Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hii hapa sapraizi ya Gamondi kwa Belouizdad

Aziz Diarra Okrah Gamondi Yanga K Hii hapa sapraizi ya Gamondi kwa Belouizdad

Fri, 23 Feb 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Hawataamini. Ndicho alichosema kocha Miguel Gamondi wakati akiwazungumzia wapinzani wa Yanga, CR Belouizdad katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika itakayopigwa Jumamosi kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa Dar es Salaam.

Gamondi amesema Yanga imeandaa sapraizi kwa ajili ya mechi hiyo muhimu ya kuamua hatima ya Wanajangwani kwenye kampeni za kuwania kufuzu hatua ya robo fainali ya michuano hiyo mikubwa zaidi kwa ngazi ya klabu barani Afrika.

Kocha huyo Muargentina amewatisha wapinzani wake akiwaambia kuwa kikosi chake kitashuka na sapraizi mpya kabisa ya kusaka mabao.

Akizungumza mara baada ya mazoezi ya timu hiyo, Gamondi amesema kikosi chake kitawaheshimu Belouizdad kitakapokutana nao kwenye mechi ya marudiano lakini Waarabu hao watakutana na mabadiliko makubwa ya mbinu zao za kusaka mabao.

Gamondi ameendelea kuwatisha Belouizdad akisema kitu anachofurahia wachezaji wake wameyashika kwa haraka mabadiliko ya mbinu anazoendelea kuzifanyia kazi kambini kwao Avic.

Mapema jana, Yanga kabla ya kuanza mazoezi yake ilitangulia kuangalia mikanda ya mechi tofauti ya wapinzani wao wanapocheza ugenini na hata zile za nyumbani Gamondi akiwa na mtaalam wa kuchambua mechi za wapinzani Mpho Maruping.

Baada ya darasa hilo kazi ikahamia katika mazoezi ya uwanjani yaliyotumia saa mbili huku mazoezi ya kushambulia yakitumia saa moja na dakika kadhaa.

Gamondi amekuwa akiwabadilishia mbinu viungo wake kutoka katikati ya uwanja Pacome Zouzoua, Maxi Nzengeli na hata Stephanie Aziz KI ya namna ya kupiga pasi za mabao na hata wao wenyewe kufunga.

Viungo hao wote watatu kwenye mazoezi hayo walifanikiwa kufunga mabao matatu huku Gamondi akisikika akiwapongeza kila walipofanya balaa la kufunga mabao makali kwa namna alivyokuwa anataka.

Mazoezi hayo yaliwachanganya mabeki wa Yanga wakiongozwa na Ibrahim Hamad 'Bacca; akionekana kila wakati kuwalaumu wenzake kwa kushindwa kutegua mitego ya viungo hao.

Mbele ya viungo hao Gamondi amekuwa pia akiwabadilisha washambuliaji wake Kennedy Musonda, Clement Mzinze, Joseph Guede ambaye mazoezini ana moto mkali wa kujua kufunga huku kila mmoja akifunga mabao mawili wakibadilishwa badilishwa kwa kucheza kwa kupishana.

"Tunataka kuhakikisha tunashinda Jumamosi, tunajua tulipoteza vipi mechi iliyopita lakini safari hii tutakuwa nyumbani tutakuwa na mabadiliko makubwa ambayo tunaamini yatatupa urahisi wa kushinda," amesema Gamondi.

"Tunafahamu tunakwenda kukutana na timu ngumu lakini mashabiki wetu wanajua nguvu yetu tunapokuwa nyumbani, kama nilivyosema awali kwamba tunahitaji kushinda lakini hatutashinda kama hatutatengeneza nafasi na hata kuzitumia kwa wingi."

"Nafurahi kuona kila mchezaji anaonyesha kushika kwa haraka kile ambacho tunataka kifanyike, kitu nawaomba mashabiki wetu ni waje wajae uwanjani ili wapinzani wetu wajue ukubwa wa hii klabu bingwa hapa Tanzania."

Yanga ina kibarua kigumu dhidi ya Belouizdad ambayo iliifunga timu hiyo ya Wananchi 3-0 katika mechi yao ya kwanza ya Kundi D kule Algeria.

Wanajangwani walitawala mechi ile ya Novemba 24, 2022, lakini walishangazwa kwa mabao ya mashambulizi ya kushtukiza huku Belouizdad wakionekana kuwa tishio kila walipoiba mpira katika nusu yao ya uwanja na kupiga mipira mirefu iliyowachanganya walinzi wa Yanga. 

Ilikuwa ni wazi kwamba Belouizdad siku ile haikutaka kushindana pasi na Yanga na kwa kufanya hivyo kwenye uwanja wa nyumbani, ni wazi itacheza mara mbili ya vile ilivyokuwa ikijilinda ikiwa ugenini Kwa Mkapa Jumamosi hii.

Belouizdad pia imetokea kuwalazimisha sare ya bila mabao mabingwa wa Afrika na vinara wa kundi D, Al Ahly katika mechi yao ya kiporo kule Algeria wiki iliyopita.

Hii inafanya Kundi D ama Group D kubeba kabisa jina lake la utani la Group of Death (Kundi la Kifo) kutokana na timu zote nne kutofautiana kwa pointi mbili tu, huku timu Al Ahly ikiongoza kwa pointi 6, Belouizdad na Yanga zikiwa zimelingana kwa kuwa na pointi 5 kila moja baada ya mechi nne, huku Medeama inayoshika mkia ikiwa na pointi 4. 

Kule kwao, kwenye Ligi Kuu ya Algeria, moja ya ligi ngumu zaidi barani Afrika, Belouizdad inashika nafasi ya pili katika msimamo ikiwa na pointi 31 katika mechi 16, ikifunga mabao 23 na kuruhusu 11. Imeshinda mechi 9, sare 4 imepoteza 3.

Kwenye ligi ya nyumbani, ambayo inatajwa kuwa ni Na.6 kwa ubora Afrika, Yanga inaongoza ikiwa na pointi 43 baada ya mechi 16, sawa na za Belouizdad ambao kule kwao wamecheza na kuvuna pointi 31 katika nafasi ya pili nyuma ya MC Alger yenye pointi 39 baada ya mechi 16 pia.

Yanga katika mechi hizo 16 za Ligi Kuu Bara, imeshinda 14, sare moja na imepoteza moja. Imefunga mabao 39 na kuruhusu mabao 8. Hii ni dalili njema kwamba timu inatembea na ina uwezo wa kufunga mabao mengi.

Huku mastaa wake wakiwa wamekamilika kikosini; Stephane Aziz Ki, Djigui Diarra, Pacome Zouzoua, Maxi Nzengeli na wengineo, Yanga inatarajiwa kucheza kiwerevu zaidi ili kushinda mechi hiyo muhimu.

Matokeo mengine yoyote nje ya ushindi yataiweka Yanga katika wakati mgumu kwani italazimika kwenda kushinda mechi ya mwisho ugenini dhidi ya timu yenye mafaniko makubwa zaidi ya nyingine yoyote katika michuano hiyo ikilibeba taji la Ligi ya Mabingwa Afrika mara 11, Al Ahly.

RATIBA KUNDI D

IJUMAA, FEBRUARI 23, 2024

Medeama v Al Ahly (saa 1:00 usiku)

JUMAMOSI, FEBRUARI 24, 2024

Yanga v CR Belouizdad (saa 1:00 usiku)

MSIMAMO KUNDI D

                               P      W     D    L      F      A         Pts

1. Al Ahly              4       1      3    0      4      1            6   

2. Belouizdad       4       1     2    1      4      2             5

3. Yanga                4       1     2    1      5      5             5

Chanzo: www.tanzaniaweb.live