Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hesabu ni kali Ligi Kuu Bara

Azizi Ki Stephen Leo Machi.jpeg Kiungo Mshambuliaji wa Yanga, Stephen Aziz Ki

Sun, 12 Mar 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Vinara wa Ligi Kuu Bara, Yanga itashuka uwanjani jioni ikiwa na hesabu kali katika mbio za ubingwa wa ligi wakati ikiikabili Geita Gold kwenye moja ya michezo mitatu inayopigwa leo nchini.

Watetezi hao wa ligi hiyo, itakuwa Uwanja wa Azam Complex, jijini Dar es Salaam kuanzia saa 12:15 jioni kuikaribisha Geita, huku mapema saa 10:00 jioni Coastal Union na Singida Big Stars zitaumana Uwanja wa Mkwakwani, Tanga na saa 2:30 usiku itakuwa ni zamu ya Dodoma Jiji na Polisi Tanzania.

Mechi hiyo ya usiku itapigwa kwenye Uwanja wa Jamhuri Dodoma, huku mtihani mkubwa ukiwa kwa Polisi inayoburuza mkia baada ya kuachiwa msala na Ruvu Shooting ambao juzi ilishinda 2-1 mbele ya Mbeya Citya na kuchupa kwa nafasi moja kwenye msimamo wa ligi hiyo.

Licha ya kuwepo kwa mechi hizo tatu, lakini macho na masikio yapo zaidi kwenye pambano la Chamazi, hii ni kutokana na ukweli ni moja kati ya mechi nne ambazo zimeshikilia hatma ya Yanga kwa msimu huu kumaliza kazi mapema kwa kutetea taji hilo kama itashinda zote kabla ligi haijaisha.

Kwa sasa Yanga ina pointi 62 baada ya mechi 23 na kama itashinda mechi hizo ikiwamo dhidi ya Simba itakayopigwa Aprili 16, ifafikisha jumla ya pointi 74 ambazo hazitaweza kufikiwa na timu yoyote, kwani watani wao watamaliza msimu na pointi zisizozidi 72 (kabla ya mechi yao ya jana).

Yanga itashuka uwanjani ikiwa na hesabu za kutotaka kudondosha pointi yoyote mbele ya Geita ikijua fika kosa la kutema pointi hata moja itatibua mipango yao ya kuliwania taji la 29 la ligi hiyo.

Ikichangizwa na ushindi wa 2-0 wa mechi ya kimataifa dhidi ya Real Bamako ya Mali, Yanga itashuka uwanjani na mzuka huohuo kuhakikisha inabakiza pointi tatu nyumbani.

Kikosi hicho cha Kocha Nasreddine Nabi kwa sasa mzuka wao upo juu baada ya mfumo wa 4-3-3 kuwa na neema ikishinda mechi zake za hivi karibuni ambapo kocha huyo amekuwa akiwatumia washambuliaji wao wawili Fiston Mayele, Kennedy Musonda na winga mmoja kufunga mabao.

Katika mechi zake 10 za ligi zilizopita Yanga hakuna mchezo ambao wamemaliza bila kupata bao huku ikishinda mechi zote hizo hali ambayo inaiweka katika nafasi kubwa kuendelea kufanya vizuri.

Kocha wa Nabi, alisema kuelekea mchezo huo Yanga haina mechi rahisi na kwamba wanajua ubora wa Geita lakini hesabu zao ni kuendeleza ushindi mbele ya wachimba madini hao.

"Hakuna mchezo rahisi kwetu Yanga, tumekuwa na hesabu Kali kwa kila mchezo ulio mbele yetu, ukiwaangalia Geita utajua kwamba hautakuwa mchezo rahisi kwa kuwa bado wana ubora mkubwa na wana kocha mzuri," alisema Nabi na kuongeza;

"Tunaweza kuwa na mabadiliko madogo lakini tutaingia kwenye mchezo huu tukiwa na akili moja ya kuhakikisha tunashinda nyumbani ili kubaki kwenye malengo yetu."

Geita iliyowasili mjini juzi itaingia na hesabu za kutaka kulipa kisasi kwa kufungwa na Yanga kwa bao 1-0 katika mchezo wa duru la kwanza na pia kushindwa kutoka na ushindi mbeye ya mabingwa hao wa Tanzania tangu wapande daraja msimu uliopita. Katika mechi za msimu uliopita Geita ilipigwa nje ndani kwa bao 1-0 mtawalia, kitu ambacho kocha Fred Felix 'Minziro' alisema safari hii watawakabili wapinzani wao hao kwa akili zaidi ili kufuta uteja huo.

Timu hiyo inakutana na Yanga ikitokea mkoani Lindi ilikopoteza kwa mabao 2-1 mbele ya Namungo na kocha Minziro alisema wataingia kwenye mchezo huo kwa tahadhari kubwa kwa kutambua ubora wa wenyeji wao wanaoshikilia rekodi ya kushinda mechi 10 mfululizo katika Ligi Kuu Bara kwa sasa.

"Hatuna maana labda tunawahofia Yanga, lakini lazima tutambua ubora walionao kwasasa, tutaingia na mpango mzuri utakaotubeba kwanza tuwazuie kucheza kwa ubora wao lakini baada ya hapo tutafunde ushindi," alisema Minziro, staa wa zamani wa Polisi Zanzibar, Yanga na Taifa Stars.

Katika Uwanja wa Mkwakwani, Tanga, wenyeji Coastal watawakaribisha Singida Big Stars katika mchezo mwingine wenye hesabu kali kwa matajiri wa Singida.

Singida inajua Coastal iliwadhalilisha nyumbani katika mchezo wa kwanza baada ya kuchapwa 2-1 lakini wanatambua wakiwa ugenini bado wamekuwa wakikosa utulivu kama ambavyo wanapokuwa nyumbani.

Wenyeji baada ya kushinda mechi mbili zilizopita, leo inahitaji ushindi mwingine kabla ya kutoka kufuata Dodoma Jiji kwenye mchezo ujao lakini wakitambua kwamba watakutana na Singida inayohitaji ushindi ili kuingia katika tatu bora wakikimbizana na Azam FC.

Jijini Dodoma nako wenyeji Dodoma Jiji itakuwa na mchezo mgumu dhidi ya Polisi inayopigana na roho yake ili isishuke daraja wakiwa chini ya msimamo kabisa.

Matokeo ya kupoteza kwa Polisi yatazidi kuiweka pabaya katika janga la kushuka daraja, lakini inajua Dodoma nao bado gari yao haijatulia ikiwa katika nafasi ya 13 huku pia wakipoteza mechi zao mbili zilizopita bado wako kwenye presha ya kutafuta ushindi ili kuituliza timu hiyo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: