Oktoba to remember. Ni siku ambayo inaweka historia kwa nchi kutokana ufunguzi wa mashindano makubwa na mapya ya African Football League.
Simba ndio watakuwa wenyeji Ijumaa wakiwakaribisha Al Ahly kwenye mchezo wa ufunguzi unaotarajiwa kupigwa kwenye uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam.
Mashindano hayo ni kwa mara ya kwanza ya aina hiyo kufanyika hapa nchini hivyo yameambatana na fursa lukuki katika maeneo tofauti. Simba ambayo ni mwakilishi pekee kutoka Tanzania imetoa fursa kwa nchini kushuhudia mechi kubwa ya uzinduzi lakini pia timu za TP Mazembe pia itatumia uwanja wa Mkapa kama uwanja wao wa nyumbani wakiikalibisha Esperance ya Tunisia.
Wakati mashabiki wakifurahia ujio wa timu hizo kwaajili ya kuangalia burudani kutoka kwa timu hizo Serikali inanufaika na ujio wa timu hizo kwa manufaa ya fedha za kigeni ambazo zimekuwa changamoto hivi karibuni.
Mwanaspoti limechambua manufaa ambayo yatapatikana nje ya burudani ya soka. Michezo ni uchumi. Wachumi waliozungumza na gazeti hili kuhusu fursa za Tanzania kuwa sehemu ya mashindano hayo waliweka umuhimu wa maelfu ya dakika za kabla ya na baada ya dakika 90 za mchezo.
Tanzania itakuwa na ugeni wa timu tatu ambazo ni TP Mazembe, Al Ahly na Esperance ambao wote ujio wao utakuwa na tija kwa Taifa kuanzia kiuchumi, kibiashara na burudani kwa wadau wa soka.
Wakati timu tatu zikitarajia kuingia nchini katika raundi ya kwanza, Idara ya Uhamiaji itapata mapato yatokanayo na vibali vya kuingia nchini kwa Wachezaji na maofisa wa timu wasio raia wa Tanzania, Afrika Mashariki na baadhi ya Mataifa ya Jumuiya ya maendeleo ya Kusini mwa Afrika. Hivyo kwa ujio wa wageni hao na kulipia vibali vyao itaongeza mapato ya nchi yasio ya kikodi lakini zaidi fedha za kigeni hususani Dola ambazo hivi sasa zimeadimika.
Kwa asilimia kubwa timu zinaposafiri idadi ya makadirio benchi la ufundi, wachezaji na viongozi ni jumla ya watu 60 hivyo kwa timu mbili kuingia na idadi hiyo ni sawa na 120.
Msemaji wa Idara ya Uhamiaji, Paul Msele anasema wachezaji wasio wa raia wa Tanzania na nchi zisizohitaji visa kuingia nchini watalazimika kulipia vibali; “Kutoka Misri na Tunisia watatakiwa kulipa dola 50(Sh125,000) kwa kila mmoja kwa upande wa timu kutoka DR Congo raia wao hawana gharama hizo kwa sababu wapo Jumuiya ya Afrika Mashariki.”
WACHUMI
Ujio wa timu hizo ni furaha kwa wadau wa soka lakini kwa upande wa wachumi wao wanasema nje ya mchezo wa dakika 90 uwanjani Tanzania itanufaika na ongezeko la fedha za kigeni kwa kuwahudumia hoteli, vyakula. Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Katoliki Mbeya (CUCoM) Dk Balozi Marwa anasema ujio wa timu hizo mbali na faida ya kuburudisha wadau wa soka pia Tanzania itanufaika na ongezeko la fedha za kigeni ambazo zimekuwa changamoto hivi karibuni.
“Uwepo wa mashindano hayo hata kwa mechi chache hapa nchini utaongeza upatikaji wa fedha za kigeni kwani wageni wanalazimika kubadilisha fedha kwa ajili ya mahitaji ya huduma za kulala, kula na mambo mengine,” anasema
Vilevile mtaalamu huyo wa uchumi anasema kuna ajira za muda mfupi kwa vijana; “Hivyo ujio wa timu hizi Tanzania utasaidia kuongeza fedha za kigeni kwenye mabenki yetu kwa kufanya biashara ya vyakula, kulipa vibali vya kuingia nchini japo sifahamu ni wageni wangapi watakuja na mambo mengine.”
Mhadhiri mwingine Mwandamizi kutoka Shule Kuu ya Biashara, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Thobias Swai yeye anasema fursa ambayo nchi imepata inatakiwa kutumiwa kwa usahihi kwa kuhakikisha wanaiingizia mapato ya kutosha hususani Dola za Marekani.
“Dola hazijapotea kama ambavyo watu wanasema kwani wenye akaunti hizo fedha wanazo lakini kwa wale ambao hawana ni fursa kwao kuzipata kwani kutakuwa na ongezeko kubwa kwani wageni watakuja kulipa kwa kutumia fedha za kigeni.” anasema.
Mbali na kuongeza mzunguko wa fedha uchambuzi zaidi ulifanywa katika maeneo mengine ambayo tukio la michezo hiyo isiyopungua miwili na kuhesabu athari chanya za kiuchumi zitakazopatikana.
Mchambuzi wa uchumi maarufu Profesa Abel Kinyondo anasema Simba imefanikisha jambo kubwa ambalo nchi inatakiwa kulitumia vyema katika kujipatia kipato kupitia michuano hiyo.
Mhadhiri huyo wa UDSM anasema ni mara ya kwanza kufanyika na imeanzia Tanzania ni jambo kubwa na la kujivunia katika kila sekta hapa nchini kuona kuna fursa katika hilo. “Hapa sekta zote zinaingia ni wakati sasa wa wao kukaa na kuangalia namna gani ya kupata pesa kupitia mashindano hayo muhimu na makubwa,”
Anasema dakika 90 za uwanjani ni jambo lingine lakini nje ya dakika hizo ndipo kwenye umuhimu mkubwa ambayo kama nchi inatakiwa kujivunia sana.
Profesa Kinyondo anasema, utalii ni jambo kubwa sana ambalo anaamini wanaohusika wameshatupia jicho lao kuona fursa zilizopo katika jambo hilo kubwa.
“Mfano wanaweza kuwaeleza juu ya nini vinapatikana hata hapo Zanzibar mtu baada ya mchezo akashawishika kwenda na sehemu nyingine nyingi ambazo ni fursa kwetu kupata pesa, tunatakiwa kutengeneza mambo mbalimbali ambayo yatafanya pesa yao iweze kubakia hapa wasirudi nayo,” Mkuu wa Idara ya Mawasiliano kutoka bodi ya Utalii Robert Masunya anasema; “Tunaandaa mabango mbalimbali ambayo yatakuwepo uwanjani hapo na kuonyesha sehemu nyingi ambazo utalii unapatikana, wengi wamezoea kaskazini lakini sehemu za kitalii ni nyingi hata kusini zipo na zinavutia.
“Mabango yatawaonyesha wageni sehemu kama Mikumi, Ruaha, Katavi na kwingine kwingi naamini tutapata kitu kupitia haya mashindano ambayo Simba ndiye mwakilishi wetu kwa Tanzania,” anasema.
“Tushaanza maandalizi mazuri tu na makubwa naamini tutafanikisha kwa na kutumia furssa hii adimu hapa nchini kujitokeza.”
Aidha Profesa Kinyondo anasema hata Wizara ya mambo ya ndani inatakiwa kutumia fursa hii muhimu ambayo ni neema kuja Tanzania.
“Mfano mtu kaja kutazama mpira ametoka uwanjani na amani na utulivu wa hali ya juu huyuhuyu akirudi kwao atakuwa balozi mzuri ambaye hatohitaji gharama yoyote kuitangaza nchi,”
Profesa Kinyondo anasema Wizara inapaswa kujipanga kuvutia biashara za nje. “Mgeni akienda Kariakoo kumbuka alikuja kuangalia mpira tu na sasa anaenda kujipatia kitu kingine tena kwa bei nafuu naamini siku nyingine atarudi tena huyu.â€
Anatolea mfano timu kama TP Mzembe inayotokea DR Congo kwa kuwa inatoka karibu na Tanzania, watu wake wakipata uzoefu mzuri wa Kariakoo watakuwa wateja wa kudumu na mabalozi.
“Naamini kupitia haya mashindano nchini itajifunza mengi ili huko mbeleni kusiwe na shida ya aina yoyote ile,” anasema Profesa Kinyondo na kuongeza kuwa mashindano haya yanapaswa kuwa chachu ya maandalizi ya michuano mikubwa ijayo ya AFCON ambayo Tanzania ni mwenyeji.
MTAANI RAHA SANA
Mama Juma ambaye ni Mamantilie, anasema ikitokea mechi kubwa ambazo zinahusisha Simba na Yanga kuchezwa Benjamin Mkapa anauza chakula kwa wingi na anapata njia nyingi mbadala za mapato.
Anasema siku za kawaida anauza kilo tano hadi sita lakini kukiwepo na mechi hizo anauza hadi kilo 20. “Hata supu napika nyama kilo 10 siku ya tukio lakini siku za kawaida nauza kilo mbili wakati mwingine hata haiishi.”
Meneja wa baa ya moja iliyopo eneo hilo la uwanja wa Benjamin Mkapa amejipanga kuhakikisha vinywaji vya aina zote vinakuwepo siku hiyo na kama Simba ikishinda anaamini watu watakesha hivyo atapata pesa zaidi na kufanya mauzo makubwa ambayo kikawaida inaweza kumtumia wiki kadhaa kuyafanya.
Jacob Masawe ambaye ni dereva wa daladala kutoka Mbezi kwenda Mbagala anabainisha kuwa siku ya michezo mikubwa biashara yake inakwenda vizuri zaidi kuliko siku nyingine.
“Mechi kubwa tunakatisha ruti hatuendi Mbagala tunaokoa mafuta si unajua tena yamepanda bei, hivyo hiyo siku hiyo mimi nadamka mapema napiga mzigo na maisha yanasonga maana mechi kama hizi kujirudia ni mara chache,”
“Naweza kusevu hadi 120,000 nje ya makubaliano na bosi wakati siku za kawaida nikisevu Sh50,000 ni bahati kubwa kwa hiyo siku za mechi kubwa naamsha mapema mashabiki wanakuwa wengi sana siku hiyo kuanzia asubuhi hadi usiku,” anasema.
Marco Noel dereva wa bodaboda anasema yeye maskani yake ni kimara lakini siku za mechi kubwa anabadilisha gia na kwenda njia ya Buguruni hivyo mechi hizo kubwa kuja nchini ni neema adhimu.