Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hivi ndivyo hali ilivyo kwenye kambi ya Yanga

Yanga Kikosi Mds Hivi ndivyo hali ilivyo kwenye kambi ya Yanga

Fri, 23 Feb 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Meneja wa Young Africans SC, Walter Harson, amezungumzia hali ya kikosi cha timu hiyo kuelekea mchezo wa Jumamosi dhidi ya CR Belouizdad ambao umepewa jina la Pacome Day kwa heshima ya kiungo wetu, Pacome Zouzoua.

Mchezo huo wa Kundi D katika Ligi ya Mabingwa Afrika, utachezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam kuanzia saa 1:00 usiku.

Kuelekea maandalizi ya mchezo huo, jana Alhamisi kikosi kilifanya mazoezi kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Akizungumzia maandalizi na hali ya kikosi, Harson alisema mpaka sasa hali ya kikosi ni nzuri, lakini tunatarajia kumkosa mchezaji mmoja pekee, Zawadi Mauya ambaye alipata maumivu ya nyonga.

“Maandalizi kuelekea mchezo wetu dhidi ya CR Belouizdad yanaendelea vizuri, kikosi kinafanya mazoezi kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, hatujacheza muda mrefu sana hapa, kuna wachezaji ni wageni pia hawajapata nafasi ya kucheza kwenye uwanja huu ambao utatumika siku ya mchezo ndio maana tumekuja kufanya mazoezi hapa.

“Kila kitu kinaenda sawa, tunamshukuru Mungu, sasa tunasubiri siku yenyewe, siku kubwa, Pacome Day iweze kufika.

“Mwenyezi Mungu akitujaalia kutokana na maandalizi tuliyoyafanya na ubora wa kikosi tulionao tunaamini tunaenda kuandika historia.

“Mipango inafanyika na mikubwa zaidi ni kuhakikisha Young Africans inakwenda kupata ushindi mkubwa katika mchezo huu kitu ambacho kitatufanya twende hatua nzuri ya robo fainali ya michuano hii ya vilabu barani Afrika.

“Ukizungumzia viongozi kuna sehemu yao wanaifanya kwa maana ya upande wa uongozi, upande wa benchi la ufundi chini ya Kocha Miguel Angel Gamondi na wao wanafanya majukumu yao, wachezaji nao wanatekeleza kile ambacho kinatolewa na benchi la ufundi.

“Kwa hiyo kila mmoja kwa upande wake anatekeleza majukumu yake ili siku ya Jumamosi kila mmoja aondoke na kile tulichodhamiria kukifanya kwa maana ya kutoka na matokeo kitu ambacho kitatuweka kwenye nafasi nzuri kuelekea hatua inayofuata.

“Hatuangalii zaidi ni aina gani ya ushindi tutapata, kikubwa kinachohitajika ni pointi tatu, hayo mengine ambayo yatakuja kutokea yatakuja baadae. Lengo letu namba moja ni kupata pointi tatu.

“Hadi wakati huu hatuna mchezaji yeyote ambaye ni majeruhi isipokuwa Zawadi Peter Mauya ambaye alipata shida ya nyonga katika mchezo uliopita wa Azam Sports Federation dhidi ya Polisi Tanzania.

“Ukimuondoa yeye kikosi kizima kipo mazoezini ikimaanisha tupo tayari, kila mtu anaitaka mechi, kwa hiyo kwa namna tulivyofanya maandalizi kocha atakuwa na siku ngumu ya kuchagua wachezaji 20 ambao watakwenda kutuwakilisha siku hiyo,” alisema Harson.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live