Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hivi ndivyo Robertinho alivyowamaliza Vipres Uganda

Robertinho X Mgunda Kampala Makocha wa Simba, Robrtinho na Juma Mgunda

Tue, 28 Feb 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Simba imerejea nchini juzi asubuhi kutoka Uganda ilipoenda kucheza na Vipers katika mechi ya Kundi C ya Ligi ya Mabingwa Afrika na kupata ushindi wa bao 1-0 na kufufua matumaini ya kuvuka kwenda makundi, huku Kocha mkuu wa timu hiyo, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ akifichua siri.

Kocha huyo Mbrazili aliyekuwa akiinoa Vipers kabla ya kutua Simba Januari mwaka huu, alisema ushindi walioupata ugenini ulichangiwa kwa kiasi kikubwa na mabadiliko machache aliyoyafanya kwenye kikosi na aina ya soka aliloingia nalo kwenye Uwanja wa St Mary’s-Kitende jijini Entebbe.

Katika mchezo huo, bao la Simba lilifungwa na beki Henock Inonga akimalizia pasi ya Moses Phiri aliyeupiga mpira kwa kichwa baada ya Clatous Chama kupiga friikiki na kuifanya timu hiyo itoke mkiani mwa kundi hadi nafasi ya tatu ikikusanya pointi tatu na bao moja, huku ikifungwa manne.

Vinara wa kundi ni Raja Casablanca yenye pointi tisa baada ya kushinda mechi tatu mfululizo ikiwamo ya juzi iliyoilaza 3-0 Horoya iliyopo nafasi ya pili na alama nne, huku Vipers ikiburuza mkia ikikusanya pointi moja tu na kila timu ikiwa imecheza mechi tatu hadi sasa.

Robetinho alimwanzisha kikosi cha kwanza Kibu Denis na Moses Phiri tofauti na ilivyozoeleka akiwapiga benchi nahodha John Bocco na Pape Ousmane Sakho, huku akitumia soka la kujilinda zaidi kuliko kushambuli na kocha huyo alisema hayo yamechangia kwa kiasi kikubwa kuwabeba.

Hata mabadiliko ya wachezaji kipindi cha pili alimtoa Phiri, Kibu na Chama na kuwaingiza, Erasto Nyoni, Kennedy Juma na Habib Kyombo na kocha alifafanua hiyo ilikuwa silaha na siri ya kupata ushindi muhimu ugenini ambao ulikuwa lengo lao.

“Nilifanya hivyo makusudi. Vipers nawajua vizuri wanacheza mchezo wa kasi na kushtukiza, hivyo nihitaji kuingia na watu wenye nguvu ya kushambulia na kukaba kwa nguvu na haraka kama Kibu,” alisema Robertinho ambaye ushindi huo ni wa kwanza kwake kwenye mechi za kimataifa akiwa na Simba, licha ya kuhusika kuivusha Vipers kuingia makundi ya msimu huu ikiwa ni rekodi kwao.

“Kama ulivyoona kuna muda walishindwa kujua mshambuliaji wa mwisho ni nani ili wamkabe, kwani Phiri, Kibu na Saido walikuwa wanabadilishana maeneo na hilo lilitusaidia kuwafanya mabeki wa Vipers kutopanda juu na muda mwingi kubaki kwenye eneo lao,” alisema Robertinho na kuongeza;

“Baada ya kupata bao tulihitaji kulilinda kwanza huku tukifanya mipango ya kutafuta mengine zaidi, na kadri muda ulivyozidi kwenda ilibidi tuongeze nguvu kwa kumwingiza Nyoni ili atulize presha na tukafanikiwa.”

SAKHO NA BALEKE Kocha huyo aliweka wazi sababu za kutowapa nafasi mastaa wengine wa kikosi hicho akiwamo, Sakho, Jean Baleke, Bocco na Peter Banda licha ya kuwa walikuwa katika benchi, kwani ana mipango nao kwenye mechi ya Jumanne ijayo watakaporudiana na Vipers, jijini Dar es Salaam.

Alisema aliowapa nafasi ndio walikuwa kwenye mpango wa mechi na waliosajilia akiwamo Baleke na Sakho watakuwa na kazi maalumu ya mechi hiyo ya nyumbani ambayo wanahitaji ushindi ili kujitegengenezea mazingira mazuri ya kwenda ropbo fainali kutoka ndani ya kundi hilo.

“Hawa nitaanza nao kwenye mechi ya Kombe la ASFC dhidi ya African Sports kisha watamalizia na Vipers na Mtibwa Sugar, kumbuka mechi hizi zote zipo karibu karibu sana, ni lazima tujiweka vyema kwani kote tuna malengo ya kufanya vizuri,” alifafanua Robertinho na kuongeza;

“Hatuwezi kuichezesha timu nzima katika mechi moja, kwanza tunahitaji kushukuru kumaliza mchezo salama hao ambao hawakupata nafasi sio kwamba ni wabaya, lakini tuna mechi nyingi na muhimu zaidi mbele yetu na ratiba ni ngumu, kwahiyo tulihitaji kuhifadhi nguvu ya ziada kwaajili ya mechi hizo. Kila mechi na mpango wake, huenda mkawaona kwenye mechi zijazo.”

Chanzo: www.tanzaniaweb.live