Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hispania, Uingereza ni fainali ya rekodi, visasi

Final Euroooo Hispania, Uingereza ni fainali ya rekodi, visasi

Fri, 12 Jul 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Ni Hispania dhidi ya England. Fainali ya michuano ya Euro 2024 imeshajulikana timu gani zitakutana baada ya juzi Jumatano England kuifuata Hispania kwenye mchezo huo utakaopigwa Jumapili, Julai 14. Ni kwenye Uwanja wa Olympiastadion, jijini Berlin.

Vijana wa Mfalme Charles wa tatu wa Uingereza dhidi ya wenzao wa Mfalme Felipe VI wa Hispania katika mchezo huo ambao unatarajiwa kuwa mkali.

Hispania ndiyo ilikuwa ya kwanza kufuzu fainali baada ya kuichapa Ufaransa mabao 2-1, huku England ikiichapa Uholanzi mabao 2-1.

Usichokijua. England itakutana na Hispania (Spain) kwenye mchezo huo ikiwa ni timu ya kwanza katika historia ya michuano hiyo na Kombe la Dunia kukutana na wapinzani watano tofauti na majina ya nchi zao yanaanzia na herufi (S).

Kwenye Kundi C ilikokuwepo, ilicheza dhidi ya Serbia na Slovenia, kisha kucheza na Slovakia kwenye 16 bora na kukutana na Uswisi (Switzerland) hatua ya robo fainali na sasa inaenda kucheza fainali na Hispania (Spain).

Pia fainali hii ni ya pili mfululizo kwa England ikiungana na timu nyingine nne zilizofanya hivyo ambazo ni Soviet Union (Kabla ya kumeguka na kuundwa mataifa mengine), Ujerumani ya Mashariki na Hispania.

Chini ya Kocha Gareth Southgate wababe hawa wameweka rekodi ya kufika fainali mbili katika mashindano manne ya Kombe la Dunia na Euro kijumla.

Pia ni taifa la kwanza kufika fainali ya Euro licha ya kuanza kwa kufungwa katika mechi za robo na nusu fainali.

Hispania ambao ni mabingwa wa kihistoria wa Euro ikiwa sawa na Ujerumani zikibeba taji hili mara tatu, itakuwa inaingia katika mchezo huu ikiwa ina rekodi ya kushinda mechi nane mfululizo za mwisho ikiwa ni rekodi yao bora tangu mwaka 2010 iliposhinda mechi 12 mfululizo chini ya Kocha Vicente del Bosque.

Pia ndiyo timu ya kwanza katika historia ya Euro kushinda mechi sita zote katika kalenda ya shindano moja.

Vile vile hii inakuwa ni fainali ya tano kwa Hispania katika michuano hii ikiwa ndiyo timu iliyofika hatua hiyo mara nyingi zaidi katika historia ya Euro.

Kijumla timu hizi zimekutana mara 27 katika michuano mbalimbali, mara ya kwanza ni mwaka 1929 katika mchezo wa kirafiki na England ilichapwa mabao 4-3.

England ndio inaonekana kuwa na rekodi nzuri mbele ya Hispania katika mechi hizo kwani imeshinda 14 sare tatu na kufungwa 10.

Kijumla Hispania haijawahi kuifunga England hata mara moja katika michuano ya Euro na katika mechi nne imepoteza zote, lakini ina rekodi nzuri mbele ya England katika michuano ya Kombe la Dunia na katika mechi mbili ilizokutana imeshinda moja na kutoa sare moja.

Hata hivyo, katika mechi 10 za mwisho ilizokutanisha mataifa haya, England imefanya vibaya kwa kufungwa tano, ikashinda nne na mmoja ukamalizika kwa sare.

Mara ya mwisho mataifa haya kukutana katika Euro ni mwaka 1996 katika robo fainali na England ilipenya kwa changamoto ya mikwaju ya penalti 4-2, mwaka huo England ndio ilikuwa mwenyeji wa michuano hiyo.

Mechi ya mwisho kukutanisha timu hizi ni Oktoba 15, 2018, katika michuano ya Uefa Nations League na England ikashinda mabao 3-2.

Mchezo huu ambao utapigwa saa 4:00 usiku, unatarajiwa kushuhudiwa na zaidi ya mashabiki 74,475 watakaoujaza uwanja huo.

Chanzo: Mwanaspoti