Shina la utani wa jadi lilinza mwaka 1936 ambapo baadhi ya wachezaji waliugomea uongozi wa New Youngs na kuamua kujitenga na timu. Walijiita majina mbalimbali mpaka walifikia kujiita Sunderland kulikuwa na majina ya ‘Stanley’, Eagle of Night- (Tai wa Usiku). Sunderland ilivuma sana Dar es Salaam na vijana walioanzisha walitoka katika madrasa ya Maalim Bu-Hamis.
WALIBANIWA
Kipindi hicho mambo ya wazalendo yalikuwa hayatangazwi na Gazeti la kikoloni la Tanganyika Standard lililoanza Januari Mosi, 1930 halikuandika kabisa habari za Sunderland wala New Youngs, hilo likafanya kumbukumbu nyingi za zama hizo kuwategemea wazee.
Wazee wanasema katika miaka 1944 mpaka 1946, Sunderland ilivuma sana na wanakiri ilikuwa ikipata tabu kwa New Youngs ambayo baadaye ilibadilisha jina na kujiita Young Africans maarufu kama Yanga.
Hapo ndipo utani wa jadi ulipokolea na inadaiwa kipindi fulani Sunderland haikufua dafu mbele ya Yanga isipokuwa kwenye baadhi ya mashindano. Kumbukumbu zinaonesha Sunderland ilikuwa bingwa wa Dar es Salaam mwaka 1964-65 na 1965-66.
UTANI UMEKOMAA
Hadi kufikia miaka hii utani wa Simba na Yanga ulikuwa umekomaa na ilifikia hatua kila Mtanzania lazima atakuwa na upande. Hadi leo watu wanaulizana ‘Wewe ni Simba au Yanga?’ sio kwa watu wa kawaida tu, kwani hata viongozi wa serikali na vyama vya kisiasa wamegawanyika katika pande hizo mbili.
SIKIA HII
Miaka ya 60, mwanakamati mmoja wa Yanga alijiuzulu alipochagiliwa kuwa kiongozi wa serikali na chama. Wasiwasi wake mkubwa ulikuwa ni kwamba asingeweza kutoa hukumu katika masuala ya michezo.
Kisa kingine ni kiongozi mmoja wa kisiasa alipoikana Yanga hadharani pamoja na kufahamika kwamba alikuwa ni mwanachama wa klabu hiyo.
KIGOGO WA FAT NAYE
Wakati fulani kiongozi mmoja wa Chama cha Soka cha Tanzania (wakati huo FAT) alipoulizwa kama yeye ni mwanachama wa Yanga alikana. Kitu cha ajabu baada ya kustaafu uongozi na Yanga kubeba ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati Zanzibar Januari 13, 1975 alifurahia uhusiano wake na Yanga hadharani.
YANGA TANU, SIMBA A.N.C
Mambo ya Simba na Yanga yaliwachanganya sana wanasiasa na Julai 17, 1975 mbunge wa Kigoma (wakati huo) Losa Yemba alizungumzia jambo hilo. Yemba alisema anadhani Yanga ina uhusiano na chama cha siasa cha Tanu na Simba inakipinga chama hicho na kuwa na uhusiano na chama cha African National Congress (A.N.C).
Yemba alisema sababu kubwa ni rangi za timu hizo kushabiana na vyama hivyo, wakati ile ya Yanga ikifanana na Tanu, rangi ya Simba ilifanana sana na A.N.C kilichopingana na Tanu katika uchaguzi wa mwaka 1962.
MTEMVU KUMBE YANGA
Hata hivyo, ilikuja kufahamika baadaye kwamba Rais wa A.N.C Zuberi Mtemvu alikuwa ni kadi ya uanachama wa Yanga! Hii ni mifano michache inayoonesha kuwapo kwa uhasama na utani kati ya Simba na Yanga.
YANGA NI SERIKALI?
Jambo hili lilisemwa sana kwa kuitaja Yanga kama klabu ya serikali. Inawezekana jambo hilo lilikuzwa kutokana na historia ya Yanga ambapo wanachama wake ni watu waliokuwa na marafiki wengi serikalini na ndani ya chama cha Tanu. Lakini je, wanachama wa Simba hawakuwa na ndugu, wachama serikalini na kwenye chama?
Hayo ndio maneno yaliyozidisha ubishi na kutafuta viongozi gani ni wapenzi wa Simba na Yanga.
Kimsingi hakuna jambo baya kama mtu kuwa shabiki wa Yanga au Simba kwasababu utatakiwa kutoa uamuzi dhidi ya timu nyingine hasa unapokuwa na madaraka.
SIMBA NA YANGA ZIFUTWE
Mwaka 1970 baadhi ya watu waliiomba serikali izifute Simba na Yanga ili kufuta utani wao ambao ulileta uhasama ndani ya jamii. Hata hivyo ilibainika kufanya hivyo isingekuwa suluhu kwa kuwa wanachama hao wangeungana tena na kutumia majina mengine.