Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hii Yanga ya Gamondi tutalaumu wapinzanzi bure

Yanga 2 0 Singida Hii Yanga ya Gamondi tutalaumu wapinzanzi bure

Sun, 29 Oct 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Kuna watu wanateseka kwa vita. Kuna watu wanateseka kwa njaa. Kuna watu wanateseka na magonjwa. Mateso ni mengi sana. Halafu kuna watu wanateseka na Yanga.

Ndio. Leo nitazungumzia hawa wanaoteseka na Yanga. Sitazungumza wale wanaoteseka Ukanda wa Gaza au Ukraine. Hawa Mungu atawasaidia.

Nataka nizungumze hawa wanaoteswa na hii Yanga ya Miguel Gamondi. Ni wapinzani wa Yanga msimu huu.

Wana hali ngumu sana. Kuna mechi za Ligi Kuu, halafu kuna mechi dhidi ya Yanga. Kucheza dhidi ya Wananchi katika zama hizi za Gamondi ni mateso makubwa.

Gamondi ameingia Yanga katika nyakati ngumu kama kocha. Ameingia wakati Yanga imetoka kupata mafanikio makubwa.

Ilitwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara na ule wa Kombe la Shirikisho la Azam. Ikafika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa mara ya kwanza katika historia.

Yanga ya ‘Profesa’ Nasreddine Nabi ilifanya kila kitu ilichojisikia. Ikaweka rekodi ya kucheza Ligi Kuu Bara michezo mingi bila kupoteza. Ikaweka rekodi ya kushinda mechi mfululizo. Hii ndio Yanga ya Nabi.

Ukiwa kama kocha mpya katika timu iliyotoka kupata mafanikio makubwa kama haya ni jambo gumu.Unakwenda kuwapa kitu gani cha tofauti?

Bahati mbaya kwa Gamondi ni kwamba wakati anaingia Yanga, aliyekuwa staa wa timu hiyo, Fiston Mayele akauzwa kwenda Pyramids ya Misri.

Unaingia kwenye timu ambayo straika ni Clement Mzize na Kennedy Musonda. Halafu wanaingia sokoni na kumnunua Hafidh Konkoni. Mchezaji mzito kama kiroba cha mahindi.

Kama kocha ni mtihani mzito. Lakini kwa Gamondi ni mtihani ambao amekwenda kuushinda kwa muda mfupi.

Ndani ya miezi michache Wananchi wamewasahau Nabi na Mayele. Kwanini? Kwa sababu ya soka la Gamondi.

Yanga inacheza mpira mzuri. Yanga inacheza soka la kikatili. Yanga inawatesa wapinzani. Yanga ya Gamondi.

Kuna vitu vingi ambavyo Gamondi amevibadili kwa Wananchi. Kwanza ameweka nidhamu kubwa ya mchezo. Wachezaji wanaheshimu mechi zote.

Haijalishi Yanga inacheza na JKT Tanzania au Azam FC itacheza vilevile. Kila mchezaji anakaba na kushambulia. Inacheza zaidi kama timu.

Gamondi ameondoa utegemezi wa mchezaji mmoja kwenye timu. Yanga ya sasa unaweza kufungwa na mchezaji yeyote.

Ndio sababu utaona kule Mwanza dhidi ya Geita, staa alikuwa Pacome Zouzoua. Mechi dhidi ya Azam FC staa akawa Stephane Aziz Ki. Dhidi ya Singida Big Stars staa akawa Maxi Nzengeli.

Hii ndio Yanga ya Gamondi. Ni hatari ikiwa na mpira. Ni katili sana pindi inavyotafuta mpira. Haiwapi wapinzani nafasi ya kupiga pasi nyingi. Wanakaba kwa pamoja kama mbwa mwitu.

Kila mchezaji wa timu pinzani anaposhika mpira, mbele yake ataona wachezaji watatu ama wanne wa Yanga. Mwisho wa siku anatoa boko. Anajikuta amepiga nje au amewapasia wapinzani wake.

Hakuna jambo gumu kama kucheza na timu ambayo inakaba kama Yanga. Huwezi kupata muda wa kujenga mashambulizi dhidi yao. Labda uwe na wachezaji mahiri sana.

Yanga ikipokonya mpira inashambulia kwa kasi kubwa. Wachezaji wanakimbia katika nafasi. Wanafungua ngome za wapinzani kirahisi. Wanafunga mabao.

Hatari zaidi kwa Yanga ni kwamba ina wachezaji wengi wazuri kwenye kupiga mashuti ya mbali. Pacome anapiga. Aziz Ki anapiga. Maxi anapiga. Ni hatari kuwazuia watu wote hawa.

Kubwa zaidi ni kiwango cha utimamu wa mwili kwa wachezaji wa Yanga. Wako fiti kwelikweli. Wanakimbia bila kuchoka kwa dakika zote 90.

Ni timu chache tu kwenye ligi yetu zinaweza kucheza kwa kiwango hicho cha utimamu wa mwili kwa dakika zote.

Ni ngumu sana lakini Yanga wameweza.

Uzuri zaidi kwa Yanga ni kwamba Gamondi ametengeneza

wachezaji kama 20 kwenye timu yake ambao wanaweza kumpa ubora unaokaribiana.

Ndio sababu dhidi ya Singida Big Stars alipocheza Zawadi Mauya watu wengi hawakugundua kuwa Khalid Aucho hayupo. Kwanini? Kwa sababu Mauya alicheza kwa ubora wa juu.

Alipotoka Mudathir Yahya na kuingia Sure Boy hakuna aliyetambua. Kwanini? Kwa sababu Sure Boy alicheza katika kiwango bora pia. Ndio Yanga ya Gamondi.

Nyakati hizi wapinzani wa Yanga wanaendelea kuteseka tuwaonee huruma badala ya kuwabeza. Ni ngumu sana kucheza dhidi ya Yanga kwa sasa.

Acha tuone wikiendi ijayo Simba atatupatia picha gani kwa Yanga hii. Ila itakuwa mechi ngumu sana. Timu zote ziko vizuri. Yanga inacheza soka safi. Simba iko vizuri kwenye mbinu zake. Inashinda mechi zake. Acha tuone.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: