Licha ya kwamba Simba imekua na rekodi nzuri inapocheza na Mbeya City kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya lakini kiwango bora kilichooonyeshwa na ‘wana koma kumwanya’ hao kwenye michezo mitano ya karibuni kinaweza kuwa kikwazo leo kwa wekundu wa Msimbazi.
Mbeya City inaikaribisha Simba kwenye Uwanja wa Sokoine katika mchezo utakaoanza saa 10:00 jioni huku ikiwa na kumbukumbu nzuri ya kushinda mchezo wa msimu uliopita kwa bao 1-0 kwenye uwanja huo.
Timu hizo zinakutana zote zikiwa kwenye ubora wake kwani katika mechi tano za hivi karibuni za Ligi Kuu Bara, Mbeya City imeshinda mechi mbili na kutoka sare michezo mitatu wakati Simba michezo yake mitano ya karibuni imeshinda minne na kutoka sare mchezo mmoja.
Jambo la kushangaza ni kwamba timu hizo zote mbili mara ya mwisho kupoteza mchezo kwenye ligi zimepoteza dhidi ya Azam.
Mbeya City ilichapwa na Azam bao 1-0 katika mchezo uliofanyika Septemba 13 mwaka huu kwenye uwanja huo wakati Simba nayo ililala bao 1-0 dhidi ya matajiri hao wa Chamazi katika mchezo uliofanyika Oktoba 27 Uwanja wa Mkapa.
Hata hivyo, timu hizo zinakutana kwenye uwanja huo ikiwa ni mara ya tisa tangu Mbeya City ipande daraja mwaka 2013 na katika michezo hiyo, Simba imeshinda mara sita huku wenyeji wakishinda mara mbili tu ukiwemo ule mchezo wa msimu uliopita na mchezo mmoja zimetoka sare.
Pia katika michezo hiyo hakuna mchezo wowote baina ya hiyo uliomalizika kwa suluhu na timu yoyote kushindwa kufunga bao.
VITA YA MASTRAIKA
Wakati Mbeya City na Simba zinakutana katika mchezo huo, kwa upande mwingine itakuwa ni vita ya mastraika wanaofukuzana katika ufungaji wa wabao kwenye Ligi hiyo.
Sixstus Sabilo wa Mbeya City ndio anaongoza chati ya ufungaji hadi sasa akiwa ametupia mabao saba akifuatiwa na Moses Phiri wa Simba mwenye mabao sita sawa na Reliants Lusajo wa Namungo, Idris Mbombo wa Azam na Fiston Mayele wa Yanga ambaye jana alikuwa uwanjani kuikabili Dodoma Jiji.
Sabilo leo atapambana kutaka kuongeza idadi ya mabao ili aendelee kuwa kileleni huku Phiri nae pia akipambana kutaka kuongeza mabao ili awazidi wapinzani wake.
Hamu ya Phiri kutaka kufunga ilionekana hata katika mchezo uliopita Ruvu Shooting waliposhinda mabao 4-0 ambapo alionekana kupambana kutaka kufunga kila wakati lakini bahati haikuwa kwake siku hiyo kwani Bocco ndiye aliyeibuka staa wa mchezo kwa kufunga Hattrick huku lingine likifungwa na Shomari Kapombe.
Ukiondoa mastraika hao wawili lakini timu zote pia zina wachezaji wazuri wa nafasi hiyo mabao wanaweza kuamua matokeo muda wowote wakiwemo Augustine Okrah wa Simba mwenye mabao matatu sawa na Bocco na Pape Sakho wakati kwa upande wa Mbeya City kuna Tariq Seif mwenye mabao matatu sawa na kiungo Hassan Maulid Machezo huku pia ikitarajiwa leo mshambuliaji wao mkongwe Paul Nonga anaweza kurejea uwanjani.
KIUNGO PAMOTO
Mbeya City imeonekana kuwa bora sana msimu huu kutokana na uwepo wa viungo mahiri kama Nasor Maulid Machezo mwenye mabao matatu, George Sangija na Awadh Juma ambao wamekuwa mhimili mkubwa wa kuichezesha timu hiyo na kuweka muunganiko mzuri kwa washambuliaji wao hivyo Simba leo wanatakiwa kuwa makini sana.
Hata hivyo Simba nao hawako vibaya kwenye neo la kiungo kwani kurejea kwa Chama kumeonekana kuiimarisha timu hiyo ambaye ataisadiana na Muzamiru Yassin na Sadio Kanoute.
WASIKIE MAKOCHA
Kocha msaidizi wa Mbeya City, Anthony Mwamlima alisema utakuwa mchezo mgumu kwao hasa kwa kuangalia matokea waliyokuwa wakiyapata nyumbani msimu huu.
Tangu msimu huu uanze Mbeya City imeshinda michezo miwili pekee kati ya minane iliyocheza kwenye uwanja huo ilipoichapa Polisi Tanzania mabao 3-1 na Namungo mabao 2-1.
“Tunakutana na Simba ambayo imekuwa na mwendelezo mzuri kwenye michezo yake, hivyo tumejiandaa kukabiliana nao hasa kwa kurekebisha makosa yaliyokuwa yakijitokeza katika michezo iliyopita.” anasema Mwamlima.
Naye Nahodha wa City, Paul Nonga ambaye anakumbukwa kwa bao lake pekee kuipa timu yake ushindi msimu uliopita, alisema baada ya kuwa nje ya uwanja wa muda mrefu kwa sasa yupo fiti na tayari.
“Binafsi nimerejea baada ya majeraha ya muda mrefu, lakini ishu ya kuanza ni uamuzi wa kocha, kimsingi niwaombe mashabiki waje kwa wingi tunaahidi furaha kwani ni muda sasa hatujashinda,” alisema Straika huyo.
Naye kocha mkuu wa Simba, Juma Mgunda alisema wachezaji wana morali kubwa na yeyote anaweza akacheza kulingana na benchi la ufundi litakavyoona.
“Watu wengi wamekuwa wakiuliza uwezo wa Chama (Clatous) pamoja na Bocco (John), niseme hao wote ni wachezaji wa Simba na wanafanya majukumu yao kama ilivyo kwa wengine.
“Tunajua ubora wa Mbeya City na tumejipanga kucheza vyema ili tufanikiwe kupata pointi tatu katika mchezo huo,” amesema Mgunda.