Rais wa Klabu ya Yanga, Eng. Hersi Said amesema kuwa mbinu waliyoitumia kuwafunga watani zao Simba SC bao 5-1 kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya NBC ndiyo walioutumia na kuutekeleza kumsambaratisha Mwarabu, CR Belouizdad kwa bao 4-0 juzi katika Dimba la Mkapa.
Hersi amesema hayo wakati akiwapongeza wachezaji na benchi lake la ufundi kufuatia matokeo mazuri waliyopata Yanga juzi, Februari 24, kwa kuifunga CR Belouizdad na kutinga hatua ya robo fainali ya CAFCL wakiwa na mchezo mmoja mkononi, na kuvunja rekodi yao ya miaka zaidi ya 52 iliyopita kufika hatua hiyo.
"Kwa niaba ya uongozi wa Yanga, ninawashukuru kocha na benchi lake la ufundi, wachezaji, tunatambua na kuthamini kitu kikubwa mlichokifanya, asanteni sana.
"Kitu kilichotokea ni kwamba, wakati juzi tunafanya mazoezi ya mwisho tulisema lazima tushinde hii mechi, lakini katika kushinda, kuna motivation flani ambayo tuliitumia kwenye mchezo dhidi ya Simba na tukashinda magoli mengi (5-1).
"Nikawaambia tukishinda hii mechi Wanangu bado tunalazimika kwenda Misri kutafuta matokeo ya sare. Lakini kutokana na sheria ya mashindano haya, wataangalia timu ambayo imepata alama sawa, wataangalia matokeo ya head to head na sio tofauti ya jumla ya mabao ya kufunga na kufungwa.
"Kwa hiyo tukaja na falsafa flani ambayo ilikuwa inaendanana Falsafa na Novemba 5, 2023, siwezi kuisema. Nikawaambia kwa hiyo tushinde lakini tukiifuata ile falsafa, tunaweza kushinda bao 4 tunaweza kufuzu tukiwa hapa hapa Tanzania.
"Basi wakaenda wakatekeleza yale maneno na waliotekeleza ni hawa wanajeshi. Tunajivunia kazi kubwa mlioifanya, asanteni sana," amesema Hersi.