Aliyefanya skauti ya kumleta kiungo Clatous Chama, katika klabu ya Simba anastahili heshima ya kubarikiwa jicho la kuona kipaji hicho kwa kufanya uamuzi wa kumsajili staa huyo.
Kwa mara ya kwanza Chama alijunga na Simba 2018 akitokea klabu ya Dynamos ya Lusaka, ambapo msimu wa 2020/21 alikuwa kinara wa asisti 15 Ligi Kuu na alifunga mabao manane.
Baada ya kumalizika kwa msimu huu (2020/21) alinunuliwa na RS Berkane ya Morocco ambako hakufanya vizuri akarejea tena Msimbazi msimu uliopita na sasa ndiye kinara wa asisti 14 kwenye ligi inayoendelea na amefunga mabao matatu.
Chama ambaye amechezea Zesco United (2016), Al Ittihad (2017), Dynamos (2017/18) na sasa Simba ana uzoefu na michuano ya kimataifa na amekuwa mhimili muhimu ndani ya klabu hiyo, kwani zipo mechi alizoamua matokeo.
Mwanaspoti linakuchambulia kwa njia ya data baadhi ya mechi ambazo ameivusha Simba kutoka sehemu moja kwenda nyingine Ligi ya Mabingwa Afrika, huku baadhi ya wadau wakisifu ukomavu wa kutumia akili kufanya maamuzi akiwa kwenye majukumu yake.
2018, SIMBA VS NKANA
Chama aliwapa raha mashabiki wa Simba baada ya kufunga bao la tatu la kisigino dakika ya 89 timu hiyo ikishinda 3-1 dhidi ya Nkana ya Zambia, ambapo ugenini ilichapwa 2-1, hivyo ikatinga hatua ya makundi CAF (Desemba 23, 2018) kwa jumla ya mabao 4-3.
2018-19 SIMBA VS AS VITA
Machi 17, 2019, Chama aliivusha Simba kwenda robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kufunga bao la pili dakika ya 90, baada ya bao la kusawazisha la Mohammed Hussein dakika ya 36. AS Vita ilianza kufunga dakika 13 kupitia Kazad Kasengu.
2021, SIMBA VS FC PLATINUM
Februari 6, 2021 Uwanja wa Benjamin Mkapa, Simba ikishinda mabao 4-0 dhidi ya FC Platinum Chama ndiye aliyefunga la mwisho lililoipeleka timu hiyo hatua ya makundi, ambapo ugenini Wekundu wa Msimbazi walipoteza kwa bao 1-0.
2021, SIMBA VS VITA
Aprili 12, 2021 hatua ya makundi katika ushindi wa Simba wa mabao 4-1 dhidi ya AS Vita, Uwanja wa Benjamin Mkapa, Chama alifunga mabao mawili dakika ya 45+1, 84 mengine yalifungwa na Luis Miqquisone dakika ya 30 na Larry Bwalya dakika ya 66 pia timu hiyo ilishinda bao 1-0 ugenini.
2022/23 ALICHOKIFANYA SIMBA VS BIG BULLETS
Simba dhidi ya Big Bullets, ikishinda mabao 2-0 ugenini dakika ya 30 Moses Phiri alifunga bao la tikitaka mpira wa kutenga ulianzia kwa Chama kisha Kibu Denis akaupiga kwa kichwa, huku bao la pili lililofungwa na John Bocco dakika ya 83 asisti ilikuwa ya Chama (Sept 10, 2022).
Mechi ya marudiano ya Septemba 14, Simba ilishinda mabao 2-0 yakifungwa na Phiri, Chama alitoa pasi ya bao la dakika ya 29 na bao la pili lilifungwa dakika ya 50.
SIMBA VS DE AGOSTO
Simba ilishinda mabao 3-1 ugenini dhidi ya Primeiro de Agosto, Chama alitupia dakika ya 9 na kutoa asisti ya bao la Phiri dakika ya 76, bao lingine lilifungwa na Israel Patrick Mwenda dakika ya 63 ambapo Chama alipiga mpira wa kutenga ukamkuta Sadio Kanoute alitoa pasi ya bao (Oktoba 9,2022) Mchezo wa marudiano Oktoba 16,Phiri alifunga dakika ya 33 pasi ilikuwa ya Mohamed Hussein ‘Tshabalala’.
Big Bullets 0-2 Simba (Sept 10/2022),Simba 2-0 Big Bullets(Sept 14/2022),Primeiro de Agosto 1-3 Simba (Oktoba 9/2022)
Simba 1-0 Primeiro de Agosto (Oktoba 16/2022).
MITAZAMO YA WADAU
Jicho la kiufundi la beki wa zamani wa Simba na Stars, Boniface Pawasa linaona Chama anatumia zaidi akili kuliko nguvu na kwamba anacheza soka bila presha.
“Licha ya kipaji chake ana nidhamu inayomfanya alinde kiwango chake.”
Mtazamo wa Pawasa haukukinzani na wa Kocha wa Yanga B, Said Maulidi ‘SMG’ anayesema michuano hiyo inahitaji akili zaidi na mbinu, kitu alichokiri anakiona anachokifanya Chama.
“Chama anatumia akili sana kufanya kazi yake, hiyo itawasaidia sana Simba kwenye mechi za CAF ambazo zipo mbele yao, jambo ambalo linatakiwa kufanywa na kila mchezaji ili kushinda mechi hizo,” anasema Maulizi ambaye alishawahi kukipiga Simba.