Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hizi dili zimekula pesa ndefu sana dirisha la Januari

Skysports Virgil Van Dijk Liverpool 6236448 Hizi dili zimekula pesa ndefu sana dirisha la Januari

Thu, 28 Dec 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Dirisha la uhamisho wa wachezaji huko Ulaya limebakiza wiki moja tu kufunguliwa, ambapo makocha wa timu mbalimbali watakuwa bize kujaribu kusaka wachezaji wa kuja kuongeza kitu kwenye timu zao.

Mashabiki wa timu kadhaa ambazo zimekuwa na viwango vya hovyo kwenye nusu ya kwanza ya msimu wanatarajia makocha wao watafanya usajili wa nguvu kwenye dirisha hilo la Januari ili walau kuwa na uhakika wa kumaliza msimu vizuri mambo yasiwe mabaya zaidi.

Hata hivyo, dirisha la Januari mara nyingi limekuwa gumu kwa makocha kwa sababu kupata mchezaji mzuri itakulazimu kulipa pesa nyingi sana ili kuzishawishi timu kuachana na wachezaji wao muhimu katikati ya msimu.

Jambo hilo linafanya kuwapo kwa orodha ya wanasoka waliosajiliwa kwa pesa nyingi sana kwenye dirisha la Januari, ambao na kuingia kwenye rekodi za uhamisho huko Ulaya.

Makala haya yanahusu wachezaji waliosajiliwa kwa pesa nyingi kwenye dirisha la Januari, wakati timu mbalimbali zikisubiri kwa hamu usajili huo wa majira ya baridi huko Ulaya uanze kuona ni nani ataingia kwenye vikosi vyao na nani atatoka katika uhamisho huo wa katikati ya msimu.

Januari imeshuhudia usajili wa mastaa wengi waliofanya vizuri, lakini makala haya inawahusu waliozigharimu timu pesa nyingi bila ya kujali walikwenda kuvanya vizuri au la kwenda timu walizohamia.

Supastaa wa Kibrazili, Philippe Coutinho uhamisho wake wa kutoka Liverpool kwenda Barcelona, Januari 2018 bado unashikilia rekodi ya kuwa ghali zaidi kuwahi kutokea kwenye dirisha hilo. Lakini, wengine ni kina nani walionaswa kwa pochi nne dirisha la Januari?

10. Ferran Torres – Barcelona, Pauni 55milioni

Ferran Torres alikuwa mchezaji wa kawaida tu kwenye kikosi cha Manchester City, ambacho kilimsajili kwenye dirisha la majira ya kiangazi mwaka 2020, akitokea Valencia kwa ada ya Pauni 20.8 milioni. Kwenye kikosi cha Man City, mambo yalikuwa magumu kupata namba mbele ya wakali Riyad Mahrez na Phil Foden. Barcelona ikahitaji saini yake miezi 18 baadaye na kulipa Pauni 55 milioni kunasa huduma yake na kumvuta huyo Nou Camp kwenye dirisha la Januari 2022.

9. Bruno Fernandes – Man United, Pauni 55milioni

Bruno Fernandes amekuwa moja ya usajili bora kabisa wa Manchester United katika zama za Ligi Kuu England. Man United ilionyesha dhamira ya kumsajili kiungo huyo wa Ureno kwa muda mrefu hadi hapo walipofanikiwa kunasa saini yake Januari 2020, walipolipa Pauni 55 milioni kumsajili kutoka Sporting Lisbon. Man United iliyokuwa chini ya Ole Gunnar Solskjaer ilikuwa kwenye hali mbaya wakati Fernandes anatua na baada ya muda tu, mambo yakawa mazuri kwenye ligi.

8. Pierre-Emerick Aubameyang – Arsenal, Pauni 56milioni

Usajili wa mwisho wa kocha Arsene Wenger kwenye kikosi cha Arsenal na alifanya Januari, 2018. Staa wa Arsenal, Alexis Sanchez aliuzwa kwenda Man United wiki moja kabla – hivyo Wenger alihitaji mchezaji mwingine wa kuja kufunga mabao, ndipo alipokwenda kupiga hodi huko Borussia Dortmund kuliizia huduma ya straika Pierre-Emerick Aubameyang na kulipa Pauni 56 milioni kumpata. Auba alianza kwa kasi Arsenal na kushinda Kiatu cha Dhahabu cha Ligi Kuu England.

7. Aymeric Laporte – Man City, Pauni 57milioni

Januari 2018, Manchester City ikiwa kwenye nafasi nzuri ya kushinda ubingwa wake mwingine wa Ligi Kuu England, kocha wao Pep Guardiola bado alikuwa na mpango wa kuongeza mtu mwingine kwenye safu yake ya ulinzi na ndipo hapo alipokwenda kumsajili Aymeric Laporte kutoka Athletic Bilbao kwa ada ya Pauni 57 milioni. Ubora wa Laporte uliwaongezea nguvu Man City na kumaliza msimu wakiwa wamekusanya pointi 100 na kuweka rekodi Ligi Kuu England.

6. Christian Pulisic – Chelsea, Pauni 58milioni

Mwaka 2019, Chelsea ilikumbana na adhabu ya kufunguliwa kusajili, hivyo walifanya kila wanaloweza kumsajili Christian Pulisic kwenye dirisha la Januari. Mmarekani huyo aliwagharimu The Blues, Pauni 58 milioni kutoka Borussia Dortmund, lakini ilimwaacha hapohapo kwenye timu yake kwa mkopo hadi msimu ulipofika mwisho. Pulisic alikuwa na mwanzo mzuri katika msimu wake wa kwanza Stamford Bridge, akifunga mabao 11 na asisti 10 katika mechi 34 za michuano yote.

5. Oscar – Shanghai Port, Pauni 60milioni

Oscar alikuwa mmoja wa mastaa wenye vipaji matata kabisa waliowahi kukipiga kwenye Ligi Kuu England wakati Chelsea iliponasa saini yake akitokea Internacional mwaka 2012, kipindi hicho akiwa na umri wa miaka 20 tu. Alikuwa mtu muhimu Chelsea na alisaidia timu hiyo kushinda ubingwa wa Europa League na Ligi Kuu England mwaka 2015, kabla ya klabu ya China, Shanghai Port haijapiga hodi Stamford Bridge na Pauni 60 milioni zao kumsajili Januari 2017.

4. Mykhaylo Mudryk – Chelsea, Pauni 62milioni

Huu ulikuwa usajili wa kwanza wa bilionea Todd Boehly kwenye dirisha la Januari baada ya kuinunua Chelsea. Chelsea ilitoka kutumia Pauni 275 milioni kwenye dirisha la majira ya kiangazi 2022, lakini walihitaji kuongeza wengine kwenye dirisha la Januari 2023 na hapo wakafanikiwa kumnasa Mykhaylo Mudryk kwa pesa nyingi kutoka Shakhtar Donetsk, na walilipa Pauni 62 milioni kumvuta akakipige huko Stamford Bridge. Mudryk bado anajitafuta huko Chelsea.

3. Virgil van Dijk – Liverpool, Pauni 75milioni

Usajili wa beki wa kati Virgil van Dijk unatajwa kama hatua kubwa ya mapinduzi ya mafanikio ya kocha Jurgen Klopp kwenye kikosi cha Liverpool na hapo timu ikanza kushindania ubingwa wa Ligi Kuu England. Hata hivyo, Mdachi huyo hajatua Anfield kwa bei ndogo, kwani Liverpool ililipa Pauni 75 milioni, Januari 2018 huko Southampton ili kumnasa. Van Dijk amelipa kwa kile kilichotumika kupata saini yake, aliisaidia timu hiyo kushinda taji la Ulaya na England.

2. Enzo Fernandez – Chelsea, Pauni 105milioni

Januari 2023, Enzo Fernandez aliweka rekodi ya kuwa mchezaji ghali zaidi baada ya kunaswa na tajiri Todd Boehly akakipige huko Chelsea. Baada ya kuonyesha kiwango kizuri kwenye fainali za Kombe la Dunia 2022 akiwa na kikosi cha Argentina, Chelsea iliamua kwenda kunasa huduma dirisha la Januari baada ya kulipa Pauni 105 milioni kumsajili kutoka Benfica. Fernandez anapambana na hali yake huko Stamford Bridge akijaribu kuonyesha ubora kwenye sehemu ya kiungo.

1. Philippe Coutinho – Barcelona, Pauni 145milioni

Liverpool baada ya kufanya biashara safi kabisa ya kumuuza Philippe Coutinho kwenda Barcelona kwenye dirisha la Januari 2018 kwa mkwanja mrefu, walipata jeuri ya kwenda kumsajili beki Virgil van Dijk kwa pesa nyingi pia. Barcelona walitua Anfield kwenda kumsajili Coutinho, ambapo awali walilipa Pauni 105 milioni, huku dau hilo baadaye lilipanda na kuwa Pauni 142 milioni kutokana na kiwango chake. Barca walikuwa na pesa za mauzo ya Neymar huko PSG.

Chanzo: Mwanaspoti