Ponapona ya Nahodha wa Simba, John Bocco kusalia ndani ya kikosi hicho, impe funzo la kutafsiri nini kitafuata kwake msimu huu ambao utabeba mambo mawili kwake kupanda kwa kiwango zaidi au kushuka.
Nafasi anayocheza Bocco ina ushindani mkali wa namba ingawa takwimu zinambeba zaidi. Ukiachana na aliokuwa nao msimu uliopita kuna ongezeko la Willy Onana limekuja kuongeza chachu zaidi ya anayecheza kikosi cha kwanza kutakiwa kuwa na kitu cha zaida mbele ya kocha Roberto Oliveira ‘Robertinho’.
Ukitaja washambuliaji wazawa wenye thamani kubwa kulingana na walichofanya, basi huwezi kuacha jina lake. Bocco amekuwa na mwendelezo wa kiwango bora na kwa kizazi hiki ndiye anayeongoza kwa kufunga mabao mengi - 151 na yamesalia matatu tu kumfikia staa wa zamani wa Yanga, Mohamed Hussein ‘Mmachinga’ aliyetupia mara 153.
Ni takribani miaka miwili hivi Bocco alipitia majeraha ya hapa na ndani ya kikosi hicho yaliyomfanya muda mwingi asitumike katika kikosi cha kwanza. Hata hivyo kila alipopata nafasi ya kucheza alijitahidi kufunga mabao mengi.
Data zinaonyesha msimu wa 2021/2022 alimaliza akiwa na mabao matatu na 2022/2023 alimaliza nayo 10, hivyo inaonyesha kwamba bado kama mzawa amekuwa kwenye rekodi bora ya ufungaji wa mabao.
Tangu msimu uliopita zilikuwepo tetesi za Simba kutaka kuachana na Bocco na kipindi hicho ilitajwa Ihefu FC kuhitaji huduma yake na matajiri wa timu hiyo kuahidi kumpa mashamba ya mpunga kufanya uwekezaji nje ya dau la usajili na mshahara ambao angepata.
Kwenye usajili wa msimu huu kati ya majina yaliyokuwa yanatajwa kuondolewa Msimbazi lilikuwemo lake. Wakati mabosi Simba wanataka kufanya hivyo zilitajwa Singida Fountain Gate, Namungo FC na Ihefu kwa mara nyingine kutaka kumwaga pesa za kupata saini yake.
Wahenga wanasema dalili ya mvua ni mawingu. Kutokana na uwepo wa tetesi hizo kwa muda sasa zinampa picha Bocco namna ya kujitafsiri msimu huu utakuwa wa aina gani, ingawa Kibongobongo mchezaji akifanya vizuri kila kitu kinasahaulika.
Katika tetesi za Bocco kutaka kuondolewa kikosini ilielezwa uongozi wa Simba ulitaka kumpa majukumu mengine kati ya umeneja na ukocha wa timu za vijana, jambo lililodaiwa hakukubaliana nalo ikidaiwa anataka kucheza.
Bocco anabebwa na takwimu zake za ufungaji ambazo zinazipa ushawishi timu nyingine kuhitaji huduma yake.
Kutokana na uwepo wa tetesi hizo kwa muda mrefu, beki wa zamani wa timu hiyo, Amir Maftah anazungumzia kiufundi anavyomuona Bocco kwamba anajitunza na ndio maana uwanjani anatimiza majukumu vizuri.
“Bocco anazalisha nini uwanjani tangu aanze kucheza pengine kuliko chipukizi wanaokuja nyuma yake na wanamuacha anaendelea kucheza kwa kiwango cha juu. Bocco apiganie kazi inayompa heshima na itaendelea kumpa heshima na mchezaji anaweza akacheza popote,” anasema
Kipa wa zamani wa Yanga, Benjamin Haule anasema kama Bocco bado atafunga basi kiwango chake kitambeba na anaamini ikifika wakati wake anaotakiwa kupumzika ataacha mwenyewe.
“Si tu Bocco anataka kucheza, pia anafunga. Ni kweli umri umeenda, ila sasa kama chipukizi hawakupi mahitaji kocha utachagua kipi umri ama kiwango cha mchezaji,” anahoji Haule.
Beki wa Mtibwa Sugar, Oscar Masai anasema kati ya washambuliaji anaowahofia wakati wa mechi dhidi ya Simba ni Bocco kutokana na kutumia akili kubwa anapolisogelea goli.
“Bocco namfahamu jinsi anavyojitunza tangu akiwa Azam FC, anajua anachokifanya na ni mfano wa kuigwa kwa vijana wengine. Wakati mwingine ukiona changamoto za kutaka kuachwa, basi zinaweza zikakupa nguvu zaidi ya kupambana na kufanya vitu bora zaidi,” anasema.
Abdi Banda, Mtanzania anayekipiga Afrika Kusini katika klabu ya Richardsbay FC maatrufu Natal Rich Boys anasema ni kawaida kwa mchezaji kupanda kiwango na kushuka, na kinachotakiwa ni yeye kusimamia ndoto zake bila kuangalia anaambiwa nini wakati gani.
“Mfano mzuri ni mimi mwenyewe. Kuna kipindi nilirejea Tanzania kujitafuta upya, sasa nipo nacheza nje. Maneno ya watu wengi yalikuwa Banda kafulia kiwango, ila hayakunifanya nikate tamaa badala yake yalinifanya nizidi kupambana zaidi. Kikubwa Bocco achukulie kwa upande wa kujenga thamani kubwa zaidi,” anasema.
Rekodi zinazoonyesha Bocco ni mkali na bora wa kupachika mabao tangu alipoanza kucheza Ligi Kuu Bara akiwa na kikosi cha Azam FC mwaka 2008 hadi sasa akiwa Simba ambapo amefikisha mabao 151.