Kuumia kwa Mlinda Lango chaguo la Kwanza, adhabu mbili za Kadi Nyekundu na kukosekana kwa baadhi ya wachezaji vijana waliopandishwa kutoka kikosi B, kumetajwa kama sababu ya Mtibwa Sugar kupoteza mchezo dhidi ya Simba SC jana Jumapili (Oktoba 30).
Mchezo huo uliopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam ulishuhudia wenyeji Simba SC ikichomoza na ushindi wa 5-0, huku Mtibwa Sugar ikiwapoteza wachezaji Pascal Kitenge na Casian Ponela walioneshwa Kadi Nyekundu.
Kocha Mkuu wa Mtibwa Sugar Salum Shaban Mayanga amesema, kushindwa kuendelea kwa Mlinda Lango wake kutoka nchini Kenya Farouk Shikalo aliyepata majeraha ya goti baada ya kukongana na Mshambuliaji wa Simba SC Pape Sakho na adhabu ya Kadi Nyekundu kuliigharimu sana timu yake hadi kufikia kupoteza kwa idadi kubwa ya mabao.
“Nikiri nina shida kwenye eneo la kuzuia ikiwa ni pamoja na Mlinda Lango Faruk Shikhalo, tulimweka nje tukafanya marekebisho, amerejea mechi iliyopita iliyopita alifanya vizuri mechi hii alianza vizuri lakini amepata maumivu ya goti ameshindwa kuendelea.”
“Vijana ambao nilianza kuwatumia bahati nzuri wameitwa kwenye timu za Taifa wanahudumia nchi. Kwa hiyo nikiri kwenye eneo hilo pia limeniumiza.”
“Kadi Nyekundu tulizopata nazo zimetugharimu sana katika mchezo huu, kwa hiyo niseme nimekubaliana na hali hii na hakuna lingine zaidi ya kujiandaa na mchezo wetu ujao dhidi ya Azam FC.” amesema Mayanga
Kupoteza kwenye mchezo dhidi ya Simba SC, kumeifanya Mtibwa Sugar kusalia na alama 15 zinazoiweka kwenye nafasi ya nne, sawa na Namungo FC inayoshika nafasi ya tatu ikiwa na alama 15.