Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hivi ndo Tuchel alivyofutwa kazi Bayern

Thomas Tuchel Ban Hivi ndo Tuchel alivyofutwa kazi Bayern

Tue, 27 Feb 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Thomas Tuchel ataondoka madarakani Bayern Munich mwisho wa msimu huu baada ya klabu kuamua kumfuta kazi. Na sasa jukumu lake ni kuhakikisha msimu huu hauwi wa kufeli jumla kwa klabu hiyo.

“Sitaanika chochote kati ya tuliyoyazungumza katika majadiliano ya uso kwa uso. Lakini mwisho wa yote, mimi ni mwajiriwa. Na waajiriwa hawana chaguo, hawana cha kufanya pale uamuzi unapotolewa. Lakini kila kitu kiko poa. Haijalishi ni namna gani nimepokea uamuzi uliotolewa juu yangu. Niko katika nafasi ya uongozi. Nawajibika kwa wafanyakazi wote. Huu ni mchezo wa kiwango cha juu, Tutapambania kila pointi. Mambo ya hisia yako kando,” Thomas Tuchel alisema alipoulizwa kama uamuzi wa kumfuta kazi ulikuwa ni makubaliano ya pande mbili.

Kuhusu uhusiano wake na wachezaji, kocha huyo mwenye umri wa miaka 50 ambaye aliwahi kufundisha Borussia Dortmund, Chelsea FC, na PSG, alisema atashangaa sana kama kutakuwa na watu ambao watafurahia kuondoka kwake. “Sitarajii kuona Aleksandar Pavlovie atafurahia kuondoka kwangu. Au Raphael Guerreiro, Minjae Kim au Manuel Neuer. Nitashangaa sana,” Tuchel alisema.

TATIZO SIO MIMI

Kocha huyo amesisitiza kwamba pamoja kuwa anaondoka klabuni hapo, tatizo sio yeye tu Bayern Munich huku akiongeza, kuujua mapema ukweli kuwa anaondoka kutamfanya asihofie kufanya baadhi ya uamuzi katika upangaji wa kikosi ambacho kitapambana zaidi.

Tuchel, anaondolewa madarakani kama sehemu ya kuisuka upya timu.

“Kilicho muhimu ni uwazi,” alisema Tuchel, aliyepewa mikoba ya timu hiyo Machi 2023.

“Uwazi unasaidia kuleta uhuru kwenye mechi na mazoezini.”

Akaongeza: “Uhuru kwa kocha (pia) unamsaidia kuamua. Unakuwa huhofii kitakachokukuta baadaye. Unaweza kuwa na timu inayopambana zaidi.

Lakini, wakifukuzia ubingwa wa 12 mfululizo wa Ligi Kuu Ujerumani msimu huu, wako nyuma kwa pointi nane dhidi ya vinara ambao hawajapoteza mchezo Bayer Leverkusen huku zikibaki mechi 12.

“Haijalishi kama nimeuelewa uamuzi wa klabu au kama nimeufurahia,” alisema Tuchel, ambaye timu yake ilishinda kwa bao la jiooni wakiilaza RB Leipzig 2-1, shukrani kwa mabao mawili ya Harry Kane.

Kane ameendelea kuongoza mbio za ufungaji bora katika ligi kubwa za Ulaya akiwa na mabao 27 akifuatiwa na Lautaro Martinez wa Inter Milan ya Italia aliyefunga mabao 22.

REKODI YA LEVERKUSEN

Bayer Leverkusen ya kocha Xabi Alonso imeweka rekodi mpya Ujerumani ya kucheza mechi 33 za kimashindano mfululizo bila ya kupoteza.

Leverkusen ilishinda 2-1 dhidi ya Mainz wikiendi iliyopita na kuivuka rekodi ya Bayern Munich ya kocha Hansi Flick iliyoweka rekodi hiyo kwa kuunga mechi za mwishoni mwa msimu wa 2020 na za mwanzoni mwa msimu wa 2021. Tofauti pekee, rekodi ya kikosi cha Alonso imewekwa ndani ya msimu mmoja.

Chama la Alonso linaendelea kuongoza kwa pointi 61 baada ya mechi 23, ikifuatiwa na Bayern yenye pointi 53, wakati VfB Stuttgart imebaki katika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 47, licha ya kushikiliwa kwa sare ya 1-1 na FC Cologne iliyo katika nafasi ya tatu kutoka mkiani ikiwa na pointi 17.

Borussia Dortmund yenye pointi 40, ilikuwa na bahati ya kutong’olewa katika nafasi ya mwisho ya Top 4 baada ya kulala 3-2 dhidi ya Hoffenheim inayoshika nafasi ya saba ikiwa na pointi 30, kwa sababu RB Leipzig yenye pointi 40, ilibakishwa katika nafasi yake ya tano kutokana na kuzamishwa na mabao ya Harry Kane ilipopigwa 2-1 na Bayern wikiendi iliyopita

Mainz imebaki katika hatari ya kushuka daraja katika nafasi ya pili kutoka mkiani ikiwa na pointi 15 baada ya kufungwa na kina Alonso waliowatumia kuweka rekodi mpya, huku nafasi ya mwisho ikibaki kwa SV Darmstadt yenye pointi 13.

Chanzo: Mwanaspoti