Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hii haina kujuana! Bato kali Ligi Kuu msimu 2024/25

Ghasia Ligi Kuuuu Hii haina kujuana! Bato kali Ligi Kuu msimu 2024/25

Mon, 22 Jul 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Ghasia za usajili kwa klabu zote 16 za Ligi Kuu Bara ndizo ambazo zinaendelea kwa wakati huu ambao ni maalum kwa ajili ya kufanya hivyo na pazia lake linatarajiwa kufungwa Julai 31, mwaka huu kama ambavyo ilibainishwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

Katika wakati huu viongozi wote wa timu wanakuwa bize katika kusaka wachezaji wale ambao wameambiwa na mabenchi yao ya ufundi kwa ajili ya kuviimarisha vikosi vyao na kufanya vizuri katika msimu ujao ili kuwapokonya ubingwa Yanga ambao walitwaa msimu uliopita.

Muda huu viongozi huzunguka ndani na nje ya mipaka ya Tanzania kwa nia moja tu kusajili wachezaji kama ambavyo walielekezwa na mabenchi yao ya ufundi juu ya wapi na wapi wasajili.

Mishe za kusaka malisho bora kuna muda huwafanya wachezaji wa timu moja kujikuta wamesajiliwa katika timu moja na wakati mwingine hujikuta wameangukia katika timu pinzani kwenye ligi moja.

Jambo hilo hutokea hata kwa wale marafiki waliokuwa wameshibana ndani ya timu moja wakawa wapinzani wakubwa kiwanjani kwa kuwa kila mmoja alihamia sehemu nyingine baada ya kutoka timu moja ambayo iliwafanya kuwa kitu kimoja.

Sasa kutokana na usajili huu unaoendelea nchini tarajia kuona wachezaji ambao walikuwa katika ligi au timu moja wamesajiliwa katika timu tofauti za Ligi Kuu Bara ambazo zitawafanya wakikutana wawe kama hawafahamiani kwa muda kwa sababu kila mmoja atakuwa bize kuitetea timu yake.

TRA BI TRA vs AHOUA

Zote ni sura ngeni katika Ligi Kuu Bara kwa kuwa ndiyo zimesajiliwa, lakini ni watu ambao wanafahamiana kwa kuwa wametoka katika Ligi Kuu Ivory Coast.

Hawa ni beki Anthony Tra Bi Tra ambaye amesajiliwa na Singida Black Stars ambayo inanolewa na kocha Mholanzi Patrick Aussems ‘Uchebe’ na aliyekuwa Mchezaji Bora wa ligi hiyo kwa msimu ulioisha, Jean Charles Ahoua aliyesajiliwa na Simba akitokea Stella Club d’Adjame.

Bato lao hawa linatarajiwa kuendelea tena kwenye ardhi hii ya Julius Nyerere kwa kuwa timu walizohamia zina upinzani mkubwa zikikutana ikiwa ni baada ya kuwa na vita nzito tangu msimu uliopita kule kwao.

BOKA vs NOUMA

Wawili hawa wana stori ya kufurahisha sana. Wenyewe kila mmoja kaja kivyake hapa nchini lakini wakiwa wametoka katika timu moja kule DR Congo, FC Lupopo na wakiwa wanacheza nafasi moja ya mlinzi wa kushoto.

Hapa kuna Chadrack Boka ambaye katua zake Yanga na Valentin Nouma aliyekuja kuimarisha ulinzi ndani ya Simba, ila wote walikuwa marafiki wakubwa kule Lupopo ambako walikuwa wakipishana kuicheza nafasi hiyo ya mlinzi wa kushoto.

Ila hapa kila mmoja itabidi aweke ‘sura ya mbuzi’ atakapokutana na mwenzake kwenye Kariakoo Derby kwa ajili tu ya kuitetea klabu yake iweze kupata matokeo mazuri mbele ya mwenzake.

RUPIA vs ABUYA

Uwezo wa juu aliouonyesha akiwa na Ihefu (Singida Black Stars sasa) ndiyo ambao uliwatoa udenda mabosi wa Yanga na kumvuta kwenye timu yao ili awe sehemu ya kikosi kwa msimu ujao. Huyo ni winga Mkenya, Duke Abuya ambaye kabla ya kuja Yanga alikuwa anaunda pacha nzuri tu na straika Elvis Rupia pale Singida Black Stars ila baada ya kuondoka ni wazi kwamba watakapokutana kutakuwa hakuna kujuana kwa sababu kila mmoja atazihitaji pointi tatu za mwenzake.

ANDAMBWILE vs KAGOMA

Miezi miwili nyuma viungo hawa wawili walikuwa katika kundi moja la WhatsApp la Singida Fountain Gate na wakiwa marafiki wa karibu tu kwa kuwa wote walikuwa wanacheza eneo moja uwanjani.

Lakini kila mmoja sasa ‘ameleft’ kundi lile la Singida na Yusuph Kagoma yeye kajiunga na kundi la Simba ambalo kasajiliwa huko huku mwenzake, Aziz Andambwile akiwa kundi la Yanga ambako naye kamwaga wino huko Jangwani.

Kagoma ndiye ambaye alikuwa akihusishwa na Yanga tangu msimu uliopita lakini kaenda kwa wapinzani wao hivyo atakapokutana na Andambwile yeye atakuwa na ‘usongo’ wa kutaka kuwaonyesha waajiri wake, Yanga kwamba hawakukosea kumsajili yeye mbele ya mwenzake hiyo.

LUSAJO vs ADAM

Wenyewe walikuwa wakiunda pacha ya ushambuliaji pale kwa Watanganyika, Mashujaa FC ya Kigoma kabla ya msimu kumalizika na kila mmoja kushika njia yake.

Adam Adam katua kwa matajiri wa Dar, Azam FC ambao watashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao wakati pacha wake, Reliants Lusajo mwenyewe kashika njia na kwenda makao makuu ya nchi pale Dodoma Jiji FC. Hivyo ni wazi wakikutana watasahau yale matukio mazuri ya kuwekeana pasi za mabao kule Mashujaa na kila mmoja akili yake itawawazia ushindi mbele ya mpinzani wake.

MANYAMA vs DUBE

Prince Dube ndiye alikuwa mchezaji wa pili kusajiliwa na Yanga katika dirisha hili la usajili akiwa mchezaji huru baada ya kumalizana na Azam FC ambao alivunja nao mkataba.

Dube moja kati ya watu ambao alikuwa anaonana nao sana pale Azam FC ni beki, Edward Charles Manyama ambaye naye kama ilivyo kwa straika huyo baada ya msimu kuisha ameondoka na kutua Singida Black Stars.

Wenyewe hawatakuwa na kujuana timu zao zitakapokutana kwenye ligi au mchezo wowote kwa kuwa Dube lengo lake ni kuifungia Yanga mabao wakati Manyama lengo lake ni kuzuia Singida isiruhusu bao.

MUTALE vs CHAMA

Mafanikio ya Chama ndani ya Simba tangu alipojiunga na timu hiyo misimu kadhaa nyuma kwa kiwango kikubwa yamechangia kuwashawishi Wazambia wengi kuja ndani ya Simba kama ilivyo kwa Moses Phiri na Joshua Mutale aliyesajiliwa sasa.

Wenyewe hawatakuwa na kujuana kwa sababu ya upinzani uliopo baina ya timu zao, Chama akiwa Yanga na Simba akiwa na Simba watakapokutana kwenye Kariakoo Dabi.

Utamu zaidi juu ya nyota hawa ni Wazambia wanaotesa katika vikosi vya timu ya taifa, hivyo wanajuana kiuchezaji, lakini huenda katika mechi baina ya timu hizo watafungiana vioo ili kila mmoja kutengeneza heshima kwa klabu anayoichezea kwa sasa. Na hilo linaweza kuonekana katika Dabi ya Kariakoo itakayopigwa Agosti 8 Kwa Mkapa wakati wa mchezo wa Ngao ya Jamii. Ngoja tuone!

Chanzo: Mwanaspoti