Jioni ya Februari 11 huenda ikawa ni siku mbaya kwa wapenda Kandanda nchini baada ya kusambaa kwa taarifa ya kifo cha aliyekuwa beki wa Ruvu Shooting Ally Mtoni Sonso kilichotokea katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
"Tumebaki na vilio". Ni kauli ya Ofisa Habari wa Ruvu Shooting, Masau Bwire akithibitisha kifo cha aliyekuwa mchezaji wao, beki Ally Mtoni 'Sonso' aliyefariki muda mchache wakati akipelekwa Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Imeelezwa kuwa kabla ya kukutwa na umauti huo, Sonso nyota wa zamani wa Lipuli, Yanga, Kagera Sugar na Ruvu Shooting alikuwa akiuguza majeraha ya mguu tangu Oktoba mwaka jana.
Bwire amesema kuwa, mchezaji huyo amefariki wakati akipelekwa Hospitali ya Taifa, Muhimbili baada ya kuuguza mguu wake tangu mchezo wao wa Ligi Kuu dhidi ya Simba, uliopigwa uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.
"Ni vilio na simanzi kwa taarifa hii tuliyopokea wakati timu ikiendelea na mazoezi, alikuwa kiungo kwenye klabu akiipa matumaini ya kufanya vizuri, alianza kuelezea maumivu ya mguu tangu mchezo wetu na Simba akawa anauguza taratibu" amesema Bwire.
Aidha ameongeza kuwa, taratibu za mazishi zinaendelea ambapo marehemu atazikwa nyumbani kwao, Kondoa Magomeni kesho Jumamosi.
"Mke wake ndiye alianza kunipigia akitoa kilio, baadaye Baba yake aliniambia hivyo na muda huu naelekea nyumbani kwao kwa taratibu za mazishi hapo kesho Jumamosi sambamba na timu nzima kwa ujumla, hakika tutamkumbuka" amesema Bwire.