Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hili 'bato' la kibabe

Sopu Azam Fc.jpeg Hili 'bato' la kibabe

Mon, 12 Jun 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wazungu wangeiita Battle of Titans, lakini sisi tunaitambua kama vita ya wababe wawili, Yanga dhidi ya Azam, ambao wanatakutana leo kwenye fainali ya Kombe la Shirikisho pale Mkwakwani, Tanga huku kila upande ukiwa na dhamira tofauti.

Ni dhamira tofauti kwa sababu ni mechi ambayo inakutanisha timu mbili – moja ikiwa katika msimu wake bora zaidi ikifanikisha takriban kila jambo, dhidi ya timu nyingine ambayo inahitaji kupata angalau kitu cha kuonyesha baada ya kufanya usajili mkubwa zaidi katika miaka ya karibuni.

Azam katika dirisha kubwa la usajili iliwaleta kina James Akaminko, Kipre Junior, Tape Edinho, Pape Malickou Ndoye, Isah Ndala, Idris Mbombo, Rodgers Kola, Ali Ahamada, Abdul Suleiman ‘Sopu’ ambao pamoja na kina Prince Dube, Ayoub Lyanga, Kenneth Muguna, Sospeter Bajana na wengineo wameunda kikosi ambacho ukisoma majina kabla ya mechi unaweza usiingize timu uwanjani.

Na ndio maana kushinda Kombe la Shirikisho la Azam Sports dhidi ya Yanga leo ni muhimu, lakini kila mmoja anatambua kwamba hilo sio lengo lao mama la kukusanya kikosi kilichojaa vipaji kiasi hiki – lakini itakuwa ni katika hatua muhimu za kukua.

MARUDIO YA 2015-2016

Mechi ya leo ni kama marudio ya fainali za msimu wa kwanza wa ASFC mara michuano hiyo iliporejeshwa na TFF ya Jamal Malinzi, baada ya Kombe la FA kusimama kwa muda mrefu tangu ilipochezwa mwaka 2002 na JKT Ruvu kubeba taji hilo.

Katika msimu huo wa kwanza wa ASFC, Yanga ilikutana na Azam kwenye fainali kali iliyopigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa (enzi hizo Uwanja wa Taifa) na kushuhudiwa Yanga ikishinda kwa mabao 3-1.

Yanga ilipata mabao yake siku hiyo kupitia Amissi Tambwe, Simon Msuva na Deus Kaseke, huku bao la kufutia machozi la Azam liliwekwa kimiani na Didier Kavumbagu aliyetokea benchi kumpokea nahodha, John Bocco.

AZAM WANAKAMIA?

Mechi kati ya Yanga na Azam haijawahi kuwa nyepesi na takwimu zinaonyesha. Takwimu za ushindi na idadi ya mabao ya kufungana kati ya timu hizi zinashabihiana sana.

Pengine ndio maana straika wa Yanga, Fiston Mayele akajikuta matatani baada ya kudai kwamba “Azam FC inakamia sana inapocheza dhidi ya timu kubwa za Simba na Yanga lakini utaisahau inapokutana na kina Namungo.”

Zimepostiwa video nyingi za mechi za Azam dhidi ya Simba na Azam dhidi ya Yanga ambazo “makosa ya kiubinadamu” yameinyima haki Azam na kuzibeba Simba na Yanga.

Mayele anaweza kuwa amekosea kutoa kauli hiyp ambayo kwa hakika itachochea “kukamiana zaidi” leo pale Mkwakwani, lakini pia Mayele anaweza kuwa na pointi katika madai yake kama ameangalia matokeo ya mechi kati ya Azam na timu hizo nyingine nje ya Simba na Yanga. Ni kweli Azam inaonewa hata inapocheza na Ihefu, Dodoma Jiji, KMC na Prisons? Labda.

Hata kama inaonewa dhidi ya Simba na Yanga, lakini msimu huu imepoteza mechi moja tu kati ya nne ilizocheza dhidi ya timu hizo mbili, ikilala 3-2 dhidi ya Yanga. Imeshinda moja 1-0 dhidi ya Simba na kutoka sare mbili (1-1 dhidi ya Simba na 2-2 dhidi ya Yanga).

Azam msimu huu imepoteza mechi saba na kutoka sare tano. Yaani kati ya mechi saba ilizopoteza msimu mzima, mechi sita imepoteza dhidi ya timu ambazo sio Simba wala Yanga!

Lakini hili bado haliondoi ukweli kwamba kauli ya Mayele itawasha moto kwenye mechi ya leo jijini Tanga, japo mwenyewe hatakuwapo uwanjani.

Pia mechi ya leo ndio itakayoamua Mfungaji Bora wa msimu kati ya Andrew Simchimba wa Ihefu ambayo ilishaaga michuano hiyo mapema akiwa na mabao saba, akifuatiwa na Mzize mwenye mabao sita, huku Abdul Suleiman 'Sopu' wa Azam aliyetwaa tuzo msimu uliopita kwa mabao tisa akiwa na Coastal Union, naye atasikilizia kwani hadi sasa ana mabao matatu.

ISHU FEI TOTO

Na si kauli ya Mayele pekee itakayowasha moto katika mechi ya leo, jingine ni ishu ya usajili uliojaa utata wa Feisal Salum kutoka Yanga kwenda Azam.

Ligi ikiwa katikati ya msimu, kiungo aliyekuwa kipenzi cha Wanayanga, Feisal Salum ‘Fei Toto’ akaliamsha dude. Akagoma kujiunga na timu hiyo ya Wananchi akisema haitaki tena na kwamba anataka kuvunja mkataba.

Azam ikahusishwa na tukio hilo ikituhumiwa kukiuka taratibu za Fifa za usajili kwa kuongea na mchezaji aliye katika mkataba na timu nyingine, tuhuma ambazo Azam ilizikana vikali ikijiweka kando na saga nzima ya Fei, ambaye alikaa nje ya timu kwa miezi sita na pengine angekaa hivyo hadi mkataba wake ukatapomalizika mwisho wa msimu, kwa sababu mamlaka za soka nchini zilisisitiza yeye ni mchezaji halali wa Yanga huku mwenyewe akisema kamwe hawezi kurejea klabuni hapo labda Rais wa klabu hiyo, Injinia Hersi aondoke. Hata hivyo, baada ya Rais Samia Hassan kuingilia kati ili kuokoa jahazi, klabu iliyokuwa ikituhumiwa kuongea naye kinyume cha taratibu za Fifa ya Azam ndiyo ambayo fasta ilijitokeza na kumsajili.

Ndio maana sakata la Fei na kauli ya Mayele vinajumuika katika kuchochea ushindani uliokuwapo kiasili kati ya timu hizo za jiji moja la Dar es Salaam kuleta ‘Battle of Titans’ pale Mkwakwani leo.

MBINGU YA SABA

Azam kumaliza nafasi ya tatu kwenye Ligi Kuu msimu huu sio malengo ya kikosi kilichojaa wachezaji wenye vipaji kama hivi kwa sababu Wanalambalamba wameshawahi kuwa na mafanikio makubwa wakitwaa ubingwa wa ligi tena bila ya kupoteza mchezo msimu wa 2013-14.

Ndio maana ni lazima wapambane kutwaa ubingwa wa Kombe la ASFC leo dhidi ya timu bora iliyopata mafanikio na rekodi zinazoifanya ijione kama iko kwenye mbingu ya saba.

Katika msimu bora zaidi kihistoria, Yanga imetwaa Ngao ya Jamii dhidi ya Simba, imebeba taji la pili mfululizo la Ligi Kuu Bara na la 29 kiujumla, imeweka rekodi ya kuwa timu ya kwanza Tanzania kucheza mechi 49 za ligi mfululizo bila ya kupoteza na kubwa kuliko yote, tangu imeasisiwa 1935, imefika fainali yake ya kwanza ya CAF katika Kombe la Shirikisho Afrika, ambako ilikosa kombe kwa sheria ya mabao mengi ya ugenini baada ya sare ya 2-2 dhidi ya USM Alger. Ilifungwa 2-1 Dar es Salaam, ikaenda kuwazamisha Waarabu kwao 1-0.

Ikaandika rekodi nyingi ikiwamo kumaliza kinara wa kundi lake CAF, kushinda mechi tano za ugenini, zikiwamo mbili za Uarabuni (Algeria na Tunisia) na huku straika wake Fiston Mayele akiibuka Mfungaji Bora wa Kombe la Shirikisho Afrika kwa mabao yake saba na akigawana tuzo ya Mfungaji Bora wa Ligi Kuu Bara na Saido Ntibazonkiza wa Simba kila mmoja akiwa na mabao 17.

SAFARI ILIVYOKUWA

Hadi kufika hatua hiyo, Yanga kma ilivyo Azam na timu nyingine za Ligi Kuu bara zilianza mechi za ASFC kwa msimu huu raundi ya tatu.

Yanga iliifumua Kurugenzi FC ya Kigoma kwa mabao 8-0, huku Azam ikiikandamiza Malimao Fc ya Rukwa kwa mabao 9-0 na kutinga raundi ya nne ambayo ni 32 Bora, huku Azam iliifunga Dodoma Jiji kwa mabao 4-1 na Yanga kugawa dozi ya 7-0 kwa Rhino Rangers ya Tabora na kuingia 16 Bora maarufu kama raundi ya tano, ambapo Vijana wa Nabi waliinyoa Tanzania Prisons pia kwa 4-1.

Hatua ya robo fainali, Yanga ilipangwa kucheza na Geita Gold na kuifunga bao 1-0, ilihali Azam yenyewe ilipewa Mtibwa Sugar na kuifumua mabao 2-0 na zote kutinga nusu fainali ambapo Yanga ilipangwa kuvaana na Singida Big Stars na Azam kupewa Simba, mechi zikichezwa Liti, Singida na Nangwanda Sijaona, Mtwara.

Yanga iliitambia Singida kwa bao 1-0, huku Azam ikiitupa nje Simba kwa mabao 2-1 na sasa kukutana fainali leo Mkwakwani, ili kuamua mbabe wa michuano hiyo iliyoasisiwa rasmi mwaka 1967 na kubadilishwa badilishwa majina kabla ya Azam Media kuidhamini na kuitwa ASFC.

KIKOSI KIPANA

Wakati Azam ikiwa na kikosi kinachoweza kukufanya usiingize timu, Yanga ina kikosi kipana ambacho kimekuwa kikitumiwa vyema na kocha ‘Profesa’ Nasreddine Nabi, ambaye mafanikio ya timu hiyo yote msimu huu na uliopita yametokea chini yake na msaidizi wake Cedrick Kaze na uongozi mzima kuanzia Rais Hersi hadi wadhamini GSM.

Kikosi cha Yanga kimejaa watu wa maana kabisa ambao wamesababisha hadi kutungiwa wimbo “ukiona Aziz KI kaanzia benchi usishangae ni mtego huo,” huku sub za Nabi zikibadili matokeo mara kwa mara.

Ni kwa sababu alipokosekana Djigui Diarra, alidaka Aboutwalib Mshery au Metacha Mnata. Kulia alipoanzia benchi Djuma Shaban, alicheza Kibwana Shomary au Kibwana alipocheza kushoto, Joyce Lomalisa alianzia kwenye mbao ndefu. Pale beki ya kati alicheza Bakar Mwamnyeto na Ibrahim Bacca, au Dickson Job angecheza na mmoja kati ya hao au hata MVP wa Ligi Kuu msimu uliopita Yannick Bangala angeondoka katika eneo la kiungo kuja kucheza beki ya kati. Kule kiungo atabaki Khalid Aucho na Salum Abubakar ‘Sure Boy’. Hata Fei alipochemka, Aziz KI aliifungia Yanga bao lililoipeleka timu hatua ya makundi ya Shirikisho. Fei alipoamua kwenda Azam, Yanga ilifika fainali ya Afrika. Hata hivyo Fiston Mayele ambaye amekuwa na kismati cha kuifunga Azam tangu alipotua nchini msimu uliopita hatakuwepo sambamba na Aziz KI ambao wameondoka nchini kwenda kuwahi kambi za timu za taifa za DR Congo na Burkina Faso zinazojiandaa na mechi za kufuzu Afcon 2023 zitakazofanyika Ivory Coast mwakani.

Bernard Morrison alipoenda kwao, Jesus Moloko na Tuisila Kisinda waliwasha moto, alipochoka Mayele aliingia Clement Mnzize na waliposajiliwa Kennedy Musonda na Mudathir Yahya wote walikuwa na mchango mkubwa katika kumalizia msimu kibabe.

Wale mafundi wa mpira wa Azam FC na hawa mastaa wa timu ya Wananchi wote watakuwapo Mkwakwani leo. Patachimbika!

FAINALI ZILIZOPITA ASFC

2015/16 - Yanga 3-1 Azam

2016/17 - Simba 2-1 Mbao

2017/18 - Singida 2-3 Mtibwa Sugar

2018/19 - Lipuli 0-1 Azam FC

2019/20 - Simba 2-1 Namungo

2020/21 - Yanga 0-1 Simba

2021/22 - Yanga 3-3 Coastal Union (4-1 penalti).

Chanzo: www.tanzaniaweb.live