Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Abdulkarim Amin 'Popat' amesema baada ya kukamilisha usajili, mashabiki watarajie mambo mazuri.
Akizungumza nasi jijini Dar es Salaam, Popat alisema usajili uliofanyika ni wa kimkakati zaidi na umezingatia ripoti ya benchi la ufundi.
"Ukiangalia kila nafasi tuliyosajili ilikuwa na pengo la mchezaji aliyeondoka msimu uliopita, hii inaonyesha ni kwa jinsi gani tumezingatia mapungufu yaliyopo kwenye timu yetu na kuweza kuyafanyia kazi kwa uharaka zaidi," alisema.
Popat aliongeza usajili wao umekamilika kwa asilimia 100 na licha ya muda bado kuwepo hadi Agosti 31 ila hawatosajili kwa presha ya timu nyingine.
"Muda bado upo na lolote linaweza kutokea lakini usajili huu hadi sasa kwetu tumekamilisha na kilichobaki ni maandalizi tu."
Wachezaji waliosajiliwa ni Feisal Salum 'Fei Toto' aliyetokea Yanga, Cheikh Sidibe (Teungueth), Alassane Diao (US Goree na Gibril Sillah kutoka Raja Casablanca.
Kikosi hicho kinachonolewa na Msenegali, Youssouph Dabo kitaondoka hivi karibuni kwenda Tunisia kwa ajili ya kambi ya maandalizi ya msimu.