Baada ya kuteuliwa kuwa meneja wa Muda wa kikosi cha Chelsea hadi mwishoni mwa msimu huu 2022/23, Frank Lampard amebainisha kuwa hana wasiwasi na nafasi hiyo ambayo amepewa, kwani huenda ikatokea akawa meneja wa kudumu klabuni hapo.
Meneja huyo ambaye aliwahi kucheza katika kikosi cha Chelsea kati ya mwaka 2001–2014, katikati ya juma hili alitangazwa kuwa Mkuu wa Benchi la Ufundi la The Blues hadi mwishoni mwa msimu huu, akichukua nafasi ya Graham Potter ambaye alifungashiwa virago baada ya michezo ya Ligi Kuu mwishoni mwa juma lililopita baada ya kuwa na mwenendo mbaya ndani ya timu hiyo.
Lampard, mwenye umri wa miaka 44, ana jukumu la kuiongoza Chelsea kusaka matokeo mazuri kwenye michezo yake minane ya Ligi Kuu ya England sambamba na Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Mabingwa watetezi Real Madrid.
Akizungumza juu ya majaaliwa yake ndani ya Chelsea, Lampard amesema: “Sijali sana nini ambacho kitatokea. Sitaenda mahali popote kwani ninahitaji kufanya kitu kizuri ambacho kitaleta athari chanya hapa. Baada ya hapo tutaona nini kitajiri.”
“Sitaki kujibu juu ya hilo. Nimepewa nafasi hii nikiwa na masharti. Kilichopo mbele yangu ni kuifanya kazi hii.”
“Ni jambo zuri kwa maamuzi niliyoyafanya. Hii ni timu yangu. Nina hisia nyingi nzuri hapa.”
“Nilikuwepo Chelsea, nikaondoka na sasa waliponiuliza nichukue nafasi hii imekuwa jambo zuri kwangu.” Baadae hii leo Jumamosi (April 08) mishale ya saa kumi na moja jioni, Lampard atakuwa na kazi ya kuhakikisha Chelsea inashinda mchezo wake wa kwanza tangu alipokabidhiwa jukumu la kukiongoza kikosi cha Klabu hiyo, mbele ya Wolverhampton Wanderers.