Ombi la Simba kutumia Uwanja wa Azam Complex katika mchezo wake wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Coastal Union, utakaopigwa kesho limegonga mwamba kwa kile kinachoelezwa viongozi wa timu hiyo kutoweka wazi sababu.
Mchezo huo wa mzunguko wa tatu ulipangwa kuchezwa kwenye Uwanja wa Uhuru ila viongozi wa Simba waliomba kupelekwa Chamazi jambo ambalo Bodi ya Ligi (TPLB) limewakataliwa kutokana na kutoeleza sababu za kuhamisha.
Kwa mujibu wa kanuni ya 15 ya TPLB ibara ya tatu inaeleza timu itakayohitaji kubadilisha uwanja wa kuchezea ni lazima ianishe sababu za kufanya hivyo jambo ambalo viongozi wa Simba walishindwa kuweka sababu hizo.
Simba ilianza msimu kwa ushindi wa mabao 4-2 dhidi ya Mtibwa Sugar na kisha kuifunga 2-0 Dodoma Jiji huku Coastal Union ikianza kwa kichapo cha 2-1 mbele ya Dodoma Jiji na kulazimishwa sare ya 1-1 na Mtibwa Sugar.
Coastal inaingia katika mchezo huo huku ikiwa haina rekodi nzuri mbele ya Simba kwani mara yao ya mwisho kukutana ilichapwa mabao 3-1, Juni 9, mwaka huu yaliyofungwa na Saidi Ntibazonkiza 'Saido' aliyefunga mawili na John Bocco.
Bao pekee la Coastal katika mchezo huo lilifungwa na aliyekuwa nyota wa kikosi hicho Mcameroon, Moubarack Amza.