa straika mpya. Staa wao Alex Iwobi, naye amekuwa akisumbuliwa na majeruhi jambo linalowapa ulazima mabosi wa Goodison Park kuhitaji saini ya mshambuliaji mwingine kwa ajili ya kufanya mambo kwenye kikosi chao ili kiwe na ushindani wa kutosha kwenye Ligi Kuu England wasiwe kwenye hatari ya kupambana kutoshuka daraja.

2) Liverpool – Kiungo mkabaji

Dominik Szoboszlai ni mchezaji makini. Alexis Mac Allister naye ni mwanasoka mahiri sana, lakini Liverpool bado inahitaji kiungo wa kukaba kwenye kikosi chao kuwa na uwiano mzuri ndani ya uwanja. Kocha, Jurgen Klopp amefanya usajili wa kiungo Wataru Endo kutoka Stuttgart, lakini ukweli ni kwamba miamba hiyo ya Anfield inahitaji kiungo wa kukaba kuwaweka salama mabeki wao kutokana na Ligi Kuu England msimu huu kuwa na upinzani mkali, huku wao wakijaribu kusaka nafasi ya kurejea kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.

1) Man United – Kiungo mkabaji

Kwenye mechi mbili ilizocheza Manchester United kwenye Ligi Kuu England msimu huu, dhidi ya Wolves na Tottenham Hotspur shida kubwa sana ilionekana kwenye sehemu yao ya kiungo ya kukaba. Kocha Erik ten Hag ameamua kutambulisha mfumo mpya wa 4-1-4-1, msimu huu, Casemiro akipewa kazi ya kuwalinda mabeki wa kati, kitu ambacho kinaonekana kuifanya Man United kwenye majanga makubwa ya ukuta wake kufikika na wapinzani muda wote. Viungo wa upinzani wamekuwa wakimtambuka tu Casemiro na kuonekana amechoka.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live