Rais wa Klabu Bingwa Tanzania Bara Young Africans Injinia Hersi Said amesema hakuwahi kufikiria kama siku moja katika maisha yake ataweza kuwa kiongozi mkubwa wa Klabu hiyo kongwe katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Hersi aliingia madarakani mwaka jana 2022 akichukuwa nafasi ya Mshindo Msolla ambaye alimaliza kipindi cha Uongozi wake, kilichodumu kwa miaka minne kwa mujibu wa katiba ya Young Afrcans.
Akizungumza na Clouds FM mapema leo Jumatano (Mei 24) Injinia Hersi amesema ni kweli kwa muda mrefu alikuwa Shabiki wa Young Africans, lakini hakudhani kama angeweza kuwa kiongozi wa ngazi ya juu.
Amesema matukio kadhaa ambayo yaliwahi kutokea klabuni hapo na kupelekea baadhi ya mambo kutokwenda sawa, ndio yalimchochea kutamani kuwa kiongozi na bahati nzuri alifanikiwa kuwashawishi Wanachama na wakamchagua.
“Sikuwahi hata kuwaza kama kuna siku nitakuwa kiongozi wa klabu kubwa ni kitu ambacho kimetokea kutokana na mfululizo wa matukio ambayo yamefanya leo nimekuwa kiongozi wa Young Africans”
Kuhusu Historia yake hadi kuwa Shabiki na Mwanachama wa Young Africans, Injinia Hesri amesema mzazi wake alikuwa kichocheo kikubwa cha kujiingiza kwenye ushabiki wa klabu hiyo tangu mwaka 1992.
“Young Africans nimekuwanayo kwa muda mrefu! Nakumbuka 1992 Mzee wangu alikuwa anasikiliza mpira kwenye Radio, hapo ndio niligundua kuwa Mzee wangu alikuwa Shabiki wa Young Africans na baada ya hapo ndio nikawa shabiki wa Young Africans, baadae nikawa mwanachama, baada ya hapo GSM ilipoingia katika uwekezaji na Young Africans ndipo nikapendekezwa kuwa Rais wa klabu.” amesema Hersi
Katika kipindi cha Uongozi wake, Injinia Hersi Said amekuwa kiongozi aliyepata mafanikio makubwa tangu kuanzishwa kwa klabu hiyo, kwani amefanikisha timu ya Young Africans kutinga Fainali ya Michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika kwa mara ya kwanza.
Young Africans itacheza mchezo wa Mkondo wa Kwanza wa Fainali Kombe la Shirikisho Barani Afrika Jumapili (Mei 28) katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, kisha itakwenda mjini Algiers-Algeria kwa ajili ya mchezo wa Mkondo wa Pili utakaopigwa Juni 03.