Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hiki ndicho alichoambiwa Nabi kuhusu Club Africain

NABI ONE TWOOO.jpeg Kocha Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi

Wed, 9 Nov 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Yanga ipo Tunisia tayari kwa mchezo wa marudiano dhidi ya Club Africain utakaopigwa leo, lakini kocha Nabi Mohammed akathibitisha kupata taarifa muhimu na za siri za wenyeji.

Kocha Nabi ambaye ni raia wa Tunisia alisema anafahamu Africain waliwapumzisha winga wao mmoja hatari na mshambuliaji wa mwisho ambao watawatumia katika mchezo wa leo Jumatano.

“Nina marafiki hapa wengi wamekuwa wakinipa taarifa za kutosha, nafahamu kwamba kwa jinsi walivyocheza mfumo wa kujilinda kuna wachezaji wawili nimeshatajiwa kwamba watacheza kwenye mchezo ujao,” alisema Nabi.

“Sisi tutajiandaa kwa mkakati wetu wa kutafuta ushindi wa kukabiliana na yoyote, kitu bora zaidi kama nilivyosema kabla tunatakiwa kutuliza kasi yao ya kushambulia.

“Watatumia sana mabeki wao wa pembeni na mawinga kutushambulia kwa nguvu kitu pekee kitakachotuweka salama ni jinsi tutakavyotekeleza majukumu ya kuzuia kwa kushirikiana na sio kwa wachache.”

Mashabiki wa Etoile ambao viongozi wao wamewaasa vigogo wa Yanga kutuliza timu, wanaamini Club Africain nyepesi zaidi kutokana kukosa wachezaji bora ingawa wamewatahadharisha haitakuwa rahisi.

Kwa upande wa uongozi wa klabu ya Yanga kupitia Msemaji wao, Ally Kamwe alisema; “Tupo vizuri na mazoezi yetu tukiwa hapa yalienda sawa, hakuna majeruhi yoyote yule na hata Sure Boy (Salum Aboubakar) ambaye tulikuja naye akiwa anaumwa na yeye amejiunga na wenzake kwenye mazoezi na anaendelea vizuri”

“Kule Tunis kuna viongozi wetu watatu ambao walishatangulia kwa ajili ya kuweka mazingira sawa na kila kitu kinaenda sawa hakuna tabu yoyote, kikosi kipo kwenye hali nzuri na tunaenda kupambana na wachezaji wote morali ipo juu kwa ajili ya mchezo huu.”

Yanga inahitaji ushindi ama sare yoyote ya mabao ili kurejea ilichofanya mwaka 2016 na 2018 ilipotinga makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika ikitokea Ligi ya Mabingwa Afrika ikizitoa kibabe Sagrada Esperança ya Angola na Welayta Dicha ya Ethiopia kwa kuzifunga kila moja mabao 2-1.

Yanga ilikwamia raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu kwa kung’olewa na Al Hilal ya Sudan kwa jumla ya mabao 2-1.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live