Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hizi mechi zilipaswa kurudiwa, hazikurudiwa

Ref Vs Ballack Hizi mechi zilipaswa kurudiwa, hazikurudiwa

Sun, 8 Oct 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Mashabiki wa soka si wageni wa kushuhudia matukio tata na uamuzi wa hovyo wa waamuzi kwenye mechi mbalimbali. Sote tumeshuhudia makosa ya waamuzi yanayogharimu timu moja kufungwa bao, au uamuzi ambao unakuwa chanzo cha timu kushindwa kupata matokeo iliyostahili.

Kwenye Ligi Kuu England wikiendi iliyopita kulishuhudiwa tukio lililokuwa na athari kubwa kwenye mchezo wa ligi hiyo kati ya Tottenham Hotspur na Liverpool.

Mchezaji Luis Diaz alidhani ameifungia timu yake ya Liverpool bao la kuongoza baada ya kumalizia vyema kabisa pasi ya kupenyezwa, lakini kibendera kilinyooshwa kwamba ameotea. Picha za marudio za tukio hilo zilionyesha Diaz hakuwa ameotea, lakini VAR ilishindwa kuthibitisha hilo ili kulikubali bao hilo kuwa lilikuwa halali na PGMOL wakalazimika kuomba radhi.

Kutokana na hilo, kocha wa Liverpool, Jurgen Klopp alidai kwa makosa yaliyotokea, mechi hiyo inapaswa kurudiwa. Kurudiwa kwa mechi hiyo bado ni kitu kinacholeta mjadala mkubwa.

Mwanaspoti linakuletea mechi zilizokuwa na matukio ya utata yaliyosababishwa na waamuzi - ambazo kimsingi kama kurudiwa basi zilipaswa kuwa hivyo kwa sababu kuna timu zilipoteza haki.

England vs Ujerumani Magharibi - Kombe la Dunia 1966

Tuanze na kipute hiki cha kibabe. Mchezo wa fainali ya Kombe la Dunia 1966, wakati matokeo yakiwa 1-1 na mechi ikiingia kwenye dakika 30 za nyongeza, staa wa England, Alan Ball alipiga krosi kwa Geoff Hurst, ambaye alipiga mpira uliogonga mwamba wa juu na kudunda chini na mpira huo kuokolewa, lakini mwamuzi aliipa bao England akidai kwamba mpira ulivuka mstari. Wachezaji wa Ujerumani Magharibi walicharuka kwelikweli na ukaibuka mjadala mkubwa kama mpira ulivuka mstari au la.

Argentina vs England - Kombe la Dunia 1986

Mechi iliyokuwa na moja ya matukio ya utata zaidi kuwahi kutokea kwenye soka na hakika mechi hiyo iliwa na haki ya kurudiwa. Wengi wanafahamu hadithi ya “Mkono wa Mungu’, kwa wale wasiofahamu ni kwamba staa Diego Maradona aliifungia Argentina bao la mkono kwenye robo fainali ya Kombe la Dunia dhidi ya England. Kipa wa England, Peter Shilton aliruka juu kuupangua mpira ulioelekezwa golini kwake, lakini wakati huo tayari Maradona alisharuka na kuugonga mpira huo kwa mkono na kutinga nyavuni na mwamuzi akalikubali bao hilo.

Chelsea vs Liverpool - Ligi ya Mabingwa Ulaya 2005

Ukiwauliza mashabiki wa Chelsea kama kuna mechi ambayo wanaamini walinyima haki yao basi ni kwenye kipute hicho cha Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Liverpool, walifungwa Bao la Maruhani. Baada ya sare ya bila kufungana Stamford Bridge, mechi ya marudio ya hatua hiyo ya nusu fainali ilipigwa Anfield na ndipo kulikotokea tukio ambalo Chelsea waanaamini walionewa. Chelsea walifungwa bao ambalo mpira unaonekana haikuvuka mstari. Mashabiki wa Liverpool walishangilia na hapo refa akaamua kuita mpira kati, huku mastaa wa Chelsea waliokuwa wakinolewa na Jose Mourinho wakati huo wakibaki wenye hasira kutokana na kilichotokea.

Chelsea vs Barcelona - Ligi ya Mabingwa Ulaya 2009

Kama mashabiki wa Chelsea hawatakuwa wanaaminika kwa madai yao ya kuonewa kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya kwenye mechi ya Liverpool basi wanaweza kuleta ubaoni mechi hii ya Barcelona. Baada ya Michael Essien kuifungia Chelsea bao la kuongoza na wakiwa mbele kwa 1-0 kwenye mchezo huo wa nusu fainali, mwamuzi Tom Henning Ovrebo aliwakatalia penalti nyingi sana. Shuti la Andres Iniesta liliwasukuma nje ya michuano na kuwaacha mastaa Michael Ballack akizozana na kipa, huku straika Didier Drogba akidai ni upuuzi mkubwa. Ovrebo baadaye alikiri kuboronga mechi hiyo.

Jamhuri ya Ireland vs Ufaransa - Kufuzu Kombe la Dunia 2010

Ufaransa na Jamhuri ya Ireland zilikutana kwenye mechi ya kuwania nafasi ya kufuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia 2010 zilizofanyika Afrika Kusini. Ufaransa ilishinda mechi ya kwanza 1-0, lakini mechi ya pili, Ireland nao wakashinda 1-0, shukrani kwa bao la Robbie Keane. Mechi ikaingia kwenye dakika za nyongeza na hapo ndipo utata ulipokuja. Mpira wa adhabu ulielekezwa kwenye goli la Ireland, mpira ulikuwa unatoka nje na staa Thierry Henry akaugonga kwa mkono kuurudisha uwanjani na kisha akatoa pasi kwa mfungaji wa bao la ushindi William Gallas. Chama cha soka Ireland kiliitaka Fifa mechi ilirudiwe, lakini waligomewa.

England vs Ujerumani - Kombe la Dunia 2010

Wanasema ukiua kwa upanga, utakufa kwa upanga. England na Ujerumani zilikutana kwenye mechi ya Raundi ya 16 bora ya Kombe la Dunia na Ujerumani ilitangulia kufunga kwa bao la mapema kabisa. Mabao ya Miroslav Klose na Lukas Podolski wakafanya Ujerumani kuwa mbele kwa mabao mawili na kuwafanya England kupambana na kufanikiwa kufunga kwa kichwa kupitia beki Matthew Upson. Kisha ukaja wakati wa utata, ambapo England ilifunga bao la pili kwa shuti kali la kiungo Frank Lampard, ambapo mpira uligonga mwamba wa juu na kudunda ndani ya mstari. Hata hivyo, refa alikataa na kudai mpira haujavuka mstari na mechi ilimalizika kwa England kuchapwa 4-1. Baadaye, Fifa iliomba radhi kwa kosa hilo.

Hoffenheim vs Bayer Leverkusen - Bundesliga 2013

Leverkusen ilikuwa mbele kwa bao 1-0 na ilidhani imeongeza bao la pili baada ya Stefan Kiessling kufunga kwa kona. Picha za marudio zilionyesha kwamba mpira huo ulipenya kwenye nyavu za pembeni na kuingia ndani ya goli. Licha ya kugomewa sana na wachezaji pinzani, bao hilo lilikubalika na kuwakera Hoffenheim, ambao walichapwa 2-1 katika mchezo huo. Baada ya hapo kuliibuka matakwa ya kuanzishwa kwa VAR na Hoffenheim waliomba mechi irudiwe, wakakataliwa.

Liverpool vs Tottenham - Ligi ya Mabingwa Ulaya 2019

Mechi nyingine baina ya Liverpool na Tottenham Hotspur iliyokuwa na utata. Hii ilikuwa kwenye fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya iliyopigwa huko Madrid. Liverpool ilitangulia kufunga kwa bao la mkwaju wa penalti, lakini marudio ya picha zilishindwa kuonyesha wazi kama Moussa Sissoko alishika mpira uliosababisha iwe penalti. Kwa wakati ule, Liverpool walinufaika na uamuzi wa refa kwenye mechi yao dhidi ya Tottenham. Na sasa wakati kocha Klopp akilalamika kutaka mechi irudiwe, mashabiki wanamkumbusha kilichotokea kwenye fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya 2019, kilichotokea.

Aston Villa vs Sheffield United - Ligi Kuu England 2020

Hili ni moja ya matukio ya mmoja kunyimwa haki yaliyowahi kutokea kwenye Ligi Kuu England. Baada ya EPL kurejea kufuatia kusimama kwa siku 100 kutokana na matatizo ya janga la uviko 19, utata ukatokea kwenye mechi ya kwanza tu. Sheffield United wakiamini kwamba wamefunga bao la kuongoza wakati kipa wa Aston Villa, Orjan Nyland alipoanguka na mpira nyuma ya mstari wa goli na picha zilionyesha mpira umevuka mstari, lakini mwamuzi Michael Oliver hakuruhusu kuwa ni bao kwa kuwa saa yake haikutuma ujumbe kwamba mpira umevuka. ilikwisha na pointi moja waliyopata Aston Villa kwenye mechi hiyo iliwafanya wawe juu kwa pointi moja dhidi ya timu iliyokuwa ikishika nafasi ya 18 kwenye msimamo, Bournemouth.

Chanzo: Mwanaspoti