Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hesabu za uhakika Simba robo fainali ni hizi

Simba Scaled Hesabu za uhakika Simba robo fainali ni hizi

Sat, 24 Feb 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Matokeo ya sare tasa ugenini dhidi ya ASEC Mimosas ya Ivory Coast jana kwenye Uwanja wa Felix Houphet Boigny yameipa Simba kazi rahisi ya kufanya katika mechi inayofuata dhidi ya Jwaneng Galaxy kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Machi 02, mwaka huu ili iweze kutinga hatua ya robo fainali ya mashindano hayo.

 Licha ya mwanzo mbaya ambao ilikuwa nao kwenye hatua ya makundi ambapo ilitoka sare mbili mfululizo, Simba sasa ipo kwenye nafasi nzuri ya kufuzu robo fainali baada ya mchezo dhidi ya ASEC jana.

Simba sasa inahitajika kupata ushindi tu katika mechi dhidi ya Jwaneng Galaxy ambayo itakuwa ya mwisho kwao kwenye hatua ya makundi ili iweze kusonga mbele.

Pointi moja ambayo Simba imevuna jana, imeifanya ifikishe pointi sita na kushika nafasi ya pili kwenye kundi B ambalo linaongozwa na ASEC Mimosas yenye pointi 11 huku Jwaneng Galax ikiwa nafasi ya tatu na pointi zake nne na Wydad ikiwa nafasi ya mwisho na pointi tatu.

Endapo Jwaneng Galaxy itaifunga Wydad leo, itafikisha pointi 7 na kupanda nafasi ya pili katika msimamo huku ikiongeza chachu ya Simba kushinda mechi yake ya mwisho kwa Mkapa. Kama itapata ushindi dhidi ya timu hiyo ya Botswana, itasonga mbele kwa vile itafikisha pointi tisa ambazo haziwezi kufikiwa na Jwaneng wala Wydad.

Kama Wydad itashinda leo, itafikisha pointi sita lakini haiwezi kufuzu ikiwa Simba itaifunga Jwaneng Galaxy kwenye mechi ya mwisho hata kama yenyewe itaifunga ASEC Mimosas kwa vile zote zitamaliza zikiwa na pointi tisa, lakini Simba itasonga mbele kwa kubebwa na kanuni ya kuangalia timu gani ilipata matokeo mazuri pindi timu mbili zilipokutana ili kuamua mshindi.

Simba inabebwa na matokeo mazuri iliyopata katika mechi mbili dhidi ya Wydad kwenye kundi hilo kwani, mechi ya kwanza ugenini ilipoteza kwa bao 1-0 na ikapata ushindi wa mabao 2-0 nyumbani.

Meneja Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally alisema kuwa baada ya sare ya jana, nguvu zao wanazielekeza katika mechi ya Jwaneng Galaxy.

"Alhamdullilah tumepata tulichokihitaji. Sasa kazi imebaki mikononi mwetu Wanasimba Machi 2, dhidi ya Jwaneng, hiyo ni mechi ya kuipeleka timu yetu robo fainali," alisema Ahmed Ally.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live