Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hivi ndivyo Simba SC ilivyopoteza alama 3 kwa Horoya

Manula Penalty Save.jpeg Mlinda mlango wa Simba, Aishi Manula akiokoa mkwaju wa Penati uliopigwa na Ndiaye

Sun, 12 Feb 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wawakilishi wa Tanzania katika Ligi ya Mabingwa Barani Afrika Klabu ya Simba imeanza vibaya michuano hiyo baada ya kupokea kichapo cha bao 1-0 dhidi ya Horoya ya Guinea kwenye mchezo wa kwanza wa hatua ya makundi uliochezwa Uwanja wa General Lansana Conte.

Bao la Horoya limefungwa na nyota wake, Pape Ndiaye dakika ya 18 ya mchezo baada ya kupiga kichwa kilichomshinda kipa Aishi Manula ambaye aliokoa penalti ya mfungaji huyo aliyopiga dakika ya 72 baada ya beki Joash Onyango kuunawa mpira eneo la hatari.

Kiungo wa Simba, Sadio Kanoute ataukosa mchezo dhidi ya Raja Casablanca utakaochezwa Februari 18 mwaka huu baada ya kuwa na kadi mbili za njano.

Mchezo huu ni wa kwanza kwa Simba kukutana na Horoya na pia timu kutoka Guinea kwenye mashindano ya klabu Barani Afrika.

Hata hivyo huu ni mchezo wa 23 kuikutanisha Simba dhidi ya klabu kutoka Afrika Magharibi katika mashindano tofauti ya Afrika ambapo kati ya hizo wawakilishi hao kutoka Tanzania wameshinda mara sita tu, sare sita na kupoteza mechi 11.

Katika michezo 11 iliyopita ya mashindano ya klabu ambayo Horoya imecheza nyumbani imeshinda sita, sare minne na kupoteza mmoja ambapo safu yake ya ushambuliaji imefunga jumla ya mabao 14 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara saba.

Kwa upande wa Simba katika michezo 11 ya ugenini imeshinda mitatu, sare mmoja na kupoteza saba ikifunga mabao tisa na kuruhusu 16.

Kwa matokeo haya yanaifanya Simba kushika nafasi ya tatu kwenye kundi C huku Horoya ikiwa ya pili na pointi tatu wakati kinara ni Raja Casablaca ya Morocco iliyoshinda jana mabao 5-0 dhidi ya Vipers kutoka Uganda ambayo inaburuza mkiani.

Baada ya mchezo huu Simba itashuka tena kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa kucheza na Raja Casablanca huku Horoya ikisafiri hadi jijini Kampala kukabiliana na Vipers ambapo michezo yote ya mzunguko wa pili itapigwa Jumamosi, Februari 18, 2023.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live