Katika kandanda, kama katika mashindano mengine, kitu kinachoumiza sana wachezaji na wapenzi wa wachezaji au klabu zinazoshiriki ni mchezo kumalizika wakiwa wamekosa ushindi.
Lakini yapo mambo katika mchezo yanayosababisha masikitiko na kati ya hayo ni mchezaji kupewa kadi ya njano na zaidi akitolewa nje kwa kadi nyekundu na timu kulazimika kuwa na wachezaji 10 na wakati mwengine 9.
Hii husababisha wachezaji waliobakia kujituma zaidi ili kuziba hilo pengo.
Katika kandanda kitendo cha mchezaji kuonyeshwa kadi nyekundu huwa doa baya na huharibu rekodi ya mchezaji.
Katika historia ya fainali za Kombe la Dunia, Jose Batista wa Uruguay kwa zaidi ya miaka 40 sasa anashikilia rekodi ya kupata kadi nyekundu ya haraka zaidi.
Alionyeshwa kadi hiyo sekunde 56 tu baada ya kuanza pambano la timu yake ya Uruguay ilipocheza na Scotland nchini Mexico 1986.
Kutolewa kwake kulipelekea Uruguay kucheza zaidi kwa kujihami na mchezo kumalizika bila ya timu hizi kufungana.
Hata hivyo, Uruguay na Scotland zilitolewa katika mzunguko wa kwanza wa kundi lao. Uruguay ilimaliza ikishika nafasi ya tatu na Scotland ikakumbatia mkia.
Mshindi wa kwanza wa kundi hili la E alikuwa Denmark aliyokuwa na pointi 8 na kufuatiwa na Ujerumani Magharibi iliyopata pointi 3.
Kwa mshangao wa wengi, Ujerumani Magharibi ilifika fainali na kufungwa na Argentina 3-2 mbele ya watazamaji 114,600 kwenye Uwanja wa Aztec, Mexico City.
Katika Ligi Kuu ya England wapo wachezaji watatu wanaoshikilia rekodi ya aina yake ya kulimwa kadi nyekundu kutokana na mchezo mbaya bila ya kuugusa mpira hata mara moja.
Wachezaji hao ambao waliingia uwanjani kuchukua nafasi za wenzao waliotoka kwa kuumia au kubadilishwa na kocha ni pamoja na Andreas Johnstonn wakati timu yake ya Wigan ilipocheza dhidi ya Arsenal Mei 7, 2006.
Alipoingia uwanjani tu alianza kucheza rafu kwa kumvamia mchezaji na sio mpira. Kwanza alionywa kwa kidole, baadaye akapewa kadi ya njano na alivyorudia tena akatandikwa kadi nyekundu.
Kwa muda wa dakika 5 alizokuwapo uwanjani hajaugusa mpira hata mara moja, kama vile aliingia uwanjani kucheza mieleka na sio kandanda.
Wengine ni mchezaji wa Sheffield United, Keith Gillepsie katika pambano la timu hiyo dhidi ya Reading Januari 20, 2007 na Dave Kitson wakati timu yake ya Reading ikiivaa Manchester United Agosti 12, 2007.
Kwa zaidi ya miaka 10 sasa katika Ligi Kuu ya England hajatokea tena mchezaji kupewa kadi nyekundu bila ya hata kuugusa mpira moja.
Lakini hizi kadi za njano na nyekundu pia hutolewa na mwamuzi hata kwa wachezaji wa timu moja wanapofanyiana mambo yasiyokubalika katika ulimwengu wa soka.
Kwa mfano katika mwaka 2016 wachezaji wawili wa klabu ya Preston North, Jermaine Beckford na Eoine walipokuwa katika pambano na Shefield Wednesday walitolewa kwa kadi nyekundu na kuibakisha timu yao na wachezaji 9 uwanjani.
Hii ilitokana na kutoelewana na kutwangana masumbwi uwanjani. Mwamuzi alipowaonyesha kadi nyekundu aliwaambia wakaendelee na mchezo wa masumbwi nje uwanja na sio katika uwanja wa kandanda.
Vile vile katika mchezo wa mwaka 2005, dhidi ya Aston Villa, wachezaji wawili wa Newcastle United, Lee Bowyer na Kieren Dyer walitwangana makonde ile mbaya.
Muamuzi aliwatoa wote wawili nje na kilichofuata ni kufungiwa kucheza kandanda kwa miezi mitatu, mbali ya adhabu walizopewa na klabu yao.
Lakini wapo wachezaji waliopewa kadi nyekundu kwa kuvuka mpaka wa kusherehekea mafanikio yao.
Mmoja wao na ambaye video yake hutumika sana kuelezea wazimu wa kufurahia ushindi ni Medi Dresevic, mlinzi wa klabu moja ndogo ya Sweden.
Medi kutokana na kucheza kama mlinzi hakuwa na nafasi kubwa ya kufunga magoli kwa vile mara nyingi alibaki nyuma kulinda goli.
Lakini siku hiyo alifanikiwa kubandika mabao matatu mfululizo katika kipindi cha dakika 15. Kwa furaha kubwa alitoka mpaka nje ya kiwanja kufurahia na kuvua nguzo zote na kuwa kama alivyozaliwa.
Baada ya kuzivaa na kutaka kurudi uwanjani mwamuzi alimuonyesha kadi nyekundu na kumwambia bakia huko huko.
Wakati alipokuwa anavua nguo ilisikika sauti ya mtoto wake akipiga kelele: “Baba unafanya nini?”
Shabiki mmoja akamjibu kwani hujuwi kama baba yako ni mwendawazimu?
Baada ya mchezo wachezaji wenzake walimshambulia kwa matusi na klabu ikamfungia kwa miezi mitatu, lakini aliamua kutoendelea kucheza kandanda.
Siku hizi ni mara chache sana kwa Medi (pichani chini kulia) kufika katika viwanja kuangalia mchezo kwa sababu mara nyingi anapoonekana uwanjani huwa anazomewa, jambo amesema limekuwa linamuumiza sana.