Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hii ni Singida FG ya kimataifa

Onyango Singida FG Hii ni Singida FG ya kimataifa

Sat, 8 Jul 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Usajili unaoendelea kufanywa na Singida Fountain Gate unaonekana kulenga zaidi mahitaji ya ushiriki wa kimataifa msimu ujao kutokana na sifa za wachezaji iliowabakisha kikosini, inaowasajili na inaohusishwa nao.

Singida FG itakayoshiriki Kombe la Shirikisho Afrika msimu ujao, inaonekana kuwapa kipaumbele zaidi wachezaji wenye uzoefu wa mechi za kimataifa, lakini pia ikitanua ukubwa wa kikosi chake kwa kulipa benchi lao la ufundi wachezaji wasiopungua wawili wasiopishana sana.

Kwa kuanzia, timu hiyo imeongeza mikataba ya nyota wake, Bruno Gomes, Yusuph Kagoma, Aziz Andabwile na Benedict Haule, huku ikifanikiwa kuwanasa Beno Kakolanya, Nico Wadada, Dickson Ambundo na David Bryson.

Wakati ikiwanasa hao, timu hiyo inahusishwa na usajili wa winga Bernard Morrison, mabeki Joash Onyango na Yahaya Mbegu, pamoja na mshambuliaji Habibu Kiyombo.

Kakolanya ana uzoefu mkubwa wa mechi za kimataifa, ambao aliupata wakati alipokuwa akiitumikia Simba ambapo ilitinga katika hatua ya robo fainali ya mashindano ya klabu Afrika mara tatu tofauti, huku Ambundo na Bryson wakiupata katika kikosi cha Yanga kilichotinga fainali ya Kombe la Shirikisho msimu ulimalizika, ingawa watatu wote hao hawakuwa na namba katika kikosi cha kwanza.

Wadada ambaye Singida FG imemsajili kutokea Ihefu SC, amecheza idadi kubwa ya mechi za kimataifa akiwa na kikosi cha timu ya Taifa ya Uganda, Azam FC na Vipers.

Katika kundi la wachezaji ambao inahusishwa kuwasajili, ni Mbegu tu ambaye anaonekana kutokuwa na uzoefu wa mechi za kimataifa tofauti na Morrison, Onyango na Kyombo.

Kwa upande wake, Morrison ana uzoefu wa kimataifa alioupata kwa kuzitumikia Yanga, Simba, Motema pembe, Orlando Pirates na AS Vita Club, huku Kyombo akiupata kwa kuitumikia Simba na Taifa Stars.

Onyango ameitumikia kwa muda mrefu timu ya Taifa ya Kenya 'Harambee Stars', lakini pia kwa ngazi ya klabu, ameupata uzoefu kupitia Simba na Gor Mahia.

Ikiwa Singida Fountain Gate itakamilisha usajili wa wachezaji wote hao, upande wa golini machaguo yao yatakuwa ni Beno Kakolanya na Haule na msaidizi wao akiwa ni Ibrahim Rashid.

Katika nafasi ya beki wa kulia watakuwa na Wadada na Paul Godfrey wakati beki wa kushoto ni Bryson na Yassin Mustafa na mabeki wa kati ni Onyango, Pascal Wawa, Beiems Carno, Abdulmajid Mangalo na Hamad Waziri.

Nafasi ya kiungo wa ulinzi watakuwa na Kagoma, Kelvin Nashoni na Aziz Andabwile wakati ile ya kiungo wa kushambulia wakiwa na Bruno, Said Ndemla na Ibrahim Ajibu

Machaguo yao upande wa winga yatakuwa ni Morrison, Bright Adjei Nassor Saadun, Deus Kaseke na Nicholas Gyan, wakati washambuliaji wa kati ni Francis Kazadi, Medie Kagere, Habibu Kyombo na Amissi Tambwe.

Kocha wa Singida Fountain Gate, Hans Pluijm alisema kuwa usajili wao unaakisi malengo yao katika mashindano ya kimataifa msimu ujao.

"Tunakwenda kushiriki katika mashindano magumu ambayo yanahitaji wachezaji wazuri na wazoefu hivyo ni lazima usajili wetu zuingatia mahitaji hayo. Tumekuwa na kikosi kizuri lakini tunahitaji maingizo mapya machache ambayo yataimarisha zaidi," alisema Pluijm.

Mkurugenzi wa utawala wa timu hiyo, Muhibu Kanu alisema usajili wanaoufanya ni wa wachezaji wa kuongeza thamani ya kikosi chao kwani ni wa daraja la juu na wana uzoefu mkubwa.

Chanzo: Mwanaspoti