Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hizi ni pacha hatari za WPL

Sdft Hizi ni pacha hatari za WPL

Wed, 28 Feb 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Achana na ule utatu wa MAP yaani Maxi Nzengeli, Aziz KI na Pacome wa Yanga ambao umekuwa tishio na kufanya vizuri ligi kuu bara.

Huku kwenye ligi kuu ya wanawake kuna pacha zinafanya poa na zimekuwa tishio kwenye ligi hiyo ambayo imeanza kukua siku hadi siku.

Yapo maeneo tofauti ambayo yamekuwa yakifanya vizuri na hasa wakicheza wachezaji wawili na zaidi na ambao wamekuwa wakileta uhatari kwa wapinzani.

Mwanaspoti linakuchambulia baadhi ya pacha hatari zinazofanya vizuri kwa timu nne za JKT, Simba, Yanga na Fountain.

1. STUMAI, JAMILA NA WINIFRIDA (JKT QUEENS)

Wachezaji hawa watatu wamekuwa muhimu kwenye eneo la ushambuliaji la JKT wakiibeba kwa mabao yao na wamekuwa hatari kwa wapinzani.

Kwenye mabao 33 iliyofunga JKT, 20 imefunga wachezaji hao watatu, 10 akiweka nyavuni Stumai Abdallah, saba yakifungwa na Winifrida Gerald na matatu yakifungwa na Jamila Rajabu.

Mbali na utatu huo kuwa bora lakini kuna viungo ambao wanaowasaidia kufunga kutokana na pasi zao, Donisia Minja akifunga mabao manne na kutoa assisti 10 kwenye mechi tisa na Amina Ally ambaye amefunga mabao manne.

2. MNUNKA, DJAFAR NA SHIKANGWA (SIMBA QUEENS)

Moja kati ya pacha hatari kwenye ligi msimu huu kutokea mitaa ya msimbazi, Simba.

Hakuna timu isiyoifahamu safu hiyo kutokana na ubora wao ambao unaongozwa na kinara wa mabao mpaka sasa Asha Mnunka (11), Asha Djafar (6) na Jentrix Shikangwa (4).

Mbali na kufunga mabao sita lakini Djafar ametoa assisti sita huku Shikangwa akifunga mabao manne na assisti tatu.

Watatu hao wamefunga hat-trick tatu mbili zikifungwa na Mnunka dhidi ya Amani Queens na Ceasiaa Queens huku Shikangwa akifunga dhidi ya Alliance Girls.

3. PRECIOUS, KAEDA NA SAIKI (YANGA PRINCESS)

Licha ya Yanga Princess kupoteza mechi tatu kwenye mzunguko wa kwanza lakini pacha hizi mbili zimekuwa bora.

Precious Christopher, Kaeda Wilson na Saiki Atinuke wamekuwa wakicheza kwa ushirikiano mkubwa na ndio sehemu muhimu katika kikosi hicho.

Wote watatu wamefunga mabao kwenye mzunguko wa kwanza Precoius akifunga mabao mawili huku Kaeda akifunga mabao matatu na Saiki akiweka kambani bao moja.

Msimu uliopita Saiki alikuwa akicheza na Irene Kisisa lakini msimu huu wawili hao wamekuwa bora zaidi baada ya Precious aliyekuwa straika kuchezeshwa nafasi ya kiungo chini ya Kocha Charles Haalubono.

4. CHRISTER, ANASTAZIA NA JOYCE (JKT QUEENS)

Pacha nyingine hatari ni hii ya mabeki wa kati wa JKT ambao wamekuwa mwiba kwa washambuliaji wanapokutana.

Christer Bahera, Anastazia Katunzi na Joyce Lema wamekuwa na kiwango bora wote watatu na kuwanyima nafasi washambuliaji wa timu za ligi kuu WPL.

Kwenye mechi tisa mabeki hao wameruhusu bao moja dhidi ya Yanga Princess timu hiyo ilipoondoka na ushindi wa mabao 3-1 lakini mbali na hivyo Joyce ambaye anacheza kiungo amefunga bao moja.

Mabeki hao wamekuwa wakifanya vizuri sio tu kwa JKT lakini hadi kwenye kikosi cha timu ya taifa ya wanawake ‘Twiga Stars’.

5. RITICIA, JOANITHA NA CORAZONE (SIMBA QUEENS)

Riticia Nabbosa, Joanitha Ainembabazi na Vivian Corazone ni pacha matata eneo la kuingo la Simba ambalo limekuwa likifanya vizuri.

Kwa Vivian ni msimu wake wa nne akiwa na Simba huku Nabbosa na Joanitha ukiwa msimu wao wa kwanza lakini wametengeneza pacha nzuri eneo la kati.

Mbali na ubora wa Simba msimu huu lakini hawa watatu wametengeneza pacha nzuri ambayo imekuwa tishio kwa wapinzani.

Ufundi wao upo hadi kwenye kufumania nyavu, Vivian akifunga mabao mabao matatu na Joanitha akifunga mabao mawili.

6. HASNATH, AMINA NA AQUILA (FOUNTAIN GATE PRINCESS)

Wamekuwa na kazi kubwa kwenye eneo la ushambuliaji na kiungo baada ya wachezaji muhimu wa Fountain kujiunga na timu za Simba, JKT na Yanga.

Wachezaji kama Winifrida Gerald na Joyce Lema(JKT ) walikuwa muhimu kwenye kikosi hicho ambacho kipo nafasi ya tano kwenye msimamo na pointi 12.

Hasnath Ubamba, Amina Ramadhan na Aquila Gaspar wamekuwa na kazi kubwa ya kuisaidia timu hiyo ambayo haijaanza vyema ligi kuu.

Amina amefunga mabao manne, Hasnath akifunga mabao mawili na Aquila hajafunga bao lolote akiwa na kazi kubwa kwenye eneo la ulinzi na mapacha hao wamekuwa bora na tishio kwa baadhi ya timu WPL.

7.AIRIN, OLUWA NA JANET (YANGA PRINCESS)

Airin Madalina na Janet Bundi wote wawili ndio msimu wao wa kwanza kucheza ligi ya Tanzania wakitokea nchini Kenya huku Oluwa Yemisi akitokea nchini Nigeria.

Muunganiko wa watatu hawa ambao wote ni wageni katika kikosi hicho wakijiunga na Yanga msimu huu wa dirisha dogo walisajiliwa baada ya mwanzo wa msimu kuonekana kuna shida ya straika.

Janet alifunga mabao matatu na Airin na Oluwa wote wawili wakifunga bao moja hadi sasa licha ya ugeni wao wamekuwa sumu kwenye eneo la ushambuliaji la Yanga.

Mara ya mwisho Airin kufunga ilikuwa dhidi ya Fountain Yanga ilipoondoka na ushindi wa bao 1-0 lakini wamekuwa wakileta uhatari.

Chanzo: Mwanaspoti