Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hii ya JKU kuchezea mechi zote Misri kuna namna

JKU 2024 Hii ya JKU kuchezea mechi zote Misri kuna namna

Tue, 13 Aug 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Kutokana na umuhimu wa mechi za mashindano ya Shirikisho la Soka la Afrika (CAF)( na yale ya Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa), masuala ya ubora wa viwanja vinavyotumika yamepewa umuhimu mkubwa ili kila timu icheze katika mazingira yasiyo na faida kwa mwenyeji au mgeni.

Ndio maana Uwanja wa Benjamin Mkapa umekuwa mwenyeji wa mechi nyingi zisizohusisha timu za Tanzania, hata kama zimo katika mashindano hayo makubwa kwa ngazi ya klabu au timu za taifa.

Nchi kama Burundi, Sudan Kusini na hata Kenya zimeshindwa kutumia viwanja vyake vizuri vya nyumbani kutokana na takwa hilo la CAF na Fifa, huku baadhi ya nchi zikiathirika kutokana na viwanja vyake kuwa kwenye ukarabati mkubwa utakaowezesha ziwe na uwezo wa kuwa mwenyeji wa mechi kubwa zaidi.

Hii ni faida kwa nchi ambazo zina miundo mbinu inayokidhi viwango vya CAF na Fifa. Yaani kama Tanzania tuna uwanja kama wa Benjamin Mkapa na Azam Complex ambavyo vinakidhi vigezo vya mashirika hayo makubwa, maana yake tuna faida za kimichezo, kibiashara na kijamii kwa sababu mechi nyingi za CAF na Fifa zinaweza kufanyika hapa kwetu. Ukizingatia kwamba nchi nyingi kwa sasa zinataka kutumia utalii kama moja ya vyanzo vikubwa vya mapato ya fedha za kigeni, miundombinu hiyo inakuwa sehemu muhimu ya mikakati ya kuhakikisha kwamba utalii unaingiza fedha nyingi kwa kutumia michezo, hasa mpira wa miguu ambao ni maarufu kwa sit u ukanda wa Afrika Mashariki, bali Afrika na dunia nzima.

Katika mazingira hayo unategemea kwamba kila taasisi inayohusika katika uhusiano wa kimataifa, itakuwa na hiyo akili kwamba ni muhimu kuweka mbele suala la uzalendo na utalii badala ya kufanya mambo klwa maslahi ya taasisi pekee au watu binafsi nma kusahau yale ya kitaifa.

Nasema hivi kwa sababu nimesoma kwenye vyombo vya habari kuhusu uamuzi wa klabu ya Jeshi la Kujenga Uchumi Zanzibar (JKU) kuchgezea mechi zake zote mbili nchini Misri, badala ya utaratibu wa kawaida wa kila timu kucheza mechi yake ya nyumbani kwenye nchi yake.

Klabu za Zanzibar zinashiriki katika mashindano ya klabu ya Afrika baada ya CAF kutoa haki ya upendeleo kwa visiwa vya Zanzibar kuwa mwanachama wake wa muda, licha ya kanuni kuu za uanachama wa Fifa kueleza wazi kuwa nchi inayopewa uanachama wake ni ile inayokidhi vigezo vya Umoja wa Mataifa (UN) kuwa taifa kamili.

Ndio maana klabu za Zanzibar zinashiriki mashindano ya Afrika, lakini timu ya taifa ya visiwa hivyo haiwezi kushiriki mashindano ya CAF wala Fifa, isipokuwa yale ya kihistoria ya ukanda wa Baraza la Vyama vya Soka vya Afrika Mashariki (Cecafa).

Kwa hiyo, JKU imepata nafasi ya kushiriki hatua za awali Ligi ya Mabingwa wa Afrika kutokana na haki hiyo iliyotolewa na CAF kwa visiwa hivyo. Matarajio ni kwamba haki hiyo itaungamanishwa na mikakati ya serikali ya Zanzibar na ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kukuza utalii na kuipeleka Tanzania juu zaidi ya sehemu iliyopo sasa.

Lakini kitendo cha uongozi wa klabu ya JKU kinaonekana kukinzana na dhamira hiyo ya serikali na pia malengo ya nchi kwa ujumla katika ushiriki wake wa masuala ya kimataifa.

Akiongea na Mwanaspoti wiki iliyopita, Kocha wa JKU, Haji Salum alisema kuwa uamuzi wa kuchezea Misri mechi zao zote mbili za raundi ya awali ya mashindano ya Klabu Bingwa ya Afrika umetokana na udhamini walioupata.

Alisema udhamini huo ni pamoja na kulipiwa gharama za safari kwenda Misri, gharama za kambi, gharama za kufanya utalii, gharama za uwanja wa mazoezi, gharama za mafunzo kwa makocha na pia kuiingiza shule ya soka ya jeshi hilo kwenye program za klabu ya Pyramids.

Hii timu inayiogharimiwa mambo yote hayo ndiyo inategemewa kuweka upinzanin kwa Pyramids wa kuwania nafasi ya kuvuka raundi ya awali, kwenda raundi ya kwanza, hatua ya makundi, robo fainali, nusu fainali na fainali. Itafikika huko ikiwa imegharimiwa kila kitu na timu ambahyo ina malengo hayohayo kwenye mashindano hayohayo!

Haiingii akilini kuwa hilo linawezekana kwa jinsi yoyote ile, labda makubaliano hayo yawe baina ya Waisraeli na Wapalestina ambao ni aghalabu sana kukiuka misingi yao. Lakini kwa nchi kama zetu ambazo hazina tofauti kubwa za kiasilia, mpango kama huo unakuwa na harufu ya rushwa na kama si rushwa basi ni umbumbumbu wa viongozi kuhusu masuala mapana ya kitaifa.

Haiwezekani Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ikahangaika kufanya maboresho makubwa kwenye Uwanja wa Amaan ili uweze kutumika kwa mechi za kimataifa, halafu klabu zinazotakiwa kuutumia zikaamua kujipa ukimbizi usio wa lazima eti kwa sababu zimepata udhamini wa malazi, safari, uwanja wa mazoezi na utalii. Haiwezekani!

Ni lazima kuna kitu nyuma ya uamuzi huo wote. KIbaya zaidi ni kwamba JKU ni taasisi ya serikali ambayo inatakiwa iwe na ufahamu dhidi ya vitendo vya kuidhalilishba serikali kwamba haiwezi kumudu gharama za safari, malazi, utalii na uwanja wa mazoezi.

Kwamba viongozi wa JKU hawajui umuhimu wa suala la utalii katika ushiriki wa klabu hiyo katika mashindano ya kimataifa, kiasi kwamba klabu inaamua kwenda kufanya utalii Misri badala ya wapinzani wao kuja Zanzibar wakati wa mechi hizo za CAF na kufanya utalii ambao utaliingizia taifa fedha.

Kwamba macho ya viongozi wa JKU yamefumbwa kiasi cha kutoona hayo mawili na mengine mengi ya kutumia Uwanja wa Amaan kwa mechi za kimataifa za klabu katika kipindi ambacho Tanzania, Kenya na Uganda zimepewa fursa za kuandaa fainali za Mataifa ya Afrika za mwaka 2027 (Afcon 2027).

Unahitaji kuwa na viongozi mbumbumbu kutojua hayo yote na mengine mengi, na kama si mbumbumbu basi kuna ufisadi mkubwa nyuma yake unaolenga kunufaisha watu binafsi na si nchi.

Ni muhimu vyombo husika vikajitokeza kuhoji haya yote na kutoa taarifa kuhusu uwezekano wa aibu hii kubwa inalolikabili taifa kama hatua zisipochukuliwa mapema.

Chanzo: Mwanaspoti