Weka kando suala la kuongoza kwenye Ligi Kuu Bara kwa Simba, rekodi zinaonyesha kuwa ukuta wao unateseka kwenye mechi za ugenini kutokana na kutunguliwa kila wanaposhuka uwanjani.
Katika mechi tano ambazo ni dakika 450 Simba inayonolewa na Kocha Mkuu, Roberto Oliveira ni mechi tatu ilicheza ugenini huku mbili ikicheza ikiwa nyumbani.
Ukuta wa Simba chini ya Che Malone umetunguliwa mabao manne kwenye mechi tatu za ugenini ikiwa na wastani wa kuokota bao moja langoni kila baada ya dakika 112.
Mchezo wa kwanza ilishuhudia ubao wa Uwanja wa Manungu ukisoma Mtibwa Sugar 2-4 Simba, kete ya pili ubao wa Uwanja wa Sokoine ulisoma Tanzania Prisons 1-3 Simba na kete ya tatu ubao wa Uwanja wa Liti ilikuwa Singida Fountain Gate 1-2 Simba.
Ni mabao 9 safu ya ushambuliaji ya Simba inayoongozwa na Jean Baleke ilitupia ikiwa na wastani wa kufunga bao moja kila baada ya dakika 90 ikiwa ugenini.
Oliveira amesema kuwa watafanyia kazi makosa kwenye eneo la ulinzi katika eneo la mazoezi.
“Makosa ambayo yanatokeo tunayachukua na kuyafanyia kazi kwenye eneo la mazoezi ili kuwa bora, wachezaji wanajituma na wanafanya kazi kwa umakini,”.