Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hii hapa Yanga usiyoijua

Yanga Squad Full Hii hapa Yanga usiyoijua

Mon, 24 Jul 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Juzi Yanga, ilihitimisha kilele cha Siku ya Mwananchi katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini, Dar es Salaam.

Hii ni mara ya tano kwa klabu hiyo kufanya tamasha lake pamoja na kuwa na historia kubwa katika soka la Tanzania na Afrika kwa ujumla.

Hata hivyo, vijana wengi wa sasa hawaijui historia ya klabu hii ambayo jina lake la halisi ni Young Africans. Unajua Yanga imetokea wapi?

HISTORIA FUPI YA YANGA

Inaanza tangu mwaka 1910 ingawaje historia inayotambulika zaidi ni kuanzia mwaka 1935.

Yanga ilitokana na vijana wa Mkoa wa Pwani (Sasa Dar es Salaam) waliokuwa wakikutana katika Viwanja vya Jangwani kufanya mazoezi na baadaye wakaunda timu iliyojulikana kwa jina la Jangwani Boys.

Jezi za Jangwani Boys zilikuwa ni nyeupe na nyeusi zikiwa na mfano wa mnyama pundamilia. Lakini Yanga imebaki na rangi nyeusi tu na mwaka 1935 ikaanza kutumia rangi za kijani na njano.

YANGA YA KONDO KIPWATA

Rais wa kwanza ya Yanga aliitwa Kondo Kipwata ambaye alikuwa kati ya watu wa mwanzo waliojiandikisha uanachama wa klabu hiyo.

Mkutano wa kwanza wa Yanga ulifanyika mwaka 1926 katika eneo ambalo hivi sasa ipo Shule ya Sekondari ya Tambaza.

Miongoni mwa yaliyojadiliwa kwenye mkutano huo ni kuiboresha timu hiyo ambayo wachezaji wake wengi walikuwa wafanyakazi wa bandarini na mashabiki wake wengi walikuwa wabeba mizigo bandarini.

YAITWA NAVIAGATION

Baada ya mkutano huo, timu ilibadilishwa jina na kuwa Navigation, iliyotokea kuwa moto wa kuotea mbali katika timu za Waafrika enzi hizo, kabla ya Uhuru wa Tanganyika.

Timu kama Kisutu, Kitumbini, Gerezani na Mtendeni zilikuwa hazifui dafu mbele ya timu hiyo.

Ikiwa inatamba kwa jina la Navigation, wanachama na mashabiki wa timu hiyo walikuwa wanatembea kifua mbele.

SOKA LA ITALIA

Kwa sababu Italia ilikuwa inatamba kwenye ulimwengu wa soka katika miaka hiyo, wanachama wa timu hiyo nao waliamua kuibadilisha jina timu yao na kuiita Italiana.

Italiana FC ilipata mafanikio ya haraka na haikushangaza ilipopanda Ligi Daraja la Pili kanda ya Pwani (Dar es Salaam). Mwanzoni mwa miaka ya 1930 Italiana iliachana na jina lake kabla ya kuingia kwenye ligi hiyo, hivyo ikaanza kujiita New Youngs.

SIMBA ILIZALIWA HAPA

Kila ilipokuwa ikibadilisha jina, ilikuwa ikifanya vizuri zaidi, kwani ikiwa na jina la New Youngs ilitwaa Kombe la Kassum, lililoshirikisha timu mbalimbali za Mkoa wa Pwani (Dar es Salaam).

Mwaka 1935 uwezo wa klabu ulishuka na kusababisha wanachama kutofautiana na kuleta migogoro katika Klabu.

Hali hiyo ilisababisha mgogoro mkubwa wa wanachama ambao baadhi yao walijiengua na kuanzisha klabu nyingine ambayo sasa ndio Simba SC.

Kabla ya kuitwa Simba waliasisi Klabu iliyojulikana kwa jina la Queens FC ambayo baadaye ilibadilisha jina na kuitwa Sunderland na mwaka 1971 ikaitwa Simba Sports Club.

JINA LA YANGA

Baada ya mgawanyiko wanachama waliobaki waliifanyia marekebisho klabu na kubadilisha jina kutoka New Youngs na kuita Young Africans.

Mashabiki wengi walishindwa kutamka jina la Young kwa ufasaha na kusababisha kuzaliwa kwa jina la Yanga kutokana na matamshi.

Viongozi wa Yanga wakiwa pamoja wale wa Simba kabla ya kugawanyika walileta hamasa sana katika nchi na kusaidia kuwaunganisha wananchi kipindi cha kupigania uhuru wa nchi.

Ilifika hatua, Rais wa Kwanza wa Zanzibar ambaye alikuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Tanzania, Abeid Amaan Karume alikuwa akiziangalia kwa jicho la karibu klabu za Simba na Yanga.

Rais Karume alikuwa na mchango katika ujenzi wa klabu hizo, (sana kwa Yanga) ambazo zilikuwa na matawi hadi Zanzibar.

Rais Karume ndiye aliyeweka mawe ya msingi ya klabu zote na kuzifungua.

Karume ndiye aliyetoa jina la Simba ingawaje yeye mwenyewe alikuwa na mapenzi na Klabu ya Yanga.

MANGARA APEWA TIMU

Rais wa kwanza wa Yanga, Mzee Kondo Kipwata hakuwa na elimu kubwa na ilifikia hatua mwishoni mwa miaka ya 60 alimwachia uongozi Mangala Tabu Mangala. Lengo la kumwachia Mangala ilikuwa asimamie ujenzi wa jengo la klabu hiyo lililopo Mtaa wa Twiga na Jangwani, kisha Kipwata arejee madarakani.

Yanga ilikuwa na maendeleo kwa kuwa na jengo na magari yake, yakiwemo mabasi.

MABASI YA YANGA

Yanga ndio timu pekee iliyokuwa ikimiliki mabasi matano. Baadhi ya mabasi hayo yalikuwa yakitumika kusafirisha wachezaji kwenda sehemu mbalimbali kwa ajili ya kucheza mechi.

Basi la kwanza lilikuwa ni Isuzu lililokuwa na uwezo wa kuchukua watu 19. Hili lilikuwa na rangi za pundamilia.

Pia, kulikuwa na Isuzu lililotengenezwa kwa staili ya Amigo, hili lilikuwa na uwezo wa kuchukua watu 18. Pia, Yanga ilimiliki Isuzu Min- Bus lililokuwa na uwezo wa kuchukua watu 28, lilitumiwa sana na wachezaji. Yanga pia ilimikili basi aina ya Isuzu lililokuwa na uwezo kuchukua watu 65 ambalo walikuwa wakisafiri nalo mikoani.

Mwaka 1974 Yanga ilinunua basi lingine aina ya Ford baada ya ubingwa ilipoifunga Simba 2-1 katika Uwanja wa Nyamagana.

Basi hili liliandikwa ukombozi baada ya kukomboa ubingwa kutoka kwa watani zao. Yanga ilikuwa na gari aina ya Honda ambayo ilikuwa inatumiwa na Kocha Tambwe Leya.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: