Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hivi ndivyo Arsenal itakavyobeba Ubingwa EPL

Mikel Arteta Arsenal 4 Hivi ndivyo Arsenal itakavyobeba Ubingwa EPL

Wed, 5 Apr 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Pointi nane kileleni kwenye msimamo wa Ligi Kuu England na bado mechi tisa tu mambo yaishe. Lakini, kuna swali moja matata, Arsenal wanahitaji kufanya nini kushinda taji lao la kwanza la Ligi Kuu England baada ya miaka 19?

Mikel Arteta ana kikosi chenye wachezaji wengi vijana na kitu kinachovutia ni kwamba amewaduwaza wengi kwa chama hilo la Emirates kuwa kwenye mbio za kubeba ubingwa wa Ligi Kuu England msimu huu - tena mbele ya vigogo kama Manchester City na Liverpool.

Kwa kuwa na safu ngumu ya mabeki, kiungo iliyojengwa kwenye uimara mkubwa na kuwa na huduma za wakali kama Bukayo Saka, Gabriel Martinelli na Martin Odegaard ambao wamekuwa bora zaidi katika theluthi hii ya mwisho ya kumaliza msimu, kuna mambo mengi ya kufanya Arsenal iendelee kupendwa kwa kandanda safi la ndani ya uwanja.

Lakini, ni jinsi gani na lini Arsenal itakamilisha mpango wake wa kubeba taji la Ligi Kuu England? Pointi ngapi wanahitaji kumaliza ubishi? Kitu gani kipo kwenye mechi yao kubwa dhidi ya Man City huko Etihad baadaye mwezi huu?

Kutokana na kubakiza mechi nane, kuna njia nyingi tofauti Arsenal inaweza kubeba taji hilo la Ligi Kuu England. Kwa njia nyepesi, Kama Arsenal itashinda mechi nane kati ya tisa ilizobaki watakuwa mabingwa wapya wa Ligi Kuu England msimu huu.

Pointi za maajabu ambazo Arsenal inasaka ni 95. Kama watafikisha pointi 95, Man City haitaweza kufikisha idadi hiyo ya pointi, hivyo ubingwa utakwenda Emirates.

Lakini, kama Man City wataichapa Arsenal katika mechi yao itakayopigwa Etihad, Aprili 26 na kisha wakashinda kiporo chao, Arsenal watahitaji kushinda mechi zao zote tisa zilizobaki ili kunyakua taji hilo la Ligi Kuu England. Jambo hilo litawafanya Arsenal kufikisha pointi 96 na Man City watakomea pointi 94.

Kama Arsenal itatoka sare na Man City na hapo chama hilo la Pep Guardiola litamaliza na pointi 92. Hiyo ina maana, Arteta na vijana wake wa Arsenal watahitaji kufikisha pointi 94 tu kuuchukua ubingwa wao.

Kama Arsenal itashinda dhidi ya Man City, hapo Man City watakuwa na uwezo wa kufikisha pointi 91 wakishinda mechi zao nyingine zilizobaki. Hivyo, Arsenal watahitaji kupata ushindi kwenye mechi sita tu kati ya saba zitakazokuwa zimebaki ili kunyakua ubingwa.

Mambo yote hayo yanaonyesha jinsi gani mechi ya Man City na Arsenal itakayopigwa Aprili 26 inavyoshikilia hatima ya bingwa wa Ligi Kuu England msimu huu.

Mara ya mwisho Arsenal kubeba taji la Ligi Kuu England ilikuwa msimu wa 2003-04, ilipokuwa na kikosi kilichofahamika kama ‘Invincibles’ baada ya kucheza kwa msimu mzima bila ya kupoteza mchezo wowote katika mechi 38 za ligi.

Taji lao la mwisho Arsenal kubeba ilikuwa Kombe la FA katika msimu wa 2019-20 na walinyakua pia Ngao ya Jamii mwaka 2020, wakiwa chini ya kocha Arteta.

MATAJI YOTE YA ARSENAL

Kombe la FA (14), Ligi Kuu England (3), Ligi Daraja la Kwanza (10), Kombe la Ligi (2),

Ngao ya Jamii (16), Kombe la Washindi Ulaya (1), Inter-Cities Fairs Cup (1).

LIGI INARUDI WIKI HII

Mchakamchaka wa Ligi Kuu England unarudi wiki hii, ambapo leo Jumanne na kesho Jumatano zitapigwa mechi za viporo ili kufanya mambo kwenda sawa katika mikikimikiki hiyo ya kibabe kabisa.

Usiku wa leo Jumanne kutakuwa na mechi nne matata kabisa, lakini macho ya wengi yatakuwa huko Stamford Bridge, wakati Chelsea itakapokuwa nyumbani kuwakaribisha Liverpool. Miamba hiyo miwili yote imetoka kuchapwa kwenye mechi zao zilizopita, kiasi cha kuwafanya Chelsea kumfuta kazi aliyekuwa kocha wao Graham Potter.

Msala mwingine utakuwa huko King Power, ambapo Leicester City iliyoachana na kocha wake Brendan Rodgers itakipiga na Aston Villa, iliyomfukuzisha kazi Potter huko Stamford Bridge, wakati Leeds United iliyotoka kupigwa 4-1 na Arsenal itakuwa nyumbani kucheza na Nottingham Forest huko Bournemouth wakiwa na kazi mbele ya Brighton. Mechi zote ni za moto kwelikweli.

Leo, Jumatano kutakuwa na mechi mbili tu, lakini zote zikiwa na madhara makubwa kwenye Top Four ya ligi hiyo, ambapo Manchester United itakuwa nyumbani Old Trafford kukipiga na Brentford, huku West Ham United ikiwa na kazi pevu mbele ya Newcastle United.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live