Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hii hapa ndoto tamu ya kijiji cha michezo

Kijiji Cha Wananmichezo Hii hapa ndoto tamu ya kijiji cha michezo

Sun, 29 Oct 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Binafsi nimekikumbuka Kijiji cha Wanamichezo kilichokuwa kijengwe katika miaka 1970.

Nimekikumbuka kijiji hicho baada ya kuziona picha za Rais Samia Suluhu Hassan alipomtembelea Jenarali mstaafu Mrisho Sarakikya.

Najua vijana wengi wa sasa hawawezi kukumbuka kitu chochote kuhusu kijiji cha wanamichezo kilichotakiwa kujengwa maeneo ya Chang’ombe jijini Dar es Salaam.

Mbali na kutojua chochote kuhusu kijiji hicho, wengi hawamtambui Jenerali Sarakikya ni nani?

Agosti 20, mwaka huu, Rais Samia alimtembelea mkuu huyo wa kwanza wa majeshi mstaafu Jenerali Sarakikya kumjulia hali nyumbani kwake Mkoaranga, Wilaya ya Arumeru, Arusha.

Unaweza kujiuliza kijiji cha wanamichezo kinahusiana nini na picha hiyo ya Rais Samia na Jenerali Sarakikya. Kwanza kilichonivuta ni jina la Sarakikya hapo nikaukumbuka mchango wake mwingi katika nchi hii.

NDIYE MWASISI WA KIJIJI CHA MICHEZO

Jenerali Sarakikya ambaye amewahi pia kuwa balozi katika nchi mbalimbali, ndiye aliyetoa wazo la kuanzishwa kwa kijiji cha michezo.

Wazo la Sarakikya lilikuja baada ya kuona taifa lilikuwa linatumia pesa nyingi kuwagharamikia wanamichezo wa aina mbalimbali katika kuweka kambi kwenye hoteli za kitalii walipokuwa wakiliwakilisha.

Lengo lingine lilikuwa ni kuwa na kituo kizuri kwa ajili ya wanamichezo. Kituo ambacho kingekuwa na faida kubwa kwa jamii zetu leo hii.

Naamini kama kituo hicho kingekamilika basi Tanzania ingevuna matunda ya vipaji vingi ambavyo vimepotea.

Naamini kama ujenzi wa Dar es Salaam ungekamilika, basi vituo vingine vingi vingejengwa katika mikoa mingine na kuvuna vipaji vya maana kwa taifa letu. Jenerali Sarakikya akiwa Waziri wa Utamaduni wa Taifa na Vijana 1970 alitoa wazo la kujenga kijiji hicho.

NEDCO ILICHORA RAMANI

Ramani ya kijiji hicho ilikuwa imechorwa na Kampuni ya Taifa Usanii na Michoro (NEDCO) na kazi ya ujenzi ilikabidhiwa kwa Kampuni ya Afro Construction ambayo ilikuwa na makao makuu yake mkoani Singida.

KILIKAMILIKA ASILIMIA 20

Hadi mwaka 1982 ni asilimia 20 tu ya ujenzi wa kijiji hicho ndiyo iliyokuwa imefanyiwa kazi. Kijiji hicho kilikuwa kinajengwa karibu na Uwanja wa Taifa (Uwanja wa Uhuru) na Chuo cha Elimu ya Taifa maeneo ya Chang’ombe.

Lakini mwaka 1982, Wizara ya Habari na Utamaduni ilisema ingelazimika kutafuta fedha kwa njia nyingine ili kukamilisha kijiji cha wanamichezo ambacho kilitarajiwa kugharimu Sh2.2 milioni. Hiyo ni kutokana na kutokuwepo kwa fungu la kugharamikia ujenzi huo katika bajeti ya mwaka 1982-83.

Msemaji wa wizara hiyo alithibitisha kwamba hakukuwa na fungu kwa ajili ya ujenzi huo na ujenzi ulisimama tangu 1981.

FEDHA ZA BAHATI NASIBU

Hata hivyo, Wizara ya Habari na Utamaduni ilijipanga kuendeleza ujenzi kwa kutegemea fedha za mfuko maalumu ulioanzishwa na wizira hiyo kwa ajili ya maendeleo ya jamii pamoja na baadhi ya fedha kutoka Bahati Nasibu ya Taifa. Hata hivyo, hadi leo Kijiji cha Wanamichezo kimebaki kuwa ndoto nzuri iliyootwa na Jenerali Sarakikya lakini kwa bahati mbaya pamoja na nia nzuri, ndoto hiyo haikutumia.

Chanzo: Mwanaspoti