Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hili la kuahirisha tuzo ni kiburi kuwa sugu

Tuzooooooooooooo Hili la kuahirisha tuzo ni kiburi kuwa sugu

Mon, 3 Jun 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Mechi ya Fainali ya Ligi ya Mabingwa wa Ulaya baina ya Borussia Dortmund na Real Madrid iliyofanyika juzi usiku imehitimisha msimu wa soka barani Ulaya, huku wachezaji wasioteuliwa timu zao za taifa wakienda mapumzikoni na wengine katika kambi za mataifa yao kujiandaa na mechi za awali za Kombe la Dunia.

Kwa mara ya 15, Real Madrid imetwaa taji hilo kubwa Ulaya baada ya kuishinda Dortmund kwa mabao 2-0 na kuifanya klabu hiyo ya jijini Madrid kuwa yenye mafanikio kuliko klabu nyingine duniani.

Msimu umehitimishwa kwa mechi hiyo baada ya nchi zote wanachama wa Chama cha Soka Ulaya (UEFA) kumaliza ligi zao na makandokando yake, yaani kuwatuza wale waliostahili tuzo kama Mchezaji Bora wa msimu (M.V.P), Mfungaji Bora, Mchezaji Mdogo zaidi, Kipa Bora na nyinginezo.

Wote walioshinda hawazidai nchi zao kwa kuwa sherehe za kuwatuza zilishafanyika mapema, baadhi zikiwa zimefanyika kabla ya mechi mbili za mwisho za ligi na nyingine siku chache baada ya mechi za mwisho wa msimu.

Tuzo pekee kubwa inayosubiriwa kwa sasa ni ile ya Mpira wa Dhahabu (Ballon d’Or) ambayo hutolewa na Gazeti la France Football, ambalo safari hii litashirikiana na UEFA kuandaa tuzo hizo, wakati ile ya Mchezaji Bora wa Mwaka ya Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa) itatolewa mapema mwakani kutokana na utaratibu wa shirikisho hilo kwenda na mwaka wa kalenda na si wa msimu.

Hivyo tuzo hizo hupangwa na taasisi husika kulingana na taratibu za shughuli zake za mpira wa miguu. Fifa huendesha sherehe hizo Januari na uchakachuaji au uchambuzi huanzia Januari ya mwaka uliotangulia hadi Januari ya mwaka husika.

Fifa haiwezi kuandaa tuzo hizo kwa msimu kwa kuwa suala hilo liko ndani ya nchi wanachama wake. Na ikifanya mwishoni mwa msimu inaweza kugongana na shughuli za vyama vingine vingi, hivyo kuiathiri sherehe yake au kuathiri sherehe za vyama wanachama.

Wiki iliyopita, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lilitangaza kuahirisha sherehe za tuzo za wanamichezo bora hadi mwanzoni mwa msimu ujao, taarifa ambayo imeshangaza wengi walioandika mitandaoni kukosoa na wengine kudiriki hata kutukana viongozi.

Hazikuwa kauli nzuri dhidi ya viongozi, lakini inaonekana kama kuna kiburi fulani kinazidi kujengeka miongoni mwa viongozi kiasi kwamba maoni au ukosoaji wa wadau wa soka sasa unaonekana ni upuuzi na kelele masikioni mwa viongozi.

Vitu vinaanza kubadilishwa taratibu bila ya kuwa na sababu za msingi za kubadili na wala haufanyiki mkutano na waandishi wa habari kutangaza habari kubwa kama hiyo, ili kunapokuwepo utata ufafanuliwe na habari ichapishwe ikiwa kamilifu. Lakini kwa kile kiburi cha “watasema, watachoka”€inatolewa taarifa kwa vyombo vya habari yenye aya tatu zisizo na ufafanuzi wowote, halafu viongozi wanakaa kimya kusubiri hizo kelele zipigwe hadi ‘zikome’.

Sasa kuahirishaahirisha mambo kimekuwa kitu cha kawaida na kelele za kupinga uahirishaji mechi hadi ligi inakuwa ya viporo, zinasubiriwa ziibuke halafu zipotee. Sasa taasisi haioni umuhimu wa kuwajibika kwa wadau wake wakubwa ambao ni mashabiki kwa sababu wamezoea kupiga kelele.

Nataka kuamini kuwa hakuna sababu za msingi za kuahirisha shughuli hizo na kama ipo basi ni uzembe ambao mamlaka zinaona haya kuuanika hadharani kwa kuwa labda umefanywa na marafiki.

Lakini yote haya naona ni sababu ya TFF kutomudu kuendesha shughuli hizo. Awali, sherehe za kuzawadia wachezaji waliofanya vizuri katika msimu zilikuwa hazihudhuriwi na wachezaji au makocha waliokuwa wanatajwa kuwania tuzo,. Na badala yake walijazana waandishi wa habari ambao ndio waliokuwa wanapokea tuzo hizo kwa niaba ya washindi.

Badala ya kufikiria jinsi ya kuziboresha ili ziwe na mvuto zaidi, TFF wakaingiza kwenye kanuni zake ulazima kwa wachezaji kuhudhuria na kwamba asiyehudhuria ataadhibiwa kwa kufungiwa kucheza mechi tatu. Yaani mambo ya nje ya uwanja ambayo si ya lazima ingawa ni muhimu, yanahamia uwanjani.

Lakini hoja haikuwa wachezaji kuhudhuria, hoja ni ubora wa shughhuli yenyewe ambao hutokana na maandalizi mazuri na kuzingatia haki katika kupata washindi. Ni fedheha kwa mchezaji anayeona anastahili tuzo kwenda kuhudhuria sherehe ambayo anadhani mchezaji mwingine asiye na ubora ndiye anayependelewa na mamlaka ashinde tuzo.

Na hili huanza kuonekana wakati wanapotangazwa watu watatu wa mwisho wanaowania tuzo. Hapo ndipo huanza maneno kwamba fulani atashinda kwa sababu fulani - usisahau humo siasa za Simba, Yanga na sasa Azam, pia siasa za wachezaji wageni na wazawa hata kama hawatastahili.

Tayari mashabiki washaanza kuhisi kwamba tuzo hizo zitatolewa kwa kuweka uwiano. Kwamba Stephane Aziz Ki ameshashinda tuzo ya Mfungaji Bora, basi ni lazima mamlaka zitapeleka tuzo ya Mwanasoka Bora wa Mwaka kwa mchezaji mwingine -- tena mzawa hata kama raia huyo wa Burkina Faso anastahili zote.

Haya ndio mambo yanayozipotezea heshima na kukubalika kwa tuzo za Mwanasoka Bora wa TFF na si wachezaji kutohudhuria.

Kana kwamba TFF na Bodi ya Ligi Kuu zilikuwa hazijui kwamba Ligi Kuu itaisha Mei, uamuzi wa kuziahirisha umekuja siku chache baada ya msimu kuisha. Unajiuliza kama kweli kulikuwa na watu ambao wanashughulika na tuzo tu kuanzia Agosti mwaka jana hadi Mei, na kama walikumbana na vikwazo vyovyote wakatoa taarifa mapema kwamba huenda ikashindikana kuandaa mwaka huu.

Sababu kwamba zimeahirishwa kwa lengo la kuziboresha haitoshi kuhalalisha tuzo zisifanyike mwaka huu kwa kiwango chake cha sasa. Uboreshaji wa tamasha kama hilo ni mchakato wa muda mrefu ambao ungehusisha mawasiliano na baadhi ya wadau hadi pendekezo la tamasha jipya linapotoka na baadaye kuridhiwa na mamlaka.

Lakini eti uahirishe tamasha la mwaka huu kwa lengo la kuziboresha ni sababu ambayo haitoshelezi kueleza kwa kina kilichotokea.

Kwa hiyo kuna kila dalili kwamba hizi ni sherehe ambazo bado zinaisumbua TFF na hivyo ni muhimu shirikisho hilo likatafuta njia za kuliboresha na si kuhangaika na sababu ambazo zinaonekana ni kituko mbele za watu makini. Ni afadhali ingesema kwa mwaka huu hazitafanyika, ingeeleweka.

Ni muhimu sana kwa TFF kuacha tabia inayoonekana kuwa sugu ya kupuuza maoni ya wadau kwa kuwa kiburi hicho ndicho kinazidi kusababisha iendelee kufanya uamuzi mbovu bila ya kujua kuwa inaurudisha mpira kule nyuma ambako serikali ikawa inalazimika kuingilia kati kwa lengo la kunyoosha mambo ingawa ni kinyume cha utaratibu wa Fifa.

Kama TFF imekosea, ni muhimu ikakiri imekosea na kutafuta njia za kurekebisha na si kuziba masikio. Hicho ni kiburi.

Chanzo: Mwanaspoti