Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hii ndiyo Ivory Coast usiyoijua

Ivory Coast Hii ndiyo Ivory Coast usiyoijua

Sat, 13 Jan 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Ile siku ndio leo. Pazia la Fainali za Afcon 2023 linafunguliwa na mataifa 24 yote yameshafika Ivory Coast kuwania taji hilo kubwa Afrika.

Mashabiki mbalimbali pia wamesafiri hadi nchi hiyom kushuhudia miamba hiyo ikipepetuana kumsaka mfalme wa Afrika. Taji hilo kwa sasa linashikiliwa na Senegal ya Sadio Mane. Itakuaje mwaka huu, subiri tuone.

Hata hivyo, kwa mashabiki wanaosafiri kwenda kushuhudia michuano hiyo kuna mambo watakutana nayo huko ambayo ni tofauti na yaliyo nchini mwao ikiwamo utamaduni, vyakula na mambo mengine mengi.

Hapa tunakuletea baadhi ya mambo hayo yanayopatikana zaidi kwenye nchi hiyo ya Afrika Magharibi na ambayo huyajui kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2021, inakadiriwa kuwa na watu milioni 27.

ABIDJAN SIO MJI MKUU

Wengi wanaijua Ivory Coast na jiji maarufu Abidjan. Hata hivyo wasilolifahamu, ni mji huo ni mkubwa na wa kibiashara na ndio unaojulikana kuliko miji mingine yote nje ya Ivory Coast.

Kama ilivyo kwa Tanzania, Jiji la Dar es Salaam ndio linalofahamika ndani na nje ya nchi na ndio jiji la kibiashara linalopokea wageni na biashara nyingi, lakini Mji Mkuu ni Dodoma.

Ndivyo ilivyo kwa Ivory Coast, wengi wanajua Jiji la Abidjan ndio mji mkuu au makao makuu ya nchi, ila Makao makuu ya nchi hiyo yapo katika Jiji la Yamoussoukro.

KWA NINI TEMBO

Jina la timu ya taifa ya nchi hiyo ni Tembo. Hata hivyo, wengi hawajui kwa nini imeitwa hivyo. Ni hivi. Neno Tembo sio tu jina la timu ya taifa bali ni la nchi yao. Hii ni kutokana na nchi hiyo kuwa ndiyo pekee kwenye Ukanda wa Afrika Magharibi ilikuwa na idadi kubwa ya wanyama hao na kutumika kama utambulisho wa taifa hilo.

Kwa mujibu wa tovuti ya Newscientis, utafiti uliofanywa mwaka 1996 ulibainisha nchi hiyo ilikuwa na tembo kati ya 3000 hadi 5000.

Lakini kwa sasa nchi hiyo imebakiwa na jina tu na idadi kubwa ya tembo imeshatoweka, utafiti mwingine uliofanywa mwaka 2020 ulibainisha imebakiwa na tembo wasiozidi 300.

KANISA KUBWA DUNIANI

Moja ya vivutio vikubwa vya utalii, ni kanisa maarufu la Basilica of Our Lady of Peace, lililoko Mji Mkuu wa Yamoussoukro.

Ni kanisa kubwa zaidi duniani kuliko hata kanisa la St Peter’s Basilica lililoko Jiji la Vatican, Italia.

Kanisa hilo lina uwezo wa kuingiza zaidi ya watu 30,000 na lilijengwa mwaka 1990 kwa zaidi ya Euro 7 milioni.

Limetegenezwa kwa aina ya kipekee na mbali ya sehemu ya kuabudia, kuna maeneo ya makazi ya wafanyakazi wake na watalii na watu wengi hupata changamoto ya kufanya ibadqa kutokana na idadi kubwa ya watu.

UHALIFU

Hii ni tahadhari kwa wanaokwenda huko. Uhalifu nje nje. Kwa kifupi suala la usalama ni mdogo. Watu wanalizwa mchana kweupe na hasa watalii na wanaibiwa vitu vya thamani kama saa, simu,pesa na vito vingine vya thamani.

Pia uhalifu mkubwa unaofanyika huko ni wa magari kutekwa na hasa mabasi na magari madogo.

Kuna madaraja mawili ambayo ukipita lazima uache chochote, Houphouet-Boigny na De Gaulle yaliyoko Abidjan. Pia hufanyika uhalifu wa kutumia silaha hasa kwenye maduka na migahawa mikubwa nchini huko na uhalifu huo hufanyika mchana kweupe.

Maeneo mengine ya hatari ni The Guiglo, Kaskazini mwa Bouak, kwenye Jiji la Seguela.

SAFU YA MILIMA NIMBA

Tanzania kuna Kilimanjaro ndio kivutio kikubwa kwa upande wa milima. Ivory Coast kuna safu ya milima Nimba, inayotenganisha nchi za Ivory Coast, Liberia na Guinea ambako upo kwa kiasi kikubwa.

Safu hiyo ya milima imezungukwa na misitu mikubwa. Ni moja ya vivutio vikubwa vya utalii nchini huko na wageni wamekuwa wakifika kutembelea na kujionea madhari yake ikiwamo viumbe hai vinavyopatikana huko kama wanyama, ndege na mimea.

KAKAO KWA WINGI

Kama wewe ni mpenda vinywaji vya moto basi utakutana navyo Ivory Coast. Zao la kakao ndio maarufu nchini huko na duniani kwa jumla. Ndio wazalishaji wakubwa wa zao hilo duniani.

Hadi mwaka 2013 ilikuwa imesafrikisha zaidi ya tani milioni moja zuilizouzwa nje ya nchi hiyo, sawa na asilimia 31.6 ya kakao zote duniani.

Nchi hiyo inafuatiwa na Ghana kwa Afrika inayozalisha asilimia 18.99 na ndiyo ya tatu duniani.

Kwa mujibu wa Wikipedia, kakao linaiingizia Ivory Coast asilimia 40 ya pato la taifa kwa bidhaa zinazosafirishwa nje ya nchi.

VYAKULA

Ukiwa huko, moja ya vyakula maarufu ni wali unaochanganywa na karaga za kusaga zinazosimama kama mboga na unaweza kula bila ya kuweka mboga za majani, nyanya au bamia.

Pia kuku wa kuchemsha na huliwa na wali, ni moja ya vyakula ghali zaidi ukiwa huko.

Chakula kingine ni ndizi za kusaga zinazopikwa (kusongwa) kama ugali na huliwa na mafuta ya mawese na karanga. Chakula hiki huitwa Foutou ama Banana Fufu.

Tofauti na mataifa mengine ya Afrika ya Magharibi hutumia viazi vitamu vinavyosongwa kama ugali na kuliwa na mboga wanayotaka.

Chanzo: Mwanaspoti