Afisa Mtendaji Mkuu wa Simba SC, Iman Kajula, ameibuka na kubainisha kwamba, wamekuja na mpango mkakati maalum msimu huu wa 2023/24 utakaowawezesha kubeba makombe yote waliyoyakosa katika misimu miwili mfululizo ambayo yalibebwa na Young Africans.
Kauli hiyo imekuja mara baada ya Simba SC kuwapoka Young Africans kombe la kwanza la Ngao ya Jamii walilolichukua juzi Jumapili (Agosti 13) kwenye Fainali ya Ngao ya Jamii iliyochezwa Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
Simba SC ilifanikiwa kubeba ubingwa huo kwa ushindi wa Penati 3-1 dhidi ya Young Africans.
Kajula amesema Kombe lao la kwanza la Ngao ya Jamii walilolichukua ndiyo mwanzo, kwani katika msimu huu wamekuja na mpango maalum mkakati wa kuhakikisha wanapata matokeo mazuri ya ushindi kila mchezo utakaokuwepo mbele yao.
Kajula amesema kwa sasa nguvu na akili zao wamezielekeza katika ubingwa wa Ligi Kuu Bara, Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’ na Kombe la Mapinduzi ili kuhakikiksha wanarejesha furaha ya mashabiki.
“Ni furaha kuona mpango mkakati maalum tuliouandaa viongozi wa kuhakikisha tunayarejesha makombe yote ya ndani katika msimu huu kuanza vizuri kwa kuchukua Ngao ya Jamii.
“Huo ndiyo mwanzo wa mpango wetu mkakati ambao tumeupanga uongozi, sasa hivi tunaelekeza nguvu katika ubingwa wa Ligi na Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’, msimu huu ninaamini ndio wenye mafanikio makubwa kwetu,” amesema Kajula.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa Simba SC, Murtaza Mangungu, amesema ahadi yake ya kuifunga Young Africans, bado inaendelea na watafanya hivyo hadi atakapoondoka madarakani.
“Kama uongozi malengo yetu ni makubwa msimu huu, ikiwemo kuyarejesha makombe yote tuliyoyakosa katika misimu miwili iliyopita, tumeanza na Ngao ya Jamii, yanafuata mengine sambamba na kuendelea kuwafunga Young Africans kila tutakapokutana nao,” amesema Mangungu.