Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hispania kijasho kwa Ziyech, Ronaldo mikononi mwa Xhaka

Leo Pic.png Hispania kijasho kwa Ziyech, Ronaldo mikononi mwa Xhaka

Tue, 6 Dec 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Watatoboa? Ni swali tu, linalowahusu Morocco, Hispania, Ureno na Uswisi wakati leo Jumanne zitakapofahamu hatima zao kwenye mechi za mtoano za hatua ya 16 bora kwenye fainali za Kombe la Dunia 2022 huko Qatar.

Miamba hiyo minne ya soka duniani, yenyewe ndiyo inakamilisha hatua hiyo ya 16 bora kabla ya kuanza kwa robo fainali ya mchakamchaka huo huko Qatar kuanzia Ijumaa hii.

Kipute kitapigwa Morocco na Hispania kwenye Uwanja wa Education City na refarii ni Muargentina, Fernando Rapallini. Patamu hapo.

Ureno ya supastaa Cristiano Ronaldo yenyewe itafahamu hatima yake kwenye majaliwa ya kusonga mbele au kukwama kwenye hatua hiyo kwa kuwakabili Uswisi uwanjani Lusail, huku mwamuzi akitarajiwa kuwa Cesar Ramos kutoka Mexico.

Mechi ya kibabe kabisa. Morocco imetinga hatua ya mtoano ikitokea kwenye Kundi F, ambapo ilikuwa vinara baada ya kukusanya pointi saba baada ya kushinda mechi mbili na kutoka sare moja katika mechi zake za makundi, ikifunga mabao manne na kufungwa moja.

Wapinzani wao Hispania, wenyewe walimaliza nafasi ya pili kwenye Kundi E, walipokusanya pointi nne katika mechi tatu, ambapo walishinda moja, sare moja na kuchapwa moja. Kwenye hatua hiyo ya makundi, Hispania imefunga mabao tisa na kufungwa matatu.

Lakini, kipute chao cha leo kinahusu mtoano, hivyo panga pangua lazima mshindi apatikane. Zege halilali.

Morocco yenye huduma ya Hakim Ziyech na Hispania zimewahi kukutana mara moja kabla ya mchezo huo wa leo na uzuri ilikuwa kwenye fainali za Kombe la Dunia 2018 huko Russia, mchezo wa Kundi B uliomalizika kwa sare ya mabao 2-2.

Kwa maana hiyo, miamba hiyo hakuna mbabe baina yao kwenye mechi hizo za Kombe la Dunia na rekodi halisi itaandikwa kwenye Uwanja wa Education City, saa 12:00 jioni kwa saa za Afrika Mashariki. Nani atatoboa?

Baada ya mechi hiyo, usiku wa saa 4:00 kwa saa za Afrika Mashariki itakuwa zamu ya Ronaldo na chama lake lenye wakali wengi akiwamo Bruno Fernandes kufahamu hatima yao kwa fainali hizo za Qatar kwa kuikabili Uswisi yenye huduma moto kama ya wakali kama Granit Xhaka, Xherdan Shaqiri na Breel Embolo. Mechi ya mastaa na hakika patachimbika.

Uswisi imeibukia kwenye hatua ya mtoano ya 16 bora ikitokea kwenye Kundi G, ambapo ilimaliza nafasi ya pili wakiwa na pointi sita kama ilivyokuwa kwa vinara Brazil, lakini tofauti yao ilikuwa kwenye idadi ya mabao ya kufunga na kufungwa. Uswisi ilifunga mabao manne na kufungwa matatu katika mechi hizo tatu ilizocheza hatua ya makundi, ambapo ilishinda mbili na kupoteza moja, sawa na Brazil - lakini wao walifunga mabao matatu na kufungwa moja.

Ureno yenyewe ilimaliza vinara kwenye Kundi H baada ya kukusanya pointi sita katika mechi tatu, ikishinda mbili na kuchapwa moja, huku ikishinda mabao sita na kufungwa manne. Mambo ni moto.

Ureno ya Uswisi zimewahi kukutana mara sita huko nyuma na katika mechi hizo, kila moja imeshinda mechi tatu. Hakuna mbabe.

Mara ya mwisho timu hizo zimekutana kwenye Uefa Nations League kwenye mechi ya League A: Group 2 - iliyopigwa Juni ambapo mechi ya kwanza Juni 5, Ureno ilishinda mabao 4-0 ikiwa nyumbani kabla ya marudiano Juni 12, ambapo Uswisi ilishinda bao 1-0.

Uzuri wa mechi hizo ilizokutanisha Ureno na Uswisi zote zilikuwa za mashindano, hivyo kilikuwa kipimo halisi cha kufahamu upinzani wao wa uwanjani. Lakini, safari hii inakutana kwenye fainali za Kombe la Dunia na mbaya zaidi ni hatua ya mtoano, ukipigwa umesukumwa nje. Itakuwaje?

Mshindi kwenye mechi hiyo atakabiliana na mshindi wa mechi ya Morocco na Hispania kwenye hatua ya nane bora. Kazi kwelikweli.

Chanzo: Mwanaspoti