Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hizi Simba, Yanga hazikuwa na maajabu

Simba, Yanga Warejea Ligi Kuu Jumamosi Hizi Simba, Yanga hazikuwa na maajabu

Sat, 17 Feb 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Beki mahiri wa zamani wa Coastal Union ya Tanga na Timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, Salim Amir Faki ameiomba Serikali ya Tanzania kuwaangalia kwa jicho la huruma wachezaji waliocheza michuano ya Mataifa ya Afrika (AFCON) 1980.

Salim ambaye ni beki wa kati aliyasema hayo hivi karibuni alipofanya mahojiano maalumu na mwandishi wa makala haya jijini Tanga.

“Wakati wetu tulicheza soka kwa kujitolea, tulikuwa na uzalendo wa hali ya juu wa kuipigania nchi yetu, hatukupata pesa kama wanayopata wachezaji wa sasa,” alianza kusema Salim na kuongeza;

“Wengi wetu kwa sasa hatujiwezi tena ukizingatia hakuna kikubwa tulichokivuna katika maisha ya soka, hivyo serikali ingetusaidia hata kwa kutupatia kadi za afya.”

AHADI ZA NYUMBA, GARI

Salim anasema wakati walipocheza mchezo wa mwisho dhidi ya Zambia ili kufuzu kwa fainali za Afcon zilizofanyika Nigeria mwaka 1980, Rais wa Zambia, Kenneth Kaunda ‘KK’ aliwaahidi wachezaji wa taifa lake nyumba na gari.

“Sisi hatukuwa tumeahidiwa kitu chochote, tulicheza kwa moyo mmoja kulipigania taifa letu na tukafuzu kwa michuano ya Afcon,” anakumbuka Salim.

“Ingekuwa vizuri kama serikali kupitia Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo ingetukumbuka hata kwa kadi za afya ili tuweze kujiuguza kwa maana tumeshakuwa wazee,” aliongeza Salim.

Hivi karibuni serikali kupitia Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ilifanya harambee kwa ajili ya kukusanya fedha kuzisaidia timu mbalimbali za taifa na baadhi ya wachezaji walioshiriki fainali za Afcon mwaka 1980 walishiriki katika kampeni hiyo.

Mbali na Salim wachezaji wengine walioshiriki harambee hiyo ni Augustine Peter ‘Peter Tino’, Juma Pondamali ‘Mensah’, Leopold Taso Mukebezi na Leodger Chilla Tenga.

Wengine ni Hussein Ngulungu, Mohammed Rishard ‘Adolf’ Omary Hussein na Rashid Idd ‘Chama’ na mbali na hao, wachezaji wengine ambao walishiriki fainali hizo na hawakuwepo kwenye harambee hiyo ni Idd Pazi ‘Father na Jellah Mtagwa ambao wanaumwa.

Wachezaji ambao hawakuwepo kwenye harambee ni Daud Salum ‘Bruce Lee’ na Mtemi Ramadhani na wengine watatu Thuwen Ali, Ahmed Amasha na Mohammed Salim walioko nje ya nchi.

Wachezaji wanne walioshiriki fainali hizo ambao sasa ni marehemu ni Juma Mkambi, Willy Kiango, Kajole na Athumani Mambosasa.

“Harambee kama ile pia ingeweza kutusaidia na sisi kutupunguzia mzigo angalau hata kadi za afya,” aliomba Salim ambaye kiasili alianza kucheza akiwa beki wa pembeni.

Salim ambaye kwa sasa hayuko kwenye uongozi wowote wa soka, alishangazwa na kitendo cha wachezaji wa zamani (ambao hawana nguvu) kutumika kuwachangia watu wenye nguvu.

STARS ILIVYOFUZU AFCON 1980

Katika mchezo wa raundi ya kwanza, Stars ilicheza dhidi ya Mauritius na kukubali kichapo cha mabao 3-2 ugenini.

Katika mchezo wa marudiano, jijini Dar es Salaam, Stars ilishinda kwa mabao 4-0 na kufuzu kwa jumla ya mabao 6-3.

Katika raundi ya pili Stars ndipo ilipokutana na Zambia na kushinda kwa jumla ya mabao 2-1. Nyumbani ilishinda 1-0 bao lililofungwa na Adolf na ugenini ikalazimisha sare 1-1 baada ya Tino kusawazisha bao la Alex Chola.

“Mechi ilikuwa ngumu sana, Wazambia walitumia nguvu sana waliamini wangeweza kutufunga mabao manne au matano katika mchezo ule wa ugenini ambao Rais Kaunda alikuwepo uwanjani,” anasema Salim.

“Kuna wakati walituzidi sana tulilazimika kumtoa Zito (Hassan) na kumwingiza Kajole (Mohamed) ili kuwadhibiti na kweli tulifanikiwa,” anasema.

Salim anakumbuka Zambia ya wakati ule ilikuwa kali sana na ilikuwa na wachezaji wazuri wakiwemo, Godfrey Chitalu, Pele Kaimana na Alex Chola ambapo Chitalu na Chola waliwahi kuhusishwa na timu za Leeds na Liverpool za England mtawalia.

“Nashukuru, nilipewa jukumu la kumdhibiti Chitalu nilifanikiwa hapa nyumbani na kule Ndola, Zambia,” anasema.

AFCON ILIVYOKUWA

Katika fainali hizo za Nigeria, Tanzania ilipangwa kundi moja na Nigeria, Misri na Ivory Coast. Katika mchezo dhidi ya Nigeria ilifungwa mabao 3-1 na ikafungwa na Misri 2-1 ikimaliza kwa sare dhidi ya Ivory Coast.

“Michezo miwili ya mwanzo sikucheza, katikati alicheza Jellah na Tenga (nahodha). Nakumbuka kwenye mchezo dhidi ya Nigeria, Meneja wetu, mzee Abdallah Mwinyi alinitetea sana nipangwe lakini ilishindikana.”

Katika mchezo dhidi ya Ivory Coast, Salim alianza kwa kucheza namba mbili na tatu akicheza Mohammed Kajole, katikati Jellah na Tenga.

“Baadaye Jellah alitoka akangia Tasso (Leopold) aliyekuja kucheza namba mbili, mimi nikarudi katikati kucheza na Tenga,” anakumbuka;

“Baada ya mchezo huo waandishi wa habari walinifuata na kunipiga picha huku wakiuliza huyo alikuwa wapi siku zote.

“Walisema nilistahili kucheza michezo yote iliyotangulia,” anasema Salim ambaye anakubali mara nyingi alikuwa akielewana sana alipocheza na Jellah.

“Nilipocheza na Jellah kwa asilimia 90, timu ilikuwa na uhakika wa kushinda,” anasema.

KUNDI LA KAWAIDA SANA

Pamoja na kutofanya vizuri kwenye Afcon hiyo ya mwaka 1980, Salim anasema wapinzani wao walikuwa ni timu za kawaida sana tofauti na timu hizo zinavyochulikuliwa hivi sasa, tatizo ilikuwa ni upangaji wa kikosi.

“Unajua kwanza sisi tulikuwa tumemzoea sana kocha Joel Bendera lakini baadaye tukaletewa Mzungu kutoka Poland, hapo ndipo shida ilipoanza.”

Kikosi hicho kilichokuwa chini ya Kocha Mpolandi, Slawomir Wolk akisaidiwa na Joel Bendera na Ray Gama.

MARA YA KWANZA STARS

Mwaka 1974, Salim alichaguliwa kukitumikia kikosi cha vijana cha Taifa Stars akiwa na Jellah Mtagwa.

“Pia, katika kikosi hicho alikuwapo Mambosasa lakini yeye alikuwa senior kwetu, alifanya utovu wa nidhamu akaondolewa,” anasema Salim na kuongeza kwamba mwaka huohuo akiwa na Shiwa Lyambiko walichaguliwa kikosi cha wakubwa cha Taifa Stars.

Wakati huo, kikosi hicho kilikuwa chini ya kocha marehemu, Marijani Shabani “Maji Mengi’ na kilifanikiwa kutwaa ubingwa wa Kombe la Chalenji ambapo kwenye michuano hiyo alicheza beki wa kati na Mohammed Bakari ‘Tall’.

“Katika mechi hizo, Jellah alicheza namba sita,” anasema Salim huku akiwataja wachezaji wengine kwenye kikosi ni Omar Mahadhi, Zaharan Makame, Mohamed Chuma, Salim, Tall, Jellah, Godfrey Nguluko, Sunday Manara, Ramadhani Mwinda, Gibson Sembuli na Lucas Mkondola.

Chini ya kocha Marijani kikosi hicho kiliifunga timu ya Taifa ya Uganda, The Cranes kwa penalti 5-3 baada ya mchezo kuisha kwa sare ya bao 1-1.

“Nikwambie kitu, katika kikosi hicho cha mwaka 1974 ni mimi na Jellah tu ndio tuliofanikiwa kwenda Lagos kucheza Afcon.”

UDHAIFU WA STARS

Mbali na mambo mengine, Salim alizungumzia kikosi cha Taifa Stars kilichoshiriki Afcon 2023 kule Ivory Coast.

“Kikosi kina udhaifu mkubwa, hakina wachezaji wa kulazimisha kupita kuwa-drive wapinzani kama ilivyokuwa kwa Mbwana (Abushiri), Sunday (Manara) na Ngulungu (Hussein).

“Wachezaji hawana determination (malengo), spirit (hawapambani) kuweza kuisaidia timu,” alisema Salim akiizungumzia Stars iliyokuwa Kundi F na timu za Morocco, Congo DR na Zambia.

KUVUNJIKA MGUU

Mwaka 1975, Salim alichaguliwa tena katika kikosi hicho kilichokwenda Msumbiji akiwa nahodha na mwaka 1975, Salim alivunjika mguu katika mchezo wa kuwania kufuzu Kombe la Dunia dhidi ya Misri baada ya kuteleza na kuanguka chini na mshambuliaji wa Misri akamkanyaga mguuni.

“Niliumia na niliporudi nchini nilitibiwa Muhimbili na Bombo Hospital,” anasema na kuongeza kwamba alifungwa POP lililomfanya akae nje kwa muda mrefu.

AFUTWA KAZI

Wakati alipoumia alikuwa akifanya kazi katika Kampuni ya Tanzania Motor Co-operation ambayo ilimfuta kazi baada ya kuumia.

“Viongozi wa kampuni ile walikuwa wakilalamika kila nilipokuwa nikienda kuitumikia timu ya taifa. Walikuwa wakiona kama vile nilikuwa nachukua mshahara wa bure. Nilipoumia ndio ikawa balaa zaidi, hawakuchukua muda wakanifuta kazi,” anasema Salim.

Pamoja na waandishi wa habari kupiga kelele kwamba mchezaji huyo alikuwa kwenye majukumu ya taifa lakini haikusaidia.

KINGUNGE AMPA MAISHA

Mwanasiasa Kingunge Ngombale Mwiru (sasa marehemu) ambaye aliwahi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Tanga alimfanyia mpango Salim akapata kazi bandarini.

“Kingunge aliniunganisha na mzee Kimario na nikafuata taratibu zote za kujiunga na kazi, nikaanza kama kibarua na hatimaye nikapata ajira ya moja kwa moja,” anakumbuka.

Baada ya kujiuguza kwa muda mwaka 1978, Salim alirudi uwanjani rasmi katika mchezo wa marudiano wa kufuzu Afcon dhidi Mauritius jijini Dar es Salaam.

APATA MAJANGA TENA

Salim alianza kucheza timu ya mtaani ya Niger Boys baadaye alijiunga na kikosi cha pili cha Coastal Union ya Tanga kilichoitwa Coastal Heroes.

Akiwa kidato cha tatu alijiunga na kikosi cha timu kubwa na kuitumikia kuanzia 1971 hadi 1980. Pia, aliichezea Taifa Stars kwa miaka saba kuanzia 1974 hadi 1980 alipostaafu soka baada ya kuumia goti.

Salim alipatwa na maumivu hayo wakati wa mechi ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara kati ya Coastal Union na Simba iliyochezwa 1980 mjini Dar es Salaam.

“Tulikuwa tumetoka kucheza na Yanga Mwanza na kuifunga mabao 2-0, katika mchezo wa Simba pale Dar es Salaam tulitakiwa kushinda ili kutwaa ubingwa.

“Lakini ilikuwa bahati mbaya kwangu niliumia ligaments na kulazimika kutoka uwanjani dakika ya 16 na mechi ile iliisha kwa sare, Simba ikawa bingwa,” anakumbuka.

Tangu alipoumia, amefanyiwa operesheni ya goti mara tatu ya kwanza mwaka 1985 Mombasa, Kenya kutokana na huduma hiyo kutokuwepo nchini wakati huo.

“Nilifanyiwa upasuaji katika Hospitali ya Pandia Memory ya Dokta Patel, hata hivyo, haikufanikiwa kwa kiasi kikubwa,” anasema.

Beki huyo alifanyiwa tena operesheni baada ya kubainika kuwa, goti lake halikuwa limekaa vizuri na mwaka 1990 alirudia tena kufanyiwa upasuaji Dodoma kwa Dokta Baki ambaye alimwambia kuwa alikuwa amechelewa sana.

“Aliniambia kwamba baada ya miaka 15 mguu huyo utanisumbua tena kwa kuwa upasuaji wa kwanza ulikuwa umefanyika nusu, daktari hakumalizia,” alisema Salim ambaye bado anatembea kwa kuchechemea.

MASTRAIKA WALIMUOGOPA

Beki huyo anasema hakuna mshambuliaji aliyekuwa akimuhofia na kudai wengi wao walikuwa wanajiuliza mara mbilimbili pindi wanapotakiwa kucheza dhidi yake.

“Wengi walikuwa wananihofia, nilikuwa makini sana nilipokuwa uwanjani,” anakumbuka Salim na kuongeza alikuwa akivutiwa sana na soka la Mbwana Abushiri ‘Director’.

“Huyu aliitwa Mkurugenzi wa Soka, alikuwa akicheza ‘clean football’ kwa uwezo wa hali ya juu sawa na kina John Lyimo, Shariff Salim, Sembwana, Mdanzi Mohammed, Twaha Ezekel na Rose Omary.”

UCHAWI KWENYE SOKA MH!

Salim anasema katika timu zote za Tanzania, mambo hayo hayakosekani. “Hata timu ya taifa, mambo ya wachezaji kuambiwa kunawa makombe ni kitu cha kawaida, lakini siri kubwa ya kuwa bora ni mazoezi na maandalizi mazuri,” aliongeza.

MECHI ANAYOIKUMBUKA

Beki huyo mkongwe anasema katika mechi za watani wa jadi wa Tanga, Coastal na African Sports, anaikumbuka moja ambayo waliifunga Sports mabao 2-0.

“Katika mechi ile tulikuwa na kocha Muitaliano aliyeitwa, Ben Cartacci ambaye alitufundisha mfumo uliotufanya tucheze uwanja mzima bila ya kuchoka.

“Mara mbili mwamuzi alisimamamisha mpira na kutuhesabu kwa kudhani labda tulikuwa wengi uwanjani,” anasema Salim ambaye alifunga bao la pili katika mchezo huo.

KOCHA ANAYEMKUMBUKA

Salim, mkazi wa Makorora jijini Tanga pia anamkumbuka kocha wa zamani wa Taifa Stars, Bernhard Carl ‘Bert’ Trautmann alikuwa anamkubali sana.

“Alikuwa akinikubali sana, alikuwa hakubali mtu mwingine acheze namba nne, alifurahi jinsi nilivyokuwa nikitimiza majukumu aliyonipa na wakati mwingine alitoa pesa yake mfukoni,” anasema Salim ambaye licha ya umri wa miaka 70 alionao sasa, bado ana nguvu na umbile lake halijabadilika. Ni lilelile alilokuwa nalo wakati alipokuwa akicheza soka. Ni mrefu wa wastani na bado mkakamavu.

Zaidi ya yote hayo, Salim ni mchangamfu na hupenda kuzungumza kwa sauti ya taratibu, lakini akiwa na hakika na kile anachokizungumza. Hutoa majibu ya swali analoulizwa bila ya kusita ama kujiuliza mara mbili.

Salim ni mmoja kati ya wanasoka wakongwe nchini, aliyejipatia sifa na umaarufu mkubwa kutokana na staili yake ya uchezaji.

Ni mmoja kati ya mabeki waliokuwa wagumu kupitika, hasa alipokuwa akiunda ukuta wa katikati wa Taifa Stars akiwa na Jellah Mtagwa.

MKOA WA TANGA

Salim aliitwa kwenye Timu ya Mkoa wa Tanga kwa zaidi ya miaka sita, ikiwa ni pamoja na kutwaa Kombe la Taifa 1973 dhidi ya Dar es Salaam baada ya ushindi wa mabao 2-1.

Wanasoka wengine aliokuwa nao kwenye kikosi hicho ni Omar Mahadhi, Salehe Zimbwe, Mbwana Mtoto, Rashid Moyo, Mwabuda Muhaji, Hemed Mussa, Mohamed Makunda na wengineo.

KWANINI SIO KOCHA?

Salim hakutaka kujihusisha na ukocha wa soka kutokana na kutokuwa fiti kiafya.

Alisema kutokana na kufanyiwa operesheni ya goti mara tatu, hawezi kumudu mikikimikiki ya kukimbia uwanjani ama kutoa mafunzo kwa vitendo, kama ambavyo kocha anatakiwa kufanya kwa wachezaji.

“Huwezi kuwa kocha bila kuonyesha mafunzo kwa vitendo. Maumivu niliyoyapata yamesababisha nisiweze kuimudu kazi hiyo ndio sababu sikupenda kujihusisha nayo,” anasema.

Akizungumzia maendeleo ya mchezo huo nchini hivi sasa, Salim alisema bado yanahitaji kufanyiwa kazi kutokana na wachezaji kutokuwa na ari na kuvumbua vipaji vya kucheza soka.

Alisema enzi zao, kiwango cha soka kilikuwa juu na wachezaji wengi walikuwa na vipaji vya aina yake vya kucheza soka na walicheza kwa ari kubwa na kujituma.

HAKUNA TENA SUNDAY MANARA

Salim alisema kwa sasa, vipaji vya wanasoka nchini vimepungua na sio rahisi kuwapata wachezaji wa aina ya Sunday Manara na Mbwana Abushiri, ambao amewaelezea kuwa, walikuwa na uwezo wa kuufanya mpira wanavyotaka.

“Huwezi kuwalinganisha Jellah Mtagwa na Sunday Manara na wachezaji wa sasa. Ipo tofauti kubwa,” alisema beki huyo wa zamani wa Taifa Stars.

“Wachezaji wa sasa wanalipwa fedha nyingi, lakini hawana ari. Wanashindwa kuelewa kuwa, mchezo wa soka kwa sasa ni kazi yenye manufaa sana. Wanacheza soka bila kuwa na malengo,” alisema mkongwe huyo.

“Makocha wamekuwa wakijitahidi kutoa mafunzo, lakini wachezaji wanafanya vitu tofauti uwanjani. Inawezekana ni kutokana na uelewa mdogo,” aliongeza.

SIO SIMBA WALA YANGA

Salim anasema wakati alipokuwa kwenye kiwango cha juu kisoka, hakuwahi kufikiria kujiunga na mojawapo kati ya klabu kongwe nchini za Simba na Yanga kwa vile hakuona tofauti ya maisha ya wachezaji wake.

Alisema baadhi ya wachezaji aliokuwa nao Coastal Union kama vile Elisha John na Yanga Bwanga, waliwahi kujiunga na Yanga, lakini kutokana na kutopata mafanikio, waliamua kuondoka na kwenda Uarabuni.

Licha ya kucheza soka kwa zaidi ya miaka 10, Salim anasema hakuna manufaa yoyote makubwa aliyoweza kuyapata kimaisha zaidi ya kujulikana na watu wengi na kutembelea nchi mbalimbali za Afrika na Ulaya.

“Enzi zetu hakukuwa na manufaa yoyote tuliyoyapata zaidi ya kutembelea nchi nyingi. Hali haikuwa kama ilivyo sasa kwa wachezaji wetu,” anasema.

Chanzo: Mwanaspoti