Siku chache baada ya kurudishwa Simba, kocha Juma Mgunda ametaja mambo matatu yatakayombeba kwenye mechi nane zilizobaki akianza na sare ya mabao 2-2 dhidi ya Namungo ugenini.
Mgunda ambaye ni kocha wa zamani wa Coastal Union, amerudishwa akitokea timu ya wanawake Simba Queens kuchukua nafasi ya Abdelhak Benchikha ambaye ameachana na timu hiyo kwa kile kilichotajwa ana matatizo ya kifamilia.
Akizungumza na Mwanaspoti, Mgunda ambaye ni miongoni mwa makocha wazawa wazoefu, alisema ana kazi kubwa tatu kuhakikisha anairudisha Simba kwenye ushindani huku akiweka wazi kuwa ni kuwajenga kisaikolojia wachezaji, kurudisha morali na mbinu ambazo zitampa matokeo.
“Sio rahisi lakini nina imani kubwa kwamba nitaisaidia Simba kurudi kwenye ushindani kwa kufanya mambo hayo matatu naamini wachezaji watarudisha timu sehemu nzuri,” alisema na kuongeza;
“Wachezaji waliopo Simba wote wamepevuka wanaelewa namna ya kufanya ili kuiweka timu kwenye ushindani hivyo ili waweze kufanya hivyo muhimu ni kuwajenga kisaikolojia na kuwarudisha kwenye morali,” alisema.
Mgunda alisema hakuna mabadiliko makubwa ndani ya timu wachezaji wengi waliopo tayari ameshafanya nao kazi hivyo hawezi kuweka wazi kuwa anaenda kufundisha namna ya kufunga au kukaba kwani anaamini hiyo kazi tayari wanaifahamu.
“Kusema nimekuja kufundisha ni kujiweka kwenye nafasi mbaya na kutokuwaheshimu watangulizi wote. Wao walikuwa bora na walifanya kazi kwa usahihi na mimi nimekuja na vitu hivyo vitatu kwa kuanzia ili kuweza kumalizia walipoishia wao,” alisema.
Akizungumzia suala la mbinu, Mgunda alisema ni kutokutoa mwanya kwa wapinzani wao kuwachukulia kama timu ya kuchukua pointi wanapambana na wao kusaka pointi zitakazowaweka kwenye nafasi nzuri.
“Huu ni mzunguko wa lala salama kila timu inapambana kujiweka pazuri huku timu nyingine kama Simba tukisaka nafasi katika tatu za juu hivyo nataka kuijenga timu hii kuwa ya ushindani na sio ya kugawa pointi,” alisema.
MGUNDA KAMA KIRAKA
Mgunda kuna wakati anafanya majukumu yake kama kiraka. Baada ya Simba kuachana na Benchikha, hivyo Mgunda kapewa kukaimu nafasi yake, akisaidiana na Seleman Matola na mchezo wake wa kwanza ni sare ya 2-2 dhidi ya Namungo.
DATA ZA BENCHIKHA
Tangu atambulishwe, Benchikha aliiongoza timu hiyo katika jumla ya michezo 21 katika mashindano mbalimbali ikiwemo ya Ligi Kuu Bara, Ligi ya Mabingwa Afrika, Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) na Ligi ya Muungano iliyorejea mwaka huu.
Ligi Kuu Bara michezo 11 alishinda sita, sare mitatu na kufungwa miwili, mabao ya kufunga 18 ya kufungwa manane.
Ni michezo miwili tu ya Ligi Kuu Bara ambayo Benchikha hakuiongoza Simba ambayo ni dhidi ya Coastal Union ambayo timu hiyo ilishinda mabao 2-1 (Machi 9, 2024) na ushindi wa 3-1 mbele ya Singida Fountain Gate uliopigwa Machi 12, mwaka huu.
Kwenye Ligi ya Mabingwa Barani Afrika aliiongoza mechi saba, alishinda miwili, sare miwili na kupoteza mitatu, kikosi chake kiujumla kilifunga mabao manane na kufungwa mabao manne.
Michuano mingine ni ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) ambako Benchikha alijikuta akitolewa mapema tu hatua ya 16 bora dhidi ya Mashujaa, dakika 90 zilimalizika kwa bao 1-1, kisha ikatolewa kwa penalti 6-5.
Katika Ligi ya Muungano iliyorejea mwaka huu baada ya kusimama kwa miaka 22, Benchikha aliiongoza timu hiyo michezo yote miwili na kushinda yote akianza na 2-0, dhidi ya KVZ kisha kuifunga Azam FC bao 1-0 kwenye fainali na kutwaa taji hilo.
Benchikha alijiunga na kikosi hicho Novemba 24, 2023 akitoka kuipa USM Alger ubingwa wa Kombe la Shirikisho Afrika kwa kuibwaga Yanga kwa faida ya bao la ugenini kufuatia sare ya 2-2 na CAF Super Cup mbele ya Al Ahly ya Misri.
MGUNDA 2022/23
Kwa mara ya kwanza Simba, ilimchukua Mgunda kutoka Coastal Union 2022/23 ambapo mchezo wake wa kwanza kusimama benchi ilikuwa dhidi ya Big Bullets 0-2 Simba (Sept 10/2022) wa Ligi ya Mabingwa Afrika, aliziba pengo la aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Zoran Maki.
Mgunda aliiongoza timu katika mechi 16 za Ligi Kuu, akisaidiana na Matola kabla ya kuja kocha Roberto Oliveira ‘Robertinho ambaye naye akatimuliwa mikoba akapewa Benchikha ambaye pia kasepa na timu imerudi mikononi mwa Mgunda.
MECHI ZA MGUNDA 2022/23
Mechi alizoongoza Mgunda ni dhidi ya Prisons 0-1 Simba (Sep 14, 2022), Simba 3-0 Dodoma Jiji (Oktoba 2022), Yanga 1-1 Simba (Oktoba 23, 2022), Azam 1-0 Simba (Oktoba 27),Simba 5-0 Mtibwa Sugar (Oktoba 30, 2022), Singida Big Stars 1-1 Simba (Nov. 11, 2022), Simba 1-0 Ihefu (Nov 12, 2022), Simba 1-0 Namungo (Nov 16, 2022), Ruvu Shooting 0-4 Simba (Nov 19, 2022).
Mbeya City 1-1 Simba (Nov 23, 2022), Polisi Tanzania 1-3 Simba (Nov 27, 2022), Coastal Union 1-3 Simba (Des. 3, 2022), Geita Gold 0-5 Simba (Des 18, 2022), Kagera Sugar 1-1 Simba (Des. 21, 2022), KMC 1-3 Simba (Des 26, 2022), Simba 7-1 Priosns (Des 30, 2022).
Mabao ya kufunga - 37
Ya kufungwa -9
Pointi- 37
HAKUPOTEZA CAF
Big Bullets 0-2 Simba (Sept 10, 2022), Simba 2-0 Big Bullets (Sept 14, 2022), Primeiro de Agosto 1-3 Simba (Oktoba 9, 2022), Simba 1-0 Primeiro de Agosto (Oktoba 16, 2022),
Simba 8-0 Eagle
Simba 1-0 Coastal.
UJIO WA BENCHIKHA
Ujio wa Benchikha ukamuweka kando Mgunda, akaonekana na kikosi cha Simba B, hakukaa sana akapelekwa Simba Queens, akisaidiana na Mussa Mgosi na inaongoza Ligi Kuu ya Wanawake Bara (SWPL).
TAIFA STARS NAKO
Wakati Stars, inacheza michuano ya fainali za Afcon iliyofanyika nchini Ivory Coast, kocha Adel Amrouche alifungiwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) kwa kosa la kutoa kauli ya utata dhidi ya Morocco, Mgunda alikwenda kuziba pengo.
Kocha Jamhuri Kiwelu ‘Julio’ alisema kinachoendelea kwa Mgunda kiliwahi kutokea kwake miaka ya nyuma; “Timu kupita nyakati ngumu ni jambo la kawaida kipindi cha nyuma, nilikuwa naifundisha Simba kwa vipindi tofauti, hivyo naamini Mgunda atamaliza vizuri michezo iliyosalia.”
Kauli yake iliungwa mkono na kocha mkongwe, Abdallah Kibadeni akisema: “Mgunda anawajua wachezaji, waliweza kufanya vizuri, naamini watamaliza msimu salama.”