Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hivi ndivyo Dube alivyowaziba mdomo Azam FC

PRINCE DUBE MSH Prince Dube

Mon, 24 Jun 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Baada ya sintofahamu ya muda mrefu hatimaye Prince Dube amemalizana ‘kiungwana’ na Azam FC kufuatia ‘ushauri mzuri’ kutoka ‘mtu yule yule’ aliyehusika kushauri kwenye sakata la Feisal Salum 'Fei Toto'.

Dube amemalizana kwa kulipa fedh alizotakiwa kuilipa Azam ili aende anakopataka, vinginevyo mambo yangekuwa magumu kwake na hata kwa klabu iliyohusika kumshawishi kuzingua katikati ya msimu.

Mzimbabwe huyo aliyesaliwa na Azam mwaka 2020 akitokea Highlander ya Ligi Kuu ya Zimbabwe aliisusa ghafla timu hiyo ikiwa na mechi muhimu za kuwania ubingwa wa Ligi Kuu Bara kisha pande hizo mbili kufikishana Shiririkisho la Soka Tanzania (TFF) kesi ambayo hukumu yake ilikuwa haijatangazwa rasmi.

Hata hivyo, straika huyo wa kimataifa wa Zimbabwe amemalizana kiungwana na Azam na sasa yupo huru.

Awali ilionekana mambo yangekuwa magumu sana kutokana na mazingira aliyoondokea Dube na kauli alizotoa baada ya kuondoka.

Kama mshambuliaji pekee ambaye walikuwa naye kikosi cha Azam wakati ule kufuatia Idris Mbombo kuondoka na Alassane Diao kuumia, Dube aliwavurugia vibaya sana mipango yao ya kiufundi wa timu hiyo.

Hivyo hakuna ambacho kingewezekana baina ya pande mbili, Dube na Azam.

Mbaya zaidi Dube akaenda kufungua kesi TFF kukana mkataba ambao Azam wanadai alisaini mwaka 2023 ukitarajiwa kuisha 2026.

Haya yote yaliendelea ‘kuwatibua nywele’ Azam na kuapa kwamba wataifuata haki yao hata FIFA.

Lakini kama wasemavyo wahenga, muda ni tiba sahihi. Muda umefika na Azam wamekunjua roho na moyo kwa Dube.

Na aliyesimama katikati ya hili ni mtu yule yule ambaye alisimama katikati ya sakata la Feisal Salum na Yanga.

Mtu huyo aliyesimamia dili hizo zote ni mmoja wa vigogo waliowahi kuzitumikia klabu kubwa hapa nchini (jina tumelihifadhi).

UNAKUMBUKA ISHU YA AGAPE FUE

Mwaka 2013 wakati wa harakati za Uchaguzi Mkuu wa TFF, mgombea mmoja (Jamal Malinzi), aliwekewa pingamizi na mtu aliyejitambulisha kwa jina la Agape Fue.

Mtu huyu hakuwahi kufahamika hadi uchaguzi ukafanyika, Malinzi akashinda, akaingia madarakani, akahudumu kwa miaka minne, akatoka na sasa yupo Wallace Karia…bado huyo aliyemwekea pingamizi hilo hajafahamika hadi leo alikuwa nani zaidi ya hilo jina la Agape Fue.

Kwa kuwa jina hilo lina nguvu sana ya kujificha, nasi Mwanaspoti tunaamua kutumia uficho kwa jina la kigogo aliyesimamia na kufanikisha sakata zote mbili kubwa zaidi ya uhamisho hapa nchini ambaye aliwahi kufanya kazi katika mpira akiongoza klabu kubwa za hapa nchini na sasa ni ‘bosi’ wa kampuni moja kubwa inayofanya kazi kwa ukaribu sana na soka la Tanzania.

ILIANZIA NA FEISAL

Baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Samia Suluhu Hassan, kuwasihi Yanga kumalizana na Feisal Salum siku ile ya pilau la Ikulu, kigogo huyo akawafuata Azam kutaka kujua kama zile tetesi za mitandaoni kwamba wako nyuma ya Fei Toto ni za kweli.

Na kama ni za kweli basi yeye anaweza kwenda kuongea na Yanga na wakalimaliza.

Azam wakatoa ruhusa afanye kama anavyosema kama kweli anaweza. Kigogo huyo akawafuata Yanga na kuwaelezea mpango wake na utayari wa Azam FC kukaa mezani…Yanga wakakubali.

Akafuatwa Feisal Salum mwenyewe, akakubali…kazi ikaisha!

Yanga na Azam wakakaa mezani, wakakubaliana bei…Azam wakalipa, Feisal Salum akatangazwa haraka sana.

IKAJA KWA PRINCE DUBE

Hivyo baada ya mahangaiko yote ya Dube na Azam, kigogo huyo akaingilia kati kutengeneza amani.

Taarifa za mitandaoni na ushahidi wa kimazingira vilionesha fika kwamba Yanga iko nyuma ya sakata la Prince Dube.

Lakini kwa bahati mbaya Dube hakuwa na kifungu chochote cha sheria kitakachokuwa upande wake.

Kesi yake pale TFF ilisikilizwa na akaonekana hana hoja, japo hukumu haikuwahi kutolewa hadi sasa (ajabu).

Dirisha la usajili limefunguliwa na Yanga wanataka kumtambulisha Dube, lakini hawawezi hadi mambo yakae sawa.

Zikisubiriwa njia sahihi itamlazimu Dube kulipa Dola 300,000 ambazo ni zaidi ya shilingi milioni 700 za Tanzania.

Na Dube hana hizo pesa, wa kulipa ni hao hao Yanga…na wao hawawezi.

Itakumbukwa kwamba Yanga wamegharamika kiasi kikubwa sana kumpa mkataba mpya Aziz Ki, kwa hiyo wako hoi.

Njia rahisi ni kukaa na Azam mezani ili kuomba heri…sasa nani anayeweza hili?

Likaja jina la kigogo huyo, yaani yule aliyefanikisha mazungumzo ya Fei Toto.

Yanga wakamfuata na kuyajenga naye…naye akawatafuta viongozi wa Azam na kuongea nao…yakaisha.

Badala ya Dola 300,000 ambazo ni zaidi ya shilingi milioni 700, Yanga wakatoa Dola 200,000 mbili ambazo ni zaidi ya Shilingi 500 milioni.

Fedha hizi akapewa Dube mwenyewe akalipe ili aununue mkataba wake. Dube akaingiza hizo fedha na biashara ikaishia hapo.

BILA YA KIGOGO HUYO

Baada ya kesi ya Dube kuukana mkataba kusikilizwa pale TFF na tetesi kuzagaa kwamba kashindwa na anatakiwa alipe Shilingi 540 milioni, Azam waliapa kuikataa hukumu hiyo na kwenda mbele.

Walitaka kufungua kesi mbili dhidi ya Dube, na moja dhidi ya kamati iliyosikiliza kesi hiyo.

KWA DUBE

Kwanza ya madai ya fidia ya kuvunja mkataba kama mkataba unavyoagiza, yaani Dola 300,000.

Pili kuchafua jina la Azam kama kampuni kwa kudai imefoji mkataba. Kitendo chake cha kuukana mkataba maana yake Azam walifoji, na hiyo ndiyo ingekuwa kesi yao ya msingi.

KWA KAMATI

Tetesi zilisema kamati iliamua kesi ile kwa kuzingatia mkataba ambao Dube alisema anautambua, na kuucha ule ambao alisema hautambui.

Lakini kimsingi mikataba yote hiyo ilikuwa halali na Azam waliisajili TFF na kuwekwa kwenye mfumo tangu aliposaini mwaka 2023…kwanini kamati imepuuza mkataba huo halali?

Na ukweli ni kwamba tetesi za hukumu ya kesi zilikuwa sahihi na inasemekana TFF iliingia kati kusimamisha hukumu hiyo ambayo ingeichafua taasisi yao.

TFF iliogopa ingeonekana inababaisha katika hukumu zake kwa aina ile ya uamuzi…na ndio maana hukumu haikutoka.

Na hata kuvunjwa kwa kamati ile iliyosikiliza kesi, sakata la Dube ni moja ya sababu…japo sio pekee.

Hivyo endapo, kigogo huyo asingetokea hapa, yawezekana mambo yangekuwa magumu zaidi.

Maana ingewalazimu tu TFF kutoa hukumu ya kesi…na huku aidha ingekuja na malipo ya milioni 700 ambazo Dube na watu wake wangeshindwa kulipa, au milioni 540 ambazo Azam wangezikataa na kwenda mbele.

Lakini mwisho ya siku mpira umeshinda, kila upande umekunjua roho na moyo wakiacha boli litembee na sio ajabu pale Yanga ikianza kutaja majina ya nyota wapya wa kuimarisha kikosi cha msimu ujao jina la Dube likawepo katika orodha, kwani mambo yamemalizwa kiungwana bila kutarajiwa kwa sababu ya kigogo huyo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live