Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hizi hapa mechi kali EPL 2024/25

Mechi Kali EPL Hizi hapa mechi kali EPL 2024/25

Thu, 20 Jun 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Baada ya kutangazwa kwa ratiba ya Ligi Kuu England 2024/25, Mwanaspoti linakuletea mechi za kibabe, zinazotarajiwa kuwa na mvuto mkubwa, ambapo kwa mashabiki wa mikikimikiki hawapaswi kuzikosa, watakuwa wamepitwa na uhondo mkubwa.

Mechi 380 zitapigwa kwenye Ligi Kuu England msimu wa 2024-25, ambao utaanza Ijumaa ya Agosti 16, kwa kipute cha Manchester United itakayokuwa nyumbani kukipiga na Fulham uwanjani Old Trafford.

Baada ya mechi ya kwanza kwenye ligi, baada ya hapo mashabiki watapata burudani ya mechi za kibabe kabisa, ambazo kimsingi mara zote zimekuwa na mvuto mkubwa na presha ya kutosha kuanzia kwa mashabiki hadi kwa wachezaji wenyewe. Hizi mechi usikose.

Jumapili, Agosti 18 - Chelsea v Man City

Kocha mpya wa Chelsea, Enzo Maresca kibarua chake cha kwanza kwenye Ligi Kuu England atakabiliana na mabingwa watetezi wa michuano hiyo Manchester City. Uzuri wa mchezo huo kwa Enzo ni kwamba utafanyika kwenye uwanja wa nyumbani wa Stamford Bridge. Msimu uliopita, miamba hiyo ilipokutana uwanjani hapo, matokeo yalikuwa 4-4. Enzo atakutana na bosi wake wa zamani, Pep Guardiola.

Jumamosi, Agosti 24 - Aston Villa v Arsenal

Kocha wa Aston Villa, Unai Emery alishinda mara mbili msimu wa 2023/24, dhidi ya waajiri wake wa zamani Arsenal na kuwatibulia kwenye mbio zao za ubingwa wa Ligi Kuu England. Bila shaka mashabiki watakuwa na hamu kubwa kuona mechi ya kwanza baina ya timu hizo mbili zitakapokutana Villa Park, kocha Mikel Arteta atafanya kitu gani ikiwamo kulipa kisasi dhidi ya mtangulizi wake huko Emirates.

Jumamosi, Agosti 31 - Man United v Liverpool

Miamba miwili kwenye Ligi Kuu England, Man United na Liverpool mechi yao ya kwanza itapigwa Old Trafford kwenye mwezi wa kwanza wa mwanzo wa msimu, huku kinachosubiriwa ni kuona kocha mpya wa Anfield, Arne Slot kama kuna kitu atafanya dhidi ya Mdachi mwenzake, Erik ten Hag, atakayekuwa kwenye kikosi cha Man United.

Jumamosi, Septemba 14 - Tottenham v Arsenal

North London derby ya kwanza ya msimu wa 2024-25 itapigwa nyumbani kwa Tottenham Hotspur, ambapo Mikel Arteta na chama lake la Arsenal atakwenda kukabiliana na mahasimu wake hao wakubwa kabisa kwenye soka la England. Mara zote, mechi hiyo ya Spurs na Arsenal imekuwa na upinzani mkali kuanzia kwa wachezaji hadi kwa mashabiki wao.

Jumamosi, Septemba 21 - Man City v Arsenal

Timu mbili bora kabisa kwa misimu miwili iliyopita. Arsenal na Man City zilikwenda jino kwa jino kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu England kwa msimu miwili iliyopita, huku msimu wa 2023-24, Arsenal ilizoa pointi nne kutoka kwa Man City. Kwa msimu huu wa 2024-25, mechi baina yao itaanzia huko Etihad, ambapo miamba hiyo miwili, Guardiola na msaidizi wake wa zamani, Arteta watakapoonyesha kazi.

Jumamosi, Okt 19 - Liverpool v Chelsea

Timu hizo mbili zitakuwa chini ya makocha wapya, ambapo kila mmoja atahitaji kuonyesha yupo vizuri kwenye kikosi chake. Slot atakuwa nyumbani Anfield kumkaribisha Maresca katika mchezo unaotazamwa kwamba utakuwa wa upinzani mkali kutokana na rekodi za miaka ya hivi karibuni timu hizo zinapokutana kwenye mikikimikiki ya Ligi Kuu England na michuano mingine.

Jumamosi, Novemba 30 - Liverpool v Man City

Kabla ya Arsenal kuingia kwenye vita ya ubingwa wa Ligi Kuu England misimu miwili iliyopita, shughuli pevu kwenye ligi ilikuwa Liverpool na Man City. Kocha Jurgen Klopp alikuwa akichuana jino kwa jino na Guardiola kwenye mbio za ubingwa. Lakini, sasa Liverpool itakuwa chini ya kocha mwingine, Slot na kinachosubiri kuona kama Liverpool itaendelea kuwa tishio kwa Man City kwenye kuonyesha ubabe uwanjani.

Jumanne, Desemba 3 - Arsenal v Man United

Ilipokwenda Emirates msimu uliopita, Man United ilikubali kichapo cha mabao 3-1 kutoka kwa Arsenal. Kwa kifupi msimu uliopita, Man United ya Erik ten Hag haikuwa na jambo mbele ya Arsenal, jambo lililofanya mashabiki wa miamba hiyo ya Old Trafford kuishi kinyonge mbele ya wapinzani wao hao wa Emirates. Na sasa Ten Hag amepewa nafasi ya kulipa kisasi, Desemba tu hapo atakapowafuata Arsenal kwao.

Jumamosi, Desemba 7 - Everton v Liverpool

Merseyside derby ni kipute kingine cha maana kwenye Ligi Kuu England. Huu utakuwa mchezo mwingine mgumu kwa kocha Slot atakapokabiliana na mahasimu hao wa jadi, ambapo mechi yao ya kwanza itafanyika kwenye Uwanja wa Goodison Park.

Jumamosi, Desemba 14 - Man City v Man United

United iliifunga Man City kwenye fainali ya Kombe la FA msimu uliopita. Patamu!

Chanzo: Mwanaspoti