Leo saa 1:00 usiku, timu ya Young Africans SC itakuwa Dimba la Azam Complex, Dar es Salaam kusaka pointi tatu dhidi ya Kagera Sugar ukiwa ni mchezo wa Ligi Kuu ya NBC.
Ni mchezo ambao umebeba pointi za ubingwa kwetu kutokana na hesabu zilivyo hivi sasa zikisalia mechi tano.
Katika mechi tano zilizosalia, Young Africans inahitaji pointi nane pekee kuwa mabingwa, hivyo ushindi wa leo utatufanya tubakiwe na pointi tano za kuuendea ubingwa.
Young Africans ipo kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya NBC ikiwa na pointi 65, pointi nane zikipatikana zitwakua 73 ambazo haziwezi kufikiwa na wapinzani, hivyo ubingwa utakuwa wetu ambao ni wa 30 na wa tatu mfululizo.
Kocha Mkuu wa Young Africans SC, Miguel Gamondi, amesema licha ya wengi kuona timu ina nafasi kubwa ya kubeba ubingwa, lakini kwake na wachezaji wanaheshimu kila mpinzani, hivyo hawatabweteka bali wataendelea kupambana hadi mwisho.
Katika mchezo wa mzunguko wa kwanza tuliocheza ugenini dhidi ya Kagera Sugar matokeo yalikuwa 0-0, huku rekodi yetu dhidi yao kwenye michezo mitano iliyopita, tumeshinda nne na sare moja.