Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hii hapa safari ya Kipagwile kisoka

Kipagwile Pic Data Hii hapa safari ya Kipagwile kisoka

Sun, 27 Mar 2022 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Mashabiki wa soka wamemzoea kwa jina la ‘Mtoto Idd’ wakirejea ngoma matata ya Sir Juma Nature iliyowahi kubamba ‘longtime’, lakini majina yake kamili ni Idd Kipagwile, winga matata anayekipiga KMC kwa mkopo akitokea Azam FC.

Kabla ya KMC, jamaa alishapita timu za Majimaji, Namungo na Azam, huku kiwango chake kikipanda na kushuka, haya hapa mahojiano yake ambapo kufunguka mambo kadhaa ikiwamo maisha yake ya kuhama kila mara akidai yeye kambi popote.

ALIPOANZIA

Kipagwile anasema alianzia timu ya vijana ya Simba ‘B’ ila kutokana na kiwango alichoonyesha kiliwavutia Majimaji na kusajiliwa kuitumikia klabu hiyo kabla ya mabosi wa Azam kumwaga mkwanja na kumchukua kuwatumikia kwa msimu wa 2016/17.

“Ninachokiamini kwenye kila jambo ni kupambana na kuwa mvumilivu maana haya mambo mengine yanakuja tu, ninapopata nafasi nitahakikisha naitumia vizuri.” anasema.

CIOABA AMVUTA AZAM

Anasema aliyekuwa kocha wa Azam Mromania, Aristica Cioaba ndiye aliyependekeza asajiliwe na kitendo cha kufanikisha dili hilo kilimpa mwanga kwenye maisha yake.

“Ilikuwa kama ndoto kwangu kwa sababu hadi unaona timu kubwa kama Azam inakuhitaji lazima utajisikia furaha kwa kuwa ni malengo ya kila mchezaji.” anasema.

AZAM YAMPA MJENGO

Kuna mwamko sana wa wachezaji hivi sasa kutamani kufanya mambo makubwa ya kimaisha na kwa Kipagwile napo ni hivyo hivyo kwani Azam imempa maisha na kuweza kujenga mjengo wake nyumbani kwao huko Songea.

“Nilipopata pesa yangu ya usajili Azam niliamua kujenga nyumbani Songea, hiki ni kitu kikubwa sana kwa sababu hujui kesho yako na ndiyo maana nimeamua kuanza huko na hapa nilipofikia naamini mambo mazuri mengine yatakuja.”

KUMBE SIMBA ILIMTAKA

Kabla ya kutua Azam, Kipagwile anasema alihitajika na Simba lakini mtu wake wa karibu alimshauri kwenda Azam kutokana na kuahidiwa kupata kila kitu kwa wakati.

“Nilikuwa nahitaji kucheza timu kubwa na ofa zilikuja kipindi kile lakini kaka yangu ambaye ananishauri mambo mengi aliniambia niende Azam na kweli nilivyofika nilipata kila kitu kwa wakati.”

Aliongeza, baada ya Azam kuifunga Simba katika fainali ya Kombe la Mapinduzi mwaka 2018, alikuwa akihusishwa kwenda tena Simba, ingawa hakuna kiongozi yeyote ambaye alifika kuzungumza naye.

“Hakuna kiongozi yeyote wa Simba ambaye alinifuata, tetesi tu zilikuwa zinaenea na kuzisikia kama ambavyo watu wengine wanazisikia, inawezekana hawakuja kwa sababu nilikuwa na mkataba wa muda mrefu,” anasema.

MAJERAHA YAMTIBULIA

Anasema wakati anajiunga na Namungo mwaka 2020, majeraha ya goti yalitaka kuhatarisha maisha yake ya soka ila anamshukuru Mungu amerejea na anaendelea kupambana.

“Nilikaa nje ya uwanja kwa miezi sita bila kucheza, kwa hakika ilikuwa msimu mbaya sana kwenye maisha yangu, lakini Mungu ni mwema kwani nimepona na ninaendelea kuonyesha kipaji changu,” anasema.

NDOTO INAYOMTESA

Anasema moja ya malengo makubwa aliyonayo ni kuona siku moja anachukua ubingwa wa Ligi Kuu Bara maana makombe mengine kama Kagame na Mapinduzi amewahi kuchukua akiwa na Azam.

“Vikombe vingine tayari nimeshavaa medali zake, natamani sana nivae medali ya ubingwa wa Ligi Kuu, kama nikivaa nikiwa na KMC ni sawa au sehemu nyingine ila ndoto yangu ni kuvaa medali hiyo.”

HATAMSAHAU KALLY ONGALA

Anasema katika safari yake ya soka hataweza kumsahau mchezaji wa zamani wa Yanga, Azam ambaye pia aliwahi kuwa kocha wa Azam na Majimaji, Kally Ongala ambaye alimsaidia katika ukuaji wa kipaji chake kutokana na misingi aliyokuwa anampatia.

“Nimefundishwa na makocha wengi hadi hapa nilipofikia ila Ongala alinifanya nijione jasiri na nisiyekubali kukatishwa tamaa, hakika atabaki katika kumbukumbu zangu,” anasema.

KUVUKA MIPAKA

Kipagwile pia ana ndoto ya kutoboa na kwenda kujaribu bahati yake nje ya nchi.

“Mipango ipo na lolote linaweza likatokea, zilikuja ofa nyingi ila kipindi kile cha ugonjwa wa Uviko-19 ndicho kilichokwamisha, ila malengo hayo kwangu yapo ya kuhakikisha nasogea mbele zaidi na muda ukifika mtaona na kusikia,” anasema.

AZAM FRESHI TU

Anasema mkataba wake na klabu yake inayommiliki - Azam, unaisha mwisho wa msimu huu na endapo viongozi wataona anawafaa kuwatumikia tena yupo tayari kurejea.

“Nipo tayari kurudi wakinihitaji kwa sababu mpira ni kazi yangu ila kama itashindikana nitaangalia sehemu nyingine ambayo naiona itanifaa.”

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz