Mshambuliaji wa Arsenal, Bukayo Saka amesisitiza kuwa yuko tayari kujibu changamoto ya kocha Mikel Arteta ya kucheza mechi 70 msimu huu 2023/24.
Winga huyo wa England mwenye umri wa miaka 22, aliwaongoza Washika Bunduki hao katika ushindi wa mabao 5-0 dhidi ya Sheffield United Jumamosi (Oktoba 28) na kuwaweka ndani ya pointi mbili nyuma ya vinara wa ligi, Tottenham Hotspur.
Saka ameanza mechi zote isipokuwa moja ya Ligi Kuu na Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya msimu huu 2023/24.
Kuhusu kuichezea klabu hiyo mechi nyingi Saka amesema: “Nadhani inawezekana. Ukiangalia wachezaji wa juu, wapo kila baada ya siku tatu na wanashinda michezo kwa timu yao.
“Kwa hiyo ninajaribu kuwa katika kiwango hicho, ni wazi kuwa katika kiwango hicho ninahitaji kujishukuru wenyewe.
“Mimi ni mvulana ambaye siku zote nataka kuwa uwanjani, siku zote ninataka kujitolea kwa uwezo wangu wote, na ikiwa nitakuwa majeruhi na lazima nilazimishwe kuwa nje, basi bila shaka nitakaa nje.
“Lakini mradi nipo na niko tayari kucheza, siku zote nitajitolea kwa uwezo wangu wote na kuwaambia kuwa nataka kucheza.”
Lakini kwa mara nyingine tena anaweza kuwa anavaa kitambaa cha unahodha wakati Arsenal itakaposafiri kwenda Newcastle kwenye Ligi Kuu Jumamosi (Novemba 04).
Ameongeza: “Tunakaribia kilele cha jedwali la Ligi Kuu, tuko vinara wa Kundi letu la Ligi ya Mabingwa na bado tuko kwenye mashindano mengine yote.
“Nadhani hilo ni jambo ambalo tunaweza kujivunia, lakini nakubali kuna kiwango kingine cha sisi kwenda mbali zaidi ya hapa.